Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC pamoja na Menejimenti wamefanya kikao katika Ukumbi wa Hoteli ya Adden Palace jijini Mwanza kufanya mapitio ya pamoja ya mpango mkakati wa utekelezaji wa Taasisi wa miaka mitano (NEMC Strategic Plan 2026-2030) kwa lengo la kutoa mwelekeo, vipaumbele na uhalisia wa utekelezaji wake katika kuleta matokeo chanya kwa Taifa.
Kikao hicho kilichowakutanisha wataalamu kiliendeshwa na Mwenyekiti wa Bodi Mhandisi Mwanasha Tumbo, ambapo washiriki walipata fursa ya kujadili kwa kina vipaumbele vya kimkakati vinavyolenga kuimarisha Uhifadhi na Usimamizi endelevu wa mazingira, kuboresha mifumo ya kiutawala, kupongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wadau.
Aidha maono na dhamira ya Taasisi yaliendelea kusisitizwa kupitia mikakati inayochochea matumizi ya Sayansi, teknolojia na ushirikiano wa wadau wa maendeleo.
Kwa ujumla mapitio ya Mpango mkakati yamehakikisha kuwa mwelekeo wa Baraza unaendana kikamilifu na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na ilani ya Chama hususan katika kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu, kukuza uchumi wa kijani na kuboresha ustawi wa jamii.
Kupitia kikao hiki, Baraza limeonesha dhamira thabiti ya kuhakikisha Mpango mkakati unakuwa chombo hai cha kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa kwa Sasa na vizazi vijavyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni