Nyumbani

SERIKALI YASISITIZA UWAJIBIKAJI WA MAZINGIRA KWA VIWANDA NA WADAU WA TAKA HATARISHI

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za mazingira kwa sekta ya viwanda, kampuni za uteketezaji taka pamoja na wadau wanaohusika na uhifadhi wa bidhaa hatarishi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda afya za wananchi na kuhakikisha maendeleo endelevu ya taifa.


Hayo yamejadiliwa katika mkutano wa wadau wa mazingira ulioandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), uliowakutanisha wamiliki wa viwanda, wateketezaji wa taka na wenye maghala ya bidhaa hatarishi kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha usimamizi wa mazingira nchini.


Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa Reuben Nhamanilo Kwagilya, amesema ukuaji wa sekta ya viwanda unapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa sheria za mazingira ili kupunguza athari zinazoweza kuhatarisha afya za wananchi na mazingira.


Alieleza kuwa mazingira ni msingi muhimu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo kila mdau wa uzalishaji na usimamizi wa taka ana wajibu wa kuhakikisha shughuli zake zinafanyika kwa kuzingatia viwango vya usalama wa mazingira na afya.


Katika kikao hicho, Serikali ilisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, ikiwemo udhibiti wa uchafuzi wa hewa, maji na ardhi unaotokana na shughuli za viwanda pamoja na usimamizi sahihi wa taka ngumu na taka hatarishi.


Aidha, wadau walikumbushwa umuhimu wa kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) kabla ya kuanza miradi ya maendeleo pamoja na kufanya ukaguzi wa mazingira mara kwa mara ili kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaendana na matakwa ya sheria.


Mkutano huo pia uliangazia changamoto zinazotokana na ongezeko la taka za viwandani na matumizi ya kemikali hatarishi, ambapo NEMC ilihimiza matumizi ya teknolojia safi na mifumo bora ya uteketezaji na urejelezaji taka ili kupunguza uchafuzi wa mazingira.


Katika kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali, Serikali imeendelea kuhamasisha utekelezaji wa dhana ya Uchumi Mzunguko (Circular Economy) inayolenga kupunguza uzalishaji wa taka, kutumia tena bidhaa na kurejeleza malighafi kwa matumizi mengine ya kiuchumi.


Wadau wa mazingira walielezwa kuwa utekelezaji wa mfumo huo unaweza kusaidia viwanda kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko la ndani na kimataifa.


Kwa upande wake, NEMC ilisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wataalam wa mazingira ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na sekta ya viwanda inayozingatia sheria, inalinda mazingira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.


Mkutano huo umetajwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazokabili wadau wa mazingira pamoja na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wa sheria za mazingira nchini.


Kupitia mikutano kama hiyo, Serikali inalenga kujenga uelewa mkubwa kwa wadau kuhusu umuhimu wa matumizi salama ya kemikali, uhifadhi sahihi wa bidhaa hatarishi, usimamizi wa taka na uwekezaji katika teknolojia rafiki kwa mazingira kwa ajili ya ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

SERIKALI YASISITIZA UWAJIBIKAJI WA MAZINGIRA KWA VIWANDA NA WADAU WA TAKA HATARISHI

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za mazingira kwa sekta ya viwanda, kampuni za uteketezaji taka pamoja na wadau w...