Nyumbani

NEMC YATOA TUZO KWA MSHINDI WA JUMLA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi tuzo kwa Mkoa wa Njombe ikiwa ni Mshindi wa Jumla wa Shindano la Afya na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2024.


Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mgeni Rasmi wa Mkutano Maalum wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba Aprili 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).

Akimkabidhi Tuzo hiyo Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Silas Shemdoe amesema tuzo hiyo imetolewa na NEMC kwa kuthamini mchango wa Mkoa wa Njombe katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.


Akizungumza na baadhi ya Waheshimiwa Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Njombe mara baada ya zoezi hilo la utoaji wa Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza kwa kuchukulia suala la Mazingira kwa umuhimu mkubwa na kutoa rai kwa Halmashauri nyingine Nchi nzima kuiga mfano wa Mkoa wa Njombe.


Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makete, Mhe. Rabson A. Mahenge ameishukuru NEMC kwa kuthamini mchango wao katika kutunza mazingira na amesisitiza kuwa NEMC iendelee kutoa maelekezo Mkoa wa Njombe utatekeleza na matokeo yataonekana.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo NEMC huendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kila mwaka. Mwaka 2024, na miaka mingine Mkoa wa Njombe umekuwa kinara katika uimarishaji wa huduma za usafi wa Mazingira.


Mkoa huo umekuwa ukiongoza kwa kuwa na kaya zenye vyoo bora, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika ngazi ya kaya, Shule na Vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, mkoa umekuwa mfano na darasa kujifunza kwa Halmashauri nyingine katika masuala ya udhibiti wa taka ngumu na maji taka. Hali hii ya Mkoa inachangiwa na viongozi ngazi zote kuamua pamoja na wananchi kuyapa kipaumbele masuala ya usafi wa mazingira, hali inayochangia Mkoa kutopata visa vya ugonjwa wa kipindipundu kwa muda mrefu na wananchi kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.










NEMC YAKUTANA NA TAASISI ZA SERIKALI NA WADAU WA SEKTA YA MADINI GEITA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya mkutano na wadau wa mazingira tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukumbusha wadau kuhusu haki na wajibu wao katika kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake. Katika mkutano huo, viongozi wa NEMC waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuimarisha uelewa wa utekelezaji sahihi wa sheria hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira.


Aidha, wawekezaji walisisitizwa umuhimu wa kufanya usajili na kukamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao. Hatua hii inalenga kulinda mazingira, afya za binadamu na viumbe hai wengine, pamoja na kuepusha hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya miradi isiyozingatia taratibu.


Kwa upande mwingine, taasisi za serikali zilihimizwa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za mazingira. NEMC imeeleza kuwa itaendelea kuandaa mikutano kama hii katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji kuelekea maendeleo endelevu ya taifa.


Taasisi za serikali zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Halmashauri za Geita, Kahama na Shinyanga, Tume ya Madini, Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

NEMC YATOA TUZO KWA MSHINDI WA JUMLA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi tuzo kwa Mkoa wa Njombe ikiwa ni Mshindi wa Jumla wa Shindano la Afy...