Katika jamii yoyote endelevu, mazingira ni kiini cha ustawi. Na kama taifa linaanzia kwenye kaya, basi utunzaji wa mazingira nao lazima uanze mlangoni mwa kila mmoja wetu. Moja ya mfano hai unaoonyesha dhamira hii ni Bi. Magdalena Chuwa, mkazi wa Mbande, Chamazi – Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Bi. Chuwa, ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu mstaafu wa Wakala wa Vipimo (2009 hadi 2016), si tu amekuwa kinara wa taaluma, bali pia amejitoa kwa moyo wote kuwa mdau wa kweli wa mazingira. Anaamini kuwa “mazingira ni maisha, na maisha ni utunzaji wa mazingira.”
Katika picha za bustani yake tulivu, tunaona mwitikio wa kweli wa falsafa hiyo. Bustani ya nyumbani kwake siyo tu eneo la kupendezesha makazi, bali ni shule ya mazingira kwa vitendo. Miti ya palms ambayo ilianza kama mimea midogo kwenye pots alipokuwa anaishi Tabata, sasa imestawi Chamazi na kuzidi kimo cha paa la nyumba yake, ikitoa kivuli na hewa safi kwa familia na jamii inayomzunguka.
Lakini kilicho cha kipekee zaidi ni wazo lake la kuhimiza mashindano ya mazingira kuanzia ngazi ya kaya. Anaamini kuwa “kama mtu atahamasishwa, hata akiwa kwenye nyumba ya kupanga, anaweza kupanda miti kwenye pot na kuihamisha anapohamia kwake.” Hili ni wazo la kimapinduzi linalowezesha mazingira bora kwa wote – hata wale wasio na miliki ya ardhi ya kudumu.
Bi. Magdalena ni mmoja wa washiriki wa #mazingirachallengeTZ iliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo mshindi atatangazwa tarehe 6 Julai, kabla ya kilele cha Maonesho ya Saba Saba.
Katika zama hizi za mabadiliko ya tabianchi, tunahitaji mashujaa wa mazingira kutoka kila kona ya jamii yetu. Kwa mfano wa kina kama wa Bi. Magdalena, tuna hakika kuwa mabadiliko makubwa yanaweza kuanzia na mtu mmoja tu – nyumbani kwake.