Nyumbani

NEMC NA TAASISI YA CSE WAENDESHA MAFUNZO YA NAMNA YA KUTENGENEZA ORODHA YA TAKA ZA VIWANDANI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira- NEMC, kwa kushirikiana na Taasisi ya Centre of Science and Environment ( CSE) ya India imefanya mafunzo juu ya mbinu za kutengeneza Orodha ya Taka za Viwandani. 

Lengo ni kutengeneza orodha ya viwanda vyote nchini pamoja na taka zinazozalishwa na viwanda hivyo ili kuboresha usimamizi wa taka. 

Aidha, jambo hili linaenda kuchangia kwenye sera ya Taka ni Uchumi ( Circular economy) kwa kubaini aina ya taka na viwanda vinavyoweza kuchakata au kutumia taka hizo.

NEMC YASAINI MAKUBALIANO YA AWALI NA UPS KUANZISHA MFUMO WA KIDIGITALI WA UFUATILIAJI WA UCHAFUZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesaini makubaliano ya awali na Kampuni ya United Platform Solution (UPS) kwa ajili ya kuanzisha mfumo wa kidigitali wa ufuatiliaji wa uchafuzi wa mazingira katika miradi yote ya maendeleo nchini.

Hafla hiyo ya kusaini makubaliano hayo imefanyika Disemba 04,2025 katika ukumbi wa mikutano wa Baraza uliopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bw. Dickson Mjinja ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha, amesema Baraza limefikia hatua hiyo ili kurahisisha masuala mazima ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira kwani mfumo huo ukikamilika utarahisisha kubaini viashiria vya uchafuzi wa mazingira na kupata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu hali ya mazingira.

Naye Bw Mamadou Drame kutoka UPS alipozungumza amesema imekuwa azma yao kushirikiana na NEMC katika kuhakikisha uchafuzi wa Mazingira unadhibitiwa kidigitali ili kuyalinda kwa maendeleo endelevu.

Akifafanua namna mfumo huo utakavyotenda kazi, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Bw. Jamal Baruti amesema  kwa sasa utaanza mradi wa majaribio ambapo vifaa maalum vitawekwa katika miradi ya mazingira ikijumuisha miradi iliyopo katika Kanda 13 za NEMC nchi nzima hali itakayoimarisha zaidi usimamizi na Uhifadhi wa mazingira nchini.





NEMC YAUNGANA NA WATANZANIA WOTE KUADHIMISHA SIKU YA WALEMAVU DUNIANI

Yasisitiza mazingira jumuishi kwa ustawi wa walemavu 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo limeungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Walemavu Duniani kwa kutoa wito wa kuimarishwa kwa mazingira jumuishi na rafiki kwa watu wote, hususani watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema kuwa jitihada za kulinda mazingira haziwezi kuwa endelevu pasipo kuhakikisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika mipango na maamuzi yahusuyo mazingira.

“Haki ya kuishi katika mazingira safi, salama na yenye afya ni ya kila mtu. Tunajivunia kuwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha miundombinu na huduma za kimazingira zinakuwa salama na zinazofikika kwa watu wenye ulemavu,” alisema Dkt. Semesi.

 Ujenzi wa Miundombinu Rafiki 

Baraza limeendelea kuhimiza Taasisi za umma na binafsi kutekeleza ujenzi shirikishi (inclusive design) ili kuhakikisha njia za kupita, majengo, vyoo na vifaa vya kimazingira vinapatikana na kutumika na watu wote bila vikwazo.

 Ushirikishwaji Katika Maamuzi 

Kwa kutambua umuhimu wa uwakilishi, NEMC imeweka mikakati inayolenga kuwahusisha watu wenye ulemavu katika kamati na majadiliano muhimu ya usimamizi wa mazingira katika ngazi mbalimbali za Taifa.

 Ulinzi Dhidi ya Hatari za Kimazingira 

Baraza pia linaimarisha mifumo ya tahadhari dhidi ya majanga kama mafuriko, uchafuzi na taka hatarishi, likibainisha kuwa watu wenye ulemavu mara nyingi hukumbwa kwa kiwango kikubwa zaidi na madhara ya majanga hayo. Mwongozo unaotolewa kwa mamlaka za mitaa unalenga kuhakikisha mipango ya dharura inawalinda na kuwatambua kikamilifu.

Elimu na Uhamasishaji

Kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali, Baraza linaendeleza kampeni za elimu na uhamasishaji kuhusu umuhimu wa mazingira safi na salama kwa ajili ya ustawi wa watu wenye ulemavu, sambamba na kukuza mtazamo chanya katika jamii.

Dkt. Semesi alihitimisha kwa kusisitiza dhamira ya NEMC katika kuhakikisha sera na miradi ya mazingira nchini inatekelezwa kwa kuzingatia usawa na ujumuishaji.

“Hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma katika kunufaika na rasilimali za mazingira. Ustawi wa watu wenye ulemavu ni sehemu ya ustawi wa Taifa,” alisema.

𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐒𝐇𝐀 𝐌𝐀𝐅𝐔𝐍𝐙𝐎 𝐊𝐔𝐇𝐔𝐒𝐔 𝐍𝐘𝐄𝐍𝐙𝐎 𝐙𝐀 𝐔𝐒𝐈𝐌𝐀𝐌𝐈𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐙𝐈𝐍𝐆𝐈𝐑𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐖𝐈𝐙𝐀𝐑𝐀, 𝐓𝐀𝐀𝐒𝐈𝐒𝐈 𝐍𝐀 𝐇𝐀𝐋𝐌𝐀𝐒𝐇𝐀𝐔𝐑𝐈 𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐍𝐈𝐒𝐏𝐀𝐀 𝐍𝐀 𝐖𝐈𝐋𝐀𝐘𝐀

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linaendeaha mafunzo kuhusu nyenzo za usimamizi wa mazingira kwa Wizara, Taasisi pamoja na Halmashauri za Manispaa na Wilaya nchini. Mafunzo haya yameandaliwa kupitia Mradi wa kujenga uwezo wa kitaifa katika kusimamia Sheria ya usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004. Mradi huu unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA). Mradi unalenga kuimarisha uelewa na uwezo wa watumishi katika kusimamia Sheria ya mazingira kwa ufanisi katika utekelezaji wa majukumu katika maeneo yao ya kazi.


Mafunzo hayo ya siku mbili yameanza tarehe 27 na kumalizika 28 Novemba 2025 jijini Dodoma. Kupitia mafunzo haya, washiriki wanapata maarifa ya kutathmini athari za kimazingira pamoja na kupanga mikakati endelevu ya utunzaji wa mazingira huku wakizingatia Nguzo ya tatu ya Dira ya maendeleo ya Taifa 2050 ambayo imeweka mkazo juu ya kuzingatia masuala ya utunzaji wa Mazingira nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa maeneo maalum na mabadiliko ya tabianchi kutoka NEMC, Dkt. Careen Kahangwa, aliwataka washiriki kutumia fursa hiyo kuboresha utendaji katika maeneo yao ya kazi. Mafunzo haya yanaendeshwa na timu ya wataalamu kutoka NEMC. Aidha wataalamu kutoka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ofisi ya Makamu wa Rais na taasisi binafsi ya Taka ni ajira nao walishiriki Katika kutoa mafunzo.

Washiriki wa mafunzo hayo wamepata nafasi ya kujadili kwa kina changamoto za kimazingira zinazojitokeza katika taasisi zao na kujifunza mbinu bora za kukabiliana nazo. Kupitia mafunzo haya, wanatarajiwa kuboresha mifumo ya ufuatiliaji, utoaji taarifa, na utekelezaji wa sheria na kanuni za mazingira nchini. Hatua hii muhimu itachangia kwa kiasi kikubwa kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.







𝐃𝐊𝐓. 𝐅𝐄𝐒𝐓𝐎 𝐃𝐔𝐆𝐀𝐍𝐆𝐄 𝐀𝐙𝐔𝐍𝐆𝐔𝐌𝐙𝐀 𝐍𝐀 𝐖𝐀𝐓𝐔𝐌𝐈𝐒𝐇𝐈 𝐖𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂

𝐀𝐬𝐢𝐬𝐢𝐭𝐢𝐳𝐚 𝐔𝐡𝐢𝐟𝐚𝐝𝐡𝐢 𝐧𝐚 𝐔𝐬𝐢𝐦𝐚𝐦𝐢𝐳𝐢 𝐰𝐚 𝐌𝐚𝐳𝐢𝐧𝐠𝐢𝐫𝐚 𝐡𝐚𝐬𝐚 𝐮𝐝𝐡𝐢𝐛𝐢𝐭𝐢 𝐰𝐚 𝐤𝐞𝐥𝐞𝐥𝐞 𝐜𝐡𝐚𝐟𝐮𝐳𝐢 𝐦𝐚𝐞𝐧𝐞𝐨 𝐲𝐚 𝐦𝐚𝐤𝐚𝐳𝐢


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais  (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange, amefanya ziara yake ya kwanza katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kuzungumza na watumishi wa Baraza hilo, akitoa maelekezo mahsusi juu ya kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.

Katika hotuba yake, Dkt. Dugange amesisitiza umuhimu wa kulinda afya ya jamii kupitia udhibiti wa kelele chafuzi, akibainisha kuwa kelele zimekuwa chanzo cha changamoto za kiafya, hususani magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo ya makazi.

Amesema kelele chafuzi ni miongoni mwa mambo yanayoashiria uharibifu wa mazingira na yanapaswa kudhibitiwa kwa nguvu na umakini wa hali ya juu.

Akiweka msisitizo zaidi, Dkt. Dugange ameagiza NEMC kuandaa mpango mkakati wa mashirikiano  kati yake na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hasa kwenye majiji  ili kuhakikisha udhibiti wa kelele chafuzi unatekelezwa katika ngazi zote kutoka Mtaa hadi Taifa. 

Amesisitiza  kuwa kila mtumishi wa NEMC ana jukumu la kuhakikisha jamii inajengewa uelewa na Sheria za Mazingira zinatekelezwa ipasavyo.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Dugange pia ameuzungumzia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2050 unaohusisha nguzo tatu kuu, ikiwemo Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi

Amefafanua uhusiano uliopo kati ya mazingira salama, afya bora, na kupungua kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Akigusia ajenda ya nishati safi, Dkt. Dugange alikumbusha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inataka ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ambayo ina manufaa kwa jamii ikiwemo kupunguza uchafuzi wa hewa, kulinda mazingira na kupunguza gharama za maisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, ameahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt.Immaculate Sware Semesi amepokea maelekezo na kuahidi kuyatekeleza kwa mujibu wa Sheria na kuhakikisha usimamizi thabiti wa mazingira nchini.



𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐈𝐋𝐀𝐙𝐀 𝐖𝐂𝐅 𝟓 𝐁𝐈𝐋𝐀 𝐒𝐇𝐈𝐌𝐌𝐔𝐓𝐀 𝟐𝟎𝟐𝟓

Timu ya mpira wa miguu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeilaza timu ya WCF kwa jumla ya magoli matano kwa sifuri.

Mchezo huo uliochezwa Novemba 27, 2025, katika uwanja wa Highland mkoani Morogoro, ulianza kwa kasi kubwa ambapo dakika ya 15 Fortinatus Patrick alifungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati, na kufanya “mazingira ya uwanja” kuanza kuwa safi. Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 33 ambapo mfungaji huyo huyo, Fortinatus Patrick, alipachika bao la pili lililoipeleka NEMC mapumzikoni wakiwa kifua mbele, huku “mazingira” yakiendelea kupendeza uwanjani.

Kipindi cha pili kilipoanza dakika ya 46, Fortinatus Patrick aliendeleza ubabe kwa kufunga bao la tatu, kabla ya kiungo Ismail Jemba kuongeza la nne dakika ya 51.

Kama ilivyo desturi ya NEMC kutoridhishwa na uchafuzi wa mazingira nchini na kuendelea kuhimiza usafi kote nchini, vivyo hivyo hawakuridhika na matokeo hayo ya 4–0. Dakika ya 62, Emmanuel Mlungwana alipiga shuti kali kutoka katikati ya uwanja lililopenya kati ya miguu ya golikipa wa WCF na kutinga wavuni, likiwa bao la tano kwa NEMC.

NEMC ipo mkoani Morogoro kushiriki michezo ya SHIMMUTA 2025 kama sehemu ya kuimarisha afya za watumishi wake pamoja na kuendelea kutoa hamasa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini. Kwa mwaka huu, timu za NEMC zimefadhiliwa jezi na vifaa vya michezo kupitia miradi yake miwili — Adaptation Fund na EHPMP — huku zikitumia jezi hizo kueneza jumbe mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi na udhibiti wa matumizi ya zebaki (mercury).




NEMC YAELIMISHA UMMA UDHIBITI WA KELELE CHAFUZI NA MITETEMO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuimarisha juhudi za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kufuatia ongezeko la malalamiko katika maeneo ya mijini na vijijini. 

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Bw. Hamadi Taimuru, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC), amesema kelele zimeendelea kuwa changamoto kubwa kwa afya na ustawi wa wananchi kutokana na shughuli za burudani, ujenzi, biashara na matumizi ya vifaa vya sauti vinavyokiuka viwango vya kisheria.


Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamadi Taimuru akizungumza na vyombo vya habari alipokuwa akitoa taarifa kwa umma kuhusu kelele chafuzi na mitetemo

Bw. Taimuru amefafanua kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Sura 191) na Kanuni za Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015 zimeweka viwango maalumu vya kelele kwa maeneo ya makazi, biashara, viwanda na Taasisi muhimu kama Hospitali na shule, sambamba na kuainisha utaratibu wa utoaji vibali kwa shughuli zinazoweza kusababisha kelele kubwa. 

Amesema athari za kelele za muda mrefu ni pamoja na kupoteza usikivu, msongo wa mawazo, shinikizo la damu na kuathiri umakini wa watoto shuleni, hivyo kulifanya suala la udhibiti kuwa muhimu kwa kulinda afya ya umma".

Aidha, amebainisha uwepo wa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Kanuni za udhibiti, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kupimia kelele kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu athari za kelele, pamoja na baadhi ya biashara na maeneo ya burudani kutokufuata sheria na muda wa utulivu. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viwango vinavyoruhusiwa ni 70dBA mchana na 60dBA usiku kwa maeneo ya viwandani; 50dBA mchana na 35dBA usiku kwa makazi, 60dBA mchana na 50dBA usiku kwa makazi yenye viwanda vidogo,  55dBA mchana na 45dBA usiku kwa maeneo ya makazi, biashara na burudani; na 45dBA mchana na 35dBA usiku kwa Hospitali, Shule, Kumbi za mikutano na maeneo ya mapumziko.

Katika kuimarisha usimamizi, Bw. Taimuru alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya OSHA, Polisi, BASATA, Serikali za Mitaa, nyumba za ibada na wamiliki wa kumbi za burudani katika kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kusimamia vibali, kutoa elimu, kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa vya sauti na kufanya kaguzi za mara kwa mara.

Aliongeza kuwa ramani za viwango vya kelele, kampeni za uelimishaji na mifumo rahisi ya utoaji taarifa za malalamiko ni hatua muhimu zinazohitajika kuimarishwa.

Akihitimisha, Bw. Hamadi Taimuru amesema Tanzania ina mfumo madhubuti wa kisheria wa kudhibiti kelele na mitetemo, na kwamba ushirikiano wa wadau wote, sekta binafsi, Taasisi za umma na wananchi ni msingi muhimu wa kulinda afya, utulivu na ustawi wa jamii.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...