Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya mkutano na wadau wa mazingira tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Mkutano huo uliwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukumbusha wadau kuhusu haki na wajibu wao katika kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake. Katika mkutano huo, viongozi wa NEMC waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuimarisha uelewa wa utekelezaji sahihi wa sheria hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira.
Aidha, wawekezaji walisisitizwa umuhimu wa kufanya usajili na kukamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao. Hatua hii inalenga kulinda mazingira, afya za binadamu na viumbe hai wengine, pamoja na kuepusha hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya miradi isiyozingatia taratibu.
Kwa upande mwingine, taasisi za serikali zilihimizwa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za mazingira. NEMC imeeleza kuwa itaendelea kuandaa mikutano kama hii katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji kuelekea maendeleo endelevu ya taifa.
Taasisi za serikali zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Halmashauri za Geita, Kahama na Shinyanga, Tume ya Madini, Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni