Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imekutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa Taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.
Mkutano huo umefanyika kwenye kikao cha kawaida cha kila mwezi cha watumishi, ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo, akiambatana na wajumbe wengine sita wa bodi, aliwasihi watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano wa uadilifu, usafi wa mazingira, na utendaji wenye matokeo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi hao tangu uteuzi wa bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha alisema:
“Ili tuweze kutimiza majukumu yetu ipasavyo kama Taasisi ya mazingira, lazima tuanze na sisi wenyewe kwa kuwa wasafi, wawazi, wenye upendo na tuwe tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za ndani kabla ya kwenda kwa wananchi.”
Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia, majumbani kwa Watoto wadogo na kisha kusambaa kwa jamii nzima. Alisema kuwa bodi itasimamia uwazi katika maamuzi, kushirikiana kwa karibu na menejimenti pamoja na kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wote.
Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Bi. Mwanasha Tumbo (aliyesimama) akizungumza na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Baraza mara baada ya Bodi hiyo kutembelea Ofisi za Baraza
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alipopata fursa ya kuzungumza aliikaribisha rasmi Bodi hiyo mpya na kueleza kuwa Menejimenti na watumishi wa NEMC wako tayari kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha taasisi inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.
Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NEMC inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya wa kimkakati katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.
Matukio katika Picha: Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC na baadhi ya Watumishi wa NEMC wakiwa katika Kikao mara baada ya Bodi kutembelea Ofisi za Baraza Jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni