Kamati ya Taifa ya Ushauri wa Tafiti za Mazingira (Environmental Research Adivisory Committee - ERAC) yakutana mkoani Morogoro kufanya mapitio na kupitisha Rasimu ya Mwongozo wa Tafiti za Mazingira (National Environmental Research Agenda - NERA) kupitia kikao chake cha siku mbili tarehe 29 na 30, Januari 2026 katika ukumbi wa mikutano wa EDEMA.
Akizungumza Mkurugenzi wa Usimamizi na Tafiti za Mazingira (DERM) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Menan Jangu wakati wa ufunguzi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema mazingira ni suala mtambuka hivyo Mwongozo huu wa Tafiti za Mazingira ni muhimu sana katika kupata taarifa sahihi ambazo zinasaidia katika kufanya maamuzi juu ya maendeleo endelevu nchini.
Dr. Menani alifafanua kuwa “Ustawi wa Maisha yetu ya kila siku,, Uchumi wetu na masuala mbalimbali ya kijamii yanategemea afya ya mazingira; hivyo utunzaji wa mazingira yanatoa uhakika wa afya ya jamii lakini pia maendeleo endelevu ya shughuli za kila siku.Aidha, alifafanua kuwa ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 ni lazima kuwa na miongozo sahihi wa Tafiti za Mazingira ambayo itapatikana kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
“Dira inatekelezwa kwa kuwa na miongozo au nyenzo mbalimbali ikiwemo suala zima la utafiti wa mazingira kupitia Agenda ya mazingira."Aidha, alifafanua kuwa kamati hii inaundwa na wataalam wabobevu kutoka katika Taasisi za Elimu ya Juu, Wizara, Idara za serikali, kutoka katika sekta binafsi na mashirika yasiyo ya serikali; hivyo ni matarajio Rasimu ya Agenda inayojadiliwa itakuwa na uzito wa kipekee na kuwa nyezo sahihi katika utekelezaji wa Dira 2050.
Akizungumza Meneja wa Tafiti za Mazingira ambaye pia ni Mratibu wa Agenda ya Taifa ya Tafiti za Mazingira, Dkt. Rose Mtui amesema Agenda hiyo inatarajiwa kutolewa mwaka huu 2026 na huwa inadumu kwa kipindi cha miaka mitano kabla ya kupitiwa upya kwa lengo la kuingiza mambo mapya yanayojitokeza au mabadiriko ya sera na sharia mbalimbali.Alibainisha kuwa, Rasimu ya agenda hii imetengenezwa kwa kuzingatia mambo mengi ikiwemo masuala mapya kama vile Uchumi wa Blue, Mabadiliko ya tabia nchi, Tekinolojia mpya (AI), changamoto ya utupaji holela wa plastiki, Kelele na Mitetemo nk. Pia Rasimu ya agenda imezingatia mambo mbalimbali ya Kisera, Dira ya Taifa, ilani ya Uchaguzi nk. Aidha, alisema kuwa rasimu hii imepitia gazi mbalimbali ambapo wadau walipata fulsa ya kupitia agenda iliyopita (NERA 2017-2022) na kufanya tathmini ya utekelezaji wa Agenda hiyo na kuibua mambo mapya ambayo yanatakiwa kuwekewa vipaumbele.