Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
kwa kushirikiana na Taasisi ya WIOMSA (West Indian Ocean Marine Science
Association) wameendesha Warsha kwa wadau wa Sekta mbalimbali za Serikali,
binafsi na Sekta za kijamii kuhusu mchango wa vyakula vya baharini, mitoni na
maziwa "Blue foods" katika lishe na usalama wa chakula.
Warsha hiyo ya Siku mbili imefanyika kuanzia tarehe 21 hadi
22 Julai, 2025 katika Ukumbi wa Hoteli ya Tanga Resort Mkoani Tanga.
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha hiyo Mgeni rasmi,
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa buluu na Uvuvi Zanzibar Bw. Zahor Kassim
Mohamed ameeleza kuwa vyakula vya buluu "Blue foods" ni muhimu sana
katika lishe bora na usalama wa chakula.
"Vyakula vya buluu "Blue foods" kama vile
samaki, dagaa, kaa, majongoo wa baharini, mwani na viumbe wengine vinamchango
mkubwa katika lishe bora, usalama wa chakula, uchumi wa Kaya na ajira."
Amesema Bw. Zahor Mohamed.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa Warsha
Akiongea na Waandishi wa habari mara baada ya awamu ya
kwanza ya Warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi
amesema lengo kuu la Warsha hii ni kuhamasisha juu ya umuhimu wa vyakula vya
baharini, katika mito na maziwa
"Blue foods" katika lishe bora kwani vyakula hivyo vinamanufaa
makubwa katika Afya ya mwanadamu na hivyo kujenga Taifa lenye watu wenye uelewa
na kuweza kujitegemea.
Akiwasilisha mada Mkurugenzi wa Taasisi ya WIOMSA Dkt.
Arthur Tude amesema Taasisi hiyo
imejikita katika tafiti za kuboresha lishe bora na kuelimisha jamii kuhusu
vyakula vya baharini, hivyo imeamua kushirikiana na NEMC Pamoja na Taasisi
nyinginezo kuhamasisha jamii juu ya uvunaji wa vyakula vya baharini vyenye
lishe bora.
Aidha, Zahor alisisitiza kuwa ni muhimu Sekta zote binafsi
na za Serikali, Taasisi na washirika wa maendeleo na jamii za uvuvi kuhakikisha
kuwa "blue food" zinachangia kwa ufanisi kutokomeza njaa, kuongeza
kipato na kulinda Mazingira ya bahari, mito na maziwa ambavyo ni rasilimali
muhimu za kufuga vyakula buluu.
Ameongeza kuwa, licha ya changamoto zinazokabili
ustawi wa vyakula vya buluu, Serikali imeweza kuimarisha Sekta hiyo ikiwa ni
pamoja na kuwezesha ufugaji samaki katika mabwawa ya kisasa, kuwezesha vikundi
vya Wanawake na vijana katika mnyororo wa thamani wa mazao ya maji, kushiriki
katika juhudi za kimataifa za na kikanda kama vile Blue Economy na mabadiliko
ya mifumo ya chakula duniani.
Washiriki wa Warsha wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya awamu ya kwanza ya warsha hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni