Nyumbani

NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA JIJINI DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuonesha dhamira yake katika kuimarisha usafi wa mazingira kwa kushiriki kikao kazi cha wadau kilicholenga kutathmini utekelezaji wa afua mbalimbali za usafi wa mazingira kilichofanyika Januari 19, 2026 katika jiji la Dodoma.

Kikao hicho, kilichoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora yanayochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya jiji kwa ujumla.

Akitoa mada ya ufunguzi, Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Bw. Novatus Mushi, aliwasilisha juhudi na mikakati inayotekelezwa na Baraza katika kuimarisha usafi wa mazingira Jijini Dodoma. Katika wasilisho lake, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, mamlaka za Serikali za mitaa na wadau wengine wa mazingira ili kufanikisha utekelezaji endelevu wa afua hizo.

Katika kikao hicho, wadau mbalimbali waliwasilisha taarifa na mada zinazohusu utekelezaji wa afua za usafi wa mazingira kwa kuzingatia majukumu yao ya kisheria na kiutendaji. Majadiliano hayo yaliibua mapendekezo muhimu yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira pamoja na kuimarisha uratibu na uwajibikaji wa wadau husika.

Sambamba na hilo, kikao hicho kilibainisha mikakati ya pamoja itakayotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wa mazingira, kwa lengo la kuimarisha na kudumisha usafi wa mazingira kwa namna endelevu katika Jiji la Dodoma.

Wadau wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), TANROADS, TARURA, LATRA pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

NEMC YAWALETA PAMOJA WATUMISHI WAKE KUJIPANGA KWA MWAKA 2026

 Ni katika kufanya tathmini na kuimarisha umoja. 

Watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Makao Makuu na kutoka kanda zote 13 nchini, wamekutana katika eneo la Ndotopolepole, Wilaya ya Bagamoyo, katika hafla maalum iliyolenga kuimarisha mshikamano, kujengeana uelewa, kufanya tathmini fupi ya utendaji kazi na kufurahi pamoja, ikiwa pia ni sehemu ya kufunga mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amewataka watumishi wa Baraza kudumisha umoja na mshikamano katika utendaji kazi (team building), kufanya kazi kwa bidii na kuongeza nidhamu pamoja na unadhifu wa kazi, kama nguzo muhimu za kufanikisha maono na dira ya Taasisi katika mwaka 2026.

Dkt. Semesi ameongeza kuwa katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi, NEMC imejipanga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali, ambapo tayari baadhi ya mifumo ya ufuatiliaji wa mazingira imeanza kutumika, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kazi.

Hafla hiyo pia imehusisha utoaji wa zawadi kwa watumishi walioonesha utendaji kazi mzuri na bidii, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ari, nidhamu na ushindani chanya mahali pa kazi.

Akitoa pongezi kwa wafanyakazi waliofanya vizuri, Dkt. Semesi aliipongeza menejimenti na watumishi wote wa NEMC kwa ujumla, na kuwasihi kuongeza bidii, ubunifu na ari mpya katika kutekeleza majukumu yao kwa mwaka 2026.

Aidha, hafla hiyo ilipambwa na michezo mbalimbali ya kujenga ushirikiano, mshikamano na moyo wa kutokata tamaa katika kazi, ambapo washindi walitunukiwa zawadi kama motisha.





















NEMC YASHIRIKI UTEKETEZAJI WA VIELELEZO VYA DAWA ZA KULEVYA MKOANI MTWARA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini tarehe 15 Novemba 2025 lilishiriki kusimamia na kushuhudia Uteketezaji wa vielelezo mbalimbali vya Mahakama Kanda ya Kusini ambavyo ni madawa ya kulevya vyenye Kilogramu 73. Vielelezo hivyo viliteketezwa katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Mkoani Mtwara

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th United Nations Environment Assembly – UNEA-7) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya kuanzia 08 hadi 12 Disemba 2025 

Baadhi ya masuala yanayojadiliwa katika Mkutano huu ni pamoja na Mazingira Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi; Uchumi Mzunguko, Chemikali, Taka na Uchafuzi wa Mazingira; Utawala na Sheria; na Bajeti.

Mkutano huu unaoongozwa na Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira, awali ulitanguliwa na mkutano wa maandalizi wa Kamati ya wawakilishi uliofanyika jijini hapo tarehe 01 hadi 05 Disemba 2025 ambapo wakuu wa nchi wanachama watatoa hotuba katika mkutano huo.

Zaidi ya NEMC, washiriki wengine ni Pamoja na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) na Wakala wa Misitu (TFS) ambapo Kilele cha mkutano huu ni tarehe 11 na 12 Disemba 2025.

𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐇𝐀𝐌𝐀𝐒𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐒𝐀𝐅𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐙𝐈𝐍𝐆𝐈𝐑𝐀 𝐒𝐇𝐈𝐌𝐌𝐔𝐓𝐀 𝟐𝟎𝟐𝟓 - 𝐌𝐎𝐑𝐎𝐆𝐎𝐑𝐎

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia wanamichezo wake wanaoshiriki mashindano ya SHIMMUTA 2025 mkoani Morogoro wakichagizwa na kauli mbiu yao isemayo "𝑴𝒊𝒄𝒉𝒆𝒛𝒐 𝒏𝒊 𝑨𝒇𝒚𝒂, 𝑴𝒂𝒛𝒊𝒏𝒈𝒊𝒓𝒂 𝒏𝒊 𝑼𝒉𝒂𝒊" wameshiriki zoezi la kufanya usafi kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro siku ya kufunga mashindano hayo Disemba 6, 2025.

Wanamichezo hao wamefanya usafi huo ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa usafi wa Mazingira kwa watumishi wanaoshiriki mashindano hayo pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Morogoro.

Imekuwa ni utaratibu wa kawaida kwa wanamichezo hao kuhamasisha usafi wa Mazingira kila mwaka kwenye mashindano ya SHIMMUTA huku wakienzi maono ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi kuhakikisha Mazingira yanakuwa safi na yanaendelea kulindwa nchi nzima.

NEMC imeshiriki mashindano hayo ya SHIMMUTA 2025 ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya ya watumishi lakini pia kutumia fursa hiyo katika kutoa elimu kwa watumishi na Wananchi mkoani Morogoro kuhusiana na masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.

Katika kuhakikisha elimu inafika kwa watu wa rika zote pia wanamichezo hao wametoa elimu ya Mazingira na kukabidhi vifaa vya kuzolea na kuhifadhia taka katika Shule ya Msingi Mwere ambapo wanamichezo hao walikuwa wanatumia viwanja vya shule hiyo kwa ajili ya mazoezi kipindi chote wakiwa kwenye mashindano hayo.

Mashindano ya SHIMMUTA 2025 yenye Kauli Mbiu isemayo "𝑼𝒐𝒏𝒈𝒐𝒛𝒊 𝑰𝒎𝒂𝒓𝒂 𝒌𝒘𝒂 𝑴𝒊𝒄𝒉𝒆𝒛𝒐 𝑬𝒏𝒅𝒆𝒍𝒆𝒗𝒖: 𝑴𝒊𝒄𝒉𝒆𝒛𝒐 𝒏𝒊 𝑫𝒂𝒓𝒂𝒋𝒂 𝒍𝒂 𝑨𝒇𝒚𝒂, 𝑨𝒎𝒂𝒏𝒊, 𝑼𝒎𝒐𝒋𝒂, 𝒏𝒂 𝑴𝒔𝒉𝒊𝒌𝒂𝒎𝒂𝒏𝒐 𝒘𝒂 𝑲𝒊𝒕𝒂𝒊𝒇𝒂" yalianza rasmi Novemba 23, 2025 na kufungwa rasmi Disemba 6, 2025 kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima.







NEMC YAKUTANA NA MAKAMU WA RAIS MHE. BALOZI DKT. EMMANUEL JOHN NCHIMBI DODOMA

Ni katika kikao kazi cha kupitishana kwenye majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi kwenye kikaokazi cha kwanza na watendaji wake tangu kuteuliwa kwake chenye lengo la kupitishana kwenye majukumu ya utekelezaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake.

Makamu wa Rais, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na watumishi waliochini ya Ofisi hiyo wakiwemo NEMC katika kikaokazi cha kwanza tangu kuteuliwa kwake

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma kilihusisha Menejimenti na  watumishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Menejimenti ya Baraza pamoja na watendaji kutoka kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa masuala ya Carbon.

Akizungumza katika kikao hicho Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi amesema ni kikao cha kukumbushana wajibu tulionao kwa watanzania wa kudumisha Muungano pamoja na kusimamia masuala mazima ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini hasa ikizingatiwa dira ya maendeleo ya 2050 kipengele cha tatu kimezingatia masuala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira pamoja na Ustahimilivu wa masuala mazima ya mabadiliko ya Tabianchi.

 " Dhamana tuliyopewa ni kubwa, masuala ya Muungano, kutunza mazingira na uchumi wa buluu si vitu vya mchezo, ni lazima tumsaidie Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku miamoja (100) kutekeleza maagizo yahusuyo Muungano na Mazingira, tunao wajibu wa kuhakikisha Mazingira yanasimamiwa na kuhifadhiwa" Amesema Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Ametoa maagizo yafuatayo: kila mtumishi aisome ilani ya chama kilichopo madarakani pamoja na dira ya maendeleo ya 2050 kwani ndio msingi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali, masuala ya Muungano na Mazingira, Uchumi wa buluu, Carbon trade na nishati safi yasimamiwe na kutekelezwa kwa weledi,  malengo yote ya utekelezaji wa shughuli za Muungano na Mazingira yawe na namna sahihi ya ufuatiliaji na utekelezaji wake ili kufikia azma iliyokubaliwa.

Maagizo mengine ni kuandaa  mkakati wa mawasiliano utakaotoa muongozo wa namna ya kutangaza shughuli za mazingira, kuzingatia haki na stahiki za watumishi, kuhakikisha vijana wanaelewa maana halisi ya Muungano na kuuenzi pamoja na wakuu wa Taasisi kusimamia Sheria na  miongozo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema NEMC inahitaji kupewa meno kwani kero za Mazingira zimekuwa nyingi hasa uchafuzi wa vyanzo vya maji na kelele chafuzi za Mazingira.

"Hakuna kitu kinanikera kama pale ocean road kila nikipita napakuta pachafu, panatoa harufu, matakataka yamezagaa, nikiwauliza NEMC.wanasema hawana meno" Mhe. Mhandisi Hamad Masauni.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja alipozungumza aliahidi kuyasimama na kuyatekeleza maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa  kwa kushirikiana na watendaji wa Taasisi zote zilizo chini ya ofisi ya Makamu wa Rais.

Kikao kazi hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Katibu Mkuu Mazingira Profesa Peter Msoffe na Naibu Katibu Mkuu Muungano Bw. Abdallah H. Mitawi.




𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐌𝐀𝐀𝐃𝐇𝐈𝐌𝐈𝐒𝐇𝐎 𝐘𝐀 𝐒𝐈𝐊𝐔 𝐘𝐀 𝐖𝐀𝐋𝐄𝐌𝐀𝐕𝐔 𝐃𝐔𝐍𝐈𝐀𝐍𝐈

𝐘𝐚𝐬𝐡𝐢𝐤𝐚  𝐦𝐤𝐨𝐧𝐨 𝐊𝐢𝐭𝐮𝐨 𝐜𝐡𝐚 𝐄𝐫𝐢𝐜 𝐌𝐞𝐦𝐨𝐫𝐢𝐚𝐥 𝐌𝐨𝐫𝐨𝐠𝐨𝐫𝐨

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia timu yake ya wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya SHIMMUTA 2025 wametembelea Kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Erick Memorial mkoani Morogoro Disemba 4, 2025.

Timu hiyo ya NEMC ilipata fursa ya kutembelea, kufariji na kuwapa misaada ya vyakula na vifaa vya usafi pamoja na kutoa elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni sehemu ya kuienzi siku maalumu ya walemavu ambapo duniani kote hufanyika tarehe 3 Disemba ya kila mwaka.

Akizungumza kwenye kituo hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Afisa Utumishi Mkuu wa NEMC Bi. Shukrani Haule amesema Baraza linaendelea kushirikiana na watu wa makundi yote katika kuhakikisha Mazingira yanakuwa safi na  salama kwa watu wote, lakini pia kihakikisha makundi haya yanawezeshwa na kujumuishwa katika maamuzi yanayozingatia Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.

"Baraza katika kutekeleza majukumu yake linashirikiana na watu wote na kundi hili la watu wenye ulemavu limekuwa likilizingatiwa siku zote katika mipango yake yote" Amesema Bi. Shukrani.

Naye Mtendaji wa Taasisi hiyo ya Eric Memorial, Bw. Robert Mkalawa ametoa wito kwa Taasisi za Serikali kuona umuhimu wa siku hii kama ambayo NEMC imefanya.

"Tunashukuru kutembelewa Taasisi inayohusika na Mazingira ambao ni NEMC na hii inadhihirisha kuwa hakuna Mazingira bila watu na watu wenyewe ndio sisi bila kubagua, lakini nitoe rai kwa Taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano wa NEMC katika kuadhikisha siku hii ya Walemavu Duniani". Amesema Bw. Robert.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo NEMC Bw. Fortinatus Patrick amesema kilichofanyika ni muendelezo wa kile alichokisisitiza Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi katika kuweka Mazingira wezeshi kwa makundi yote kujumuisha jamii za watu wenye ulemavu katika kuhifadhi Mazingira nchini.



NEMC YATAMBUA USHIRIKIANO KATI YAKE NA JESHI LA POLISI

Yashiriki mahafali ya kumi ya programu za vyuo vya polisi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetambua mchango wa ...