Nyumbani

NEMC NA WIOMSA WAENDESHA WARSHA KUHUSU UMUHIMU WA VYAKULA VYA BULUU KATIKA LISHE NA USALAMA WA CHAKULA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Taasisi ya WIOMSA (West Indian Ocean Marine Science Association) wameendesha Warsha kwa wadau wa Sekta mbalimbali za Serikali, binafsi na Sekta za kijamii kuhusu mchango wa vyakula vya baharini, mitoni na maziwa "Blue foods" katika lishe na usalama wa chakula.

Warsha hiyo ya Siku mbili imefanyika kuanzia tarehe 21 hadi 22 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Hoteli ya Tanga Resort Mkoani Tanga.

Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha hiyo Mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa buluu na Uvuvi Zanzibar Bw. Zahor Kassim Mohamed ameeleza kuwa vyakula vya buluu "Blue foods" ni muhimu sana katika lishe bora na usalama wa chakula.

"Vyakula vya buluu "Blue foods" kama vile samaki, dagaa, kaa, majongoo wa baharini, mwani na viumbe wengine vinamchango mkubwa katika lishe bora, usalama wa chakula, uchumi wa Kaya na ajira." Amesema Bw. Zahor Mohamed.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa Warsha  

Akiongea na Waandishi wa habari mara baada ya awamu ya kwanza ya Warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema lengo kuu la Warsha hii ni kuhamasisha juu ya umuhimu wa vyakula vya baharini,  katika mito na maziwa "Blue foods" katika lishe bora kwani vyakula hivyo vinamanufaa makubwa katika Afya ya mwanadamu na hivyo kujenga Taifa lenye watu wenye uelewa na kuweza kujitegemea.
Akiwasilisha mada Mkurugenzi wa Taasisi ya WIOMSA Dkt. Arthur Tude amesema  Taasisi hiyo imejikita katika tafiti za kuboresha lishe bora na kuelimisha jamii kuhusu vyakula vya baharini, hivyo imeamua kushirikiana na NEMC Pamoja na Taasisi nyinginezo kuhamasisha jamii juu ya uvunaji wa vyakula vya baharini vyenye lishe bora.


Aidha, Zahor alisisitiza kuwa ni muhimu Sekta zote binafsi na za Serikali, Taasisi na washirika wa maendeleo na jamii za uvuvi kuhakikisha kuwa "blue food" zinachangia kwa ufanisi kutokomeza njaa, kuongeza kipato na kulinda Mazingira ya bahari, mito na maziwa ambavyo ni rasilimali muhimu za kufuga vyakula buluu.

Ameongeza kuwa, licha ya changamoto zinazokabili ustawi wa vyakula vya buluu, Serikali imeweza kuimarisha Sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuwezesha ufugaji samaki katika mabwawa ya kisasa, kuwezesha vikundi vya Wanawake na vijana katika mnyororo wa thamani wa mazao ya maji, kushiriki katika juhudi za kimataifa za na kikanda kama vile Blue Economy na mabadiliko ya mifumo ya chakula duniani.


Washiriki wa Warsha wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya awamu ya kwanza ya warsha hiyo.

NEMC YATUNUKU TUZO KWA TANTRADE UTUNZAJI WA MAZINGIRA MSIMU WA SABASABA

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akikabidhi tuzo hiyo, kwa Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Bi.Latifa Khamis


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetunuku tuzo ya heshima kwa Mamlaka ya maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuhusu utunzaji wa Mazingira, katika hafla ya kufunga maonesho ya biashara kimataifa  ya 49  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo


Akikabidhi tuzo hiyo, kwa Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Bi.Latifa Khamis,  Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema NEMC imekabidhi tuzo hiyo kwa kutambua tano bora za utunzaji na usafi wa Mazingira uliosimamiwa nao katika kipindi chote cha Maonesho ya sabasaba 2025.



Dkt. Semesi amezianisha tano Bora hizo ambazo ni;

Ubunifu siku ya maalumu ya Mazingira ambayo iliadhimishwa tarehe 06.07.2025, mandhari ya maonesho kuwa safi na ya kupendeza kipindi chote cha Maonesho, kuhamasisha matumizi ya Nishati safi, kuhamasisha washiriki kutumia bidhaa ambazo ni rafiki kwa Mazingira na kufaulu kudhibiti taka licha ya idadi kubwa ya watu kutembelea maonesho hayo.

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Selemani Saidi Jafo akizungumza

Hafla hiyo imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali Wakuu wa Serikali akiwemo Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Kassim Majaliwa ambaye ndiye mgeni rasmi na aliyefunga maonesho ya sabasaba 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Seleman Jafo pamoja na Viongozi wengine mbalimbali wa Serikali.


Maonesho ya biashara kimataifa kwa mwaka 2025 yamebeba Kaulimbiu mbiu isemayo "𝙈𝙖𝙤𝙣𝙚𝙨𝙝𝙤 𝙮𝙖 𝙗𝙞𝙖𝙨𝙝𝙖𝙧𝙖 𝙮𝙖 𝙆𝙞𝙢𝙖𝙩𝙖𝙞𝙛𝙖 𝙎𝙖𝙗𝙖𝙨𝙖𝙗𝙖, 𝙁𝙖𝙝𝙖𝙧𝙞 𝙮𝙖 𝙏𝙖𝙣𝙯𝙖𝙣𝙞𝙖".

Aidha, yamehudhuriwa na takribani nchi 22 na asilimia 70 ya wawekezaji wameweza kufikia malengo yao na kuongeza idadi ya wadau na masoko.


Baraza linaendelea kuhimiza wawekezaji na watanzania wote kwaujumla  kuendelea kuzingatia kanuni na miongozo ya utunzaji wa Mazingira kwa ajili ya Tanzania endelevu, safi na salama

HAWA HAPA WASHINDI WATATU WA MAZINGIRA CHALLENGE



 





 

NEMC YAUNGANA NA TAASISI NYINGINE KUADHIMISHA SIKU MAALUMU YA MAZINGIRA MAONESHO YA SABASABA 2025

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC  Julai 6, 2025  limeungana na Taasisi mbalimbali kuadhimisha Siku ya maalumu ya Mazingira iliyotengwa kwa mara ya kwanza kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa (sabasaba) 2025.

Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo alikuwa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Cyprian Luhemeja huku tukio hilo likibebwa na Kauli mbiu isemayo "Matumizi ya Nishati safi na utunzaji wa Mazingira Kwa ustawi wa Tanzania bora".



Akizungumza katika hotuba yake Mhe. Cyprian Luhemeja ameitaka siku hiyo ya tarehe 6 /7 itengwe rasmi kuwa siku maalumu ya Mazingira kila mwaka katika maonesho hayo kuanzia maonesho ya 50 ya biashara ya kimataifa (sabasaba).

Sambamba na hilo amesisitiza watanzania wote kutunza Mazingira kwa kuwa Mazingira yaliumbwa kwanza Kisha mwanadamu akaumbwa baadae ili ayatunze, ayahifadhi na kuyalinda.

"Hii duniani ilianza kwa kutengenezewa Mazingira, mwanadamu ameumbwa wa mwisho baada ya Mazingira kutengenezewa na mwanadamu alipoumbwa alipewa kazi ya kuyatunza na kuyahifadhi Mazingira lakini mwanadamu anayaharibu kwa uchafuzi na ukataji wa miti.




Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza washindi wa Mazingira Challenge iliyofanyika siku kadhaa zilizopita ambayo ililenga kumpata balozi kinara wa  Utunzaji wa Mazingira na anayehamasisha utunzaji wa Mazingira kwa kupiga picha ya Mazingira safi yanayomzunguka na kuwasilisha NEMC Kwa ajili ya mashindano hayo.

Maadhimisho hayo yalipambwa na mabalozi wa Mazingira pamoja na watumbuizaji nguli akiwemo Mrisho Mpoto pamoja na Mr. Tree na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC, TANTRADE, STAMICO, Wanawake na Samia, Shirika la PUMA pamoja na wananchi waliotembelea maonesho ya sabasaba.









Sethi Ura Company Limited Yasimamia Mapinduzi ya Usafi: Ushirikiano wa Jamii Katika Kuweka Mazingira Safi Hospitali ya Wilaya ya Hai

Vijana wa kujitolea wakipanga majukumu kabla ya kuanza kazi ya usafi katika eneo la hospitali.


Katika kuendeleza dhana ya afya bora inayotegemea mazingira safi na salama, kampuni ya Sethi Ura Company Limited kupitia Mkurugenzi Mtendaji wake imeongoza zoezi la usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wilaya ya Hai. Zoezi hili limefanyika kwa kushirikiana na vijana, wafanyakazi wa afya, na wanajamii, likilenga kuboresha mazingira ya hospitali ili yawe rafiki kwa wagonjwa, wahudumu na jamii kwa ujumla.

Mshikamano ukionekana wazi—watu wa rika tofauti wakifagia kwa pamoja kuhakikisha mazingira ya hospitali yanabaki safi.

Kwa mujibu wa miongozo ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mazingira safi yana mchango mkubwa katika kudhibiti magonjwa ya milipuko na kuboresha ustawi wa watu. Usafi katika maeneo ya huduma za afya hupunguza uwezekano wa maambukizi ya magonjwa na huongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa.

Katika picha mbalimbali, tunaona ari na moyo wa kujitolea wa vijana waliovalia glovu, wakiwa na vifaa vya kufanyia usafi kama vile fagio, koleo na toroli, wakifanya kazi kwa mshikamano mkubwa. Wengine wakikusanya majani yaliyokatwa, wakifagia taka, huku wakionekana wakihamasishana na kusaidiana – mfano bora wa mshikamano wa kijamii unaochochea maendeleo endelevu.


Wanawake wakionyesha mfano bora wa ushiriki katika usafi, wakikusanya majani na taka kwenye toroli.

Maneno ya Kuishi Nayo:

🌱 "Mazingira safi ni tiba ya kwanza."
💪 "Ushirikiano wa jamii ni chanzo cha afya ya kudumu."

Tukio hili linahamasisha jamii nzima, hususan kampuni binafsi na taasisi, kushiriki kikamilifu katika masuala ya usafi na utunzaji wa mazingira. Ni wakati wa kila mmoja wetu kuchukua hatua – iwe ni kwa kufyeka majani, kupanda miti, au kuongoza kampeni za usafi katika maeneo yetu ya kazi na makazi.

NEMC inaendelea kusisitiza:

✅ Mazingira safi ni haki ya kila Mtanzania
✅ Hatua ndogo tunazochukua leo, huleta athari kubwa kesho

NEMC YATOA MAFUNZO YA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA KWA WANAFUNZI WA DARTU


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha mafunzo maalum ya kuwajengea uelewa kuhusu Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) wanafunzi wa mwaka wa tatu wa kada ya ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DARTU).

Mafunzo hayo yamefanyika leo, Julai 3, 2025, katika Ukumbi wa NEMC uliopo jijini Dar es Salaam, na yaliongozwa na Afisa Mazingira Mwandamizi, Bw. Emmanuel Salyeem.

Katika mafunzo hayo, Bw. Salyeem alitoa wasilisho lililojikita katika kuelezea mchakato mzima wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira, akitoa mifano hai ya namna Baraza linaendesha tathmini hiyo kwenye miradi mikubwa, ya kati na midogo. Alisisitiza umuhimu wa TAM katika kulinda afya ya viumbe hai wote pamoja na mazingira kwa ujumla.

Kupitia mafunzo haya, wanafunzi walipata nafasi ya kuelewa kwa kina majukumu ya NEMC na mchango wa tathmini ya kimazingira katika maendeleo endelevu ya taifa.

NEMC inaendelea kutoa wito kwa taasisi za elimu, vikundi vya kijamii na wadau mbalimbali kufika katika ofisi za Baraza kwa ajili ya kupata elimu ya uhifadhi wa mazingira na kujifunza namna bora ya kushiriki katika kulinda mazingira yetu. 







 

NEMC WHATSAPP NAMBA 0680400400






 

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...