NEMC TANZANIA
Mazingira yetu, Uhai Wetu
𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲
KAMATI YA NEMC@40 YAKABIDHI TAARIFA YA MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA NEMC
📌Yamshukuru Dkt. Semesi kwa kuwaamini na kuwateua kuratibu Maadhimisho hayo
Kamati ya Maadhimisho ya Miaka 40 ya NEMC ambayo ilihusika katika maandalizi ya sherehe hiyo ambayo kilele chake kilikuwa Mei 28 na 29, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), imekabidhi taarifa ya Maadhimisho hayo kwa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi leo Agosti 19,2026.
Akizungumza wakati wa kukabidhi taarifa hiyo ya Maadhimisho, Mwenyekiti wa Kamati ya NEMC@40 Bi. Juliana Masawe ambaye pia ni Afisa Utumishi Mkuu wa NEMC amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi kwa kuiamini Kamati hiyo na kuipa jukumu hilo kubwa la kihistoria nchini.
Bi. Juliana amesisitiza kuwa kila kilichofanywa na Kamati hiyo ni kupitia maono ya Dkt. Semesi yaliyowarahisishia kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi na weledi na kufanya Maadhimisho hayo kufanikiwa kwa viwango vya juu.
Akipokea taarifa hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi ameishukuru Kamati hiyo kwa kutomuangusha katika kutekeleza jukumu hilo na amewataka kuendelea kuwa mfano bora kwa wengine katika kutekeleza majukumu wanayopangiwa.
Kamati ya NEMC@40 ilikuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Juliana Masawe, Katibu Paul Kalokola, Wajumbe ni Tajiri Kihemba, Albert Mgoye, Roselyne Mayowa, Rahim Kantinga, Upendo Mtunguja, Cecilia Douglas, Fredrick Mulinda, Shukrani Haule, Elibariki Bajuta na Mosses Nonga.
NEMC YASHIRIKI WARSHA YA MAPITIO YA RASIMU YA UHIMILIVU DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika Warsha ya Wadau inayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 17 hadi 20 Agosti 2026. Warsha hiyo imeandaliwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia Mradi wa Barabara kwa Ujumuishaji na Fursa za Kijamii na Kiuchumi (RISE).
Warsha hiyo inalenga kufanya mapitio na uboreshaji wa Rasimu ya Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Uhimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi (NCCR-AP) pamoja na Miongozo ya Utekelezaji kwa Sekta ya Barabara nchini Tanzania.
Lengo kuu la warsha ni kukusanya maoni na michango kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuboresha nyaraka hizo na kuhakikisha zinatoa mwongozo madhubuti wa kuimarisha uhimilivu wa miundombinu ya barabara dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania.
NEMC YAUNGA MKONO MAAGIZO YA MKUU WA MKOA KUHUSU TAKA SIFURI
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, kuhusu utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa katika Kata za Chamazi na Toangoma, Meneja wa Kanda ya Temeke wa NEMC, Bw. Abel Sembeka, alisema NEMC inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutenganisha taka katika chanzo na kuhakikisha taka zinazoweza kurejelezwa, kama plastiki, karatasi, vyuma na vioo, zinakusanywa na kupelekwa kwa wachakataji badala ya kutupwa ovyo.
Ameongeza kuwa maagizo hayo yanaendana na juhudi za Serikali za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama na endelevu, huku jamii ikihamasishwa kupunguza uzalishaji wa taka, kutenganisha taka katika vyanzo na kuimarisha urejelezaji wa taka ili ziweze kutumika tena kama malighafi na fursa ya kiuchumi ndani ya mzunguko wa uchumi wa kijani
NEMC imeahidi kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Manispaa ya Temeke na wadau wengine wa Mazingira katika kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Taka Sifuri, hususan katika kuongeza uelewa wa jamii kuhusu urejelezaji na matumizi ya taka kama rasilimali, kwa lengo la kupunguza taka zinazopelekwa dampo na kujenga Dar es Salaam safi na yenye mazingira endelevu.
NEMC KANDA YA KUSINI YATOA ELIMU YA UHIFADHI WA MAZINGIRA - MTWARA
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kanda ya Kusini limetoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa jamii ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, tarehe 15 Agosti 2026, kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, wajibu wa jamii katika uhifadhi wa mazingira na fursa za kiuchumi zinazotokana na usimamizi endelevu wa mazingira katika Mkoa wa Mtwara na mikoa jirani.
Elimu hiyo imetolewa kwa wananchi kupitia Dira Mpya Group na Star Women, vikundi vinavyojishughulisha na usafi wa mazingira na ujasiriamali. Mafunzo hayo yameongozwa na Meneja Ngowo Gift, akishirikiana na Dkt. Kharid Mwakoba na Obasanjo Nniwako kutoka NEMC.
Katika mafunzo hayo, wananchi wameelimishwa kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira, sambamba na kutambua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotokana na matumizi na usimamizi endelevu wa rasilimali za mazingira.
Katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi ni Nguzo ya Tatu ya Dira hiyo. Hivyo, mazingira si suala la pembeni katika maendeleo ya Taifa, bali ni sehemu ya msingi ya Tanzania tunayoijenga kwa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.
Juhudi za utoaji wa elimu ya mazingira zinazoendelea kufanywa na NEMC zinalenga kujenga jamii yenye uelewa na uwezo wa kutambua athari za uharibifu wa mazingira, kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti madhara, pamoja na kutumia fursa zinazotokana na usimamizi endelevu wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
NEMC inaendelea kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, kwa kutambua kuwa mazingira salama ni msingi wa afya, maendeleo na uchumi endelevu wa Taifa
NKM OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA) DKT. MADUHU KAZI AZURU NEMC
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Maduhu Kazi, amezuru NEMC kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kazi ameipongeza Serikali kwa kuthamini masuala ya Mazingira na kuipa kipaumbele ajenda ya mazingira katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo ya Taifa yanaenda sambamba na uhifadhi endelevu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, ameipongeza NEMC kwa uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake na kulitaka Baraza kuendelea kusimamia misingi ya Sheria, huku likiimarisha ufanisi katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa manufaa ya Taifa na vizazi vya baadae.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokuwa akizungumza alimweleza Dkt. Kazi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Baraza na hatua zinazochukuliwa katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira, huku akiahidi kuendelea kusukuma mbele ajenda ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya Serikali.
𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa ...
-
Ni katika kufanya tathmini na kuimarisha umoja. Watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Makao Makuu na k...
-
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...
-
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini tarehe 15 Novemba 2025 lilishiriki kusimamia na kushuhudia Uteke...