Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati, PURA na TANESCO, wametembelea Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway, kinachoendeshwa na kampuni ya Norcem chini ya Heidelberg Materials, ambacho ni kiwanda cha kwanza duniani cha saruji kuendesha kituo kamili cha kunasa na kuhifadhi hewa ya ukaa (CCS). Sekta ya saruji ni ngumu kupunguza hewa ya ukaa kwa sababu malighafi yake kuu (chokaa), huzalisha kaboni dioksaidi wakati wa mchakato.
Baadhi ya Wataalamu wa Mazingira wa NEMC na Wataalamu wa Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway wakiwa katika picha ya pamojaKiwanda hiki kinatumia teknolojia ya kunasa dioksidi kaboni kwa njia ya amini (amine absorption) ambapo gesi ya ukaa hutenganishwa kutoka kwenye moshi wa mitambo, kisha hubanwa (compressed) na kubadilishwa kuwa kimiminika ili kusafirishwa. Ukaa ulionaswa unasafirishwa kupitia mtandao wa hifadhi wa Northern Lights. Baada ya kubadilishwa kuwa kimiminika, husafirishwa kwa meli hadi kituo cha nchi kavu kisha huingizwa kwenye tabaka za miamba ya ardhini chini ya Bahari ya Kaskazini. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Longship wa Norway unaolenga kusaidia viwanda kupunguza hewa chafu ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.
Mradi huu wenye thamani ya takriban Euro milioni 400 unategemea ushirikiano wa karibu na msaada mkubwa wa kifedha wa serikali (takriban 75%) kutokana na gharama zake kubwa za kiufundi. Pia mradi huu umewezesha kutengenezwa kwa bidhaa mpya za saruji zenye alama ya “evoZero”, zinazouzwa kama saruji yenye uzalishaji usio na hewa ya ukaa kwa sababu ukaa wake unanaswa na kuhifadhiwa. Mafunzo na uzoefu unaopatikana hapa yanatarajiwa kusaidia katika utekelezaji wa miradi mingine ya CCS Duniani kote.
Kwa ujumla, kituo cha CCS cha Brevik kinaonyesha kuwa inawezekana kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa katika sekta ya saruji. Ingawa bado kuna changamoto za gharama na matumizi makubwa ya nishati, mradi huu ni hatua kubwa ya kihistoria katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ni mfano bora kwa viwanda vingine vizito vinavyolenga kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ya ukaa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni