Nyumbani

NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA JIJINI DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuonesha dhamira yake katika kuimarisha usafi wa mazingira kwa kushiriki kikao kazi cha wadau kilicholenga kutathmini utekelezaji wa afua mbalimbali za usafi wa mazingira kilichofanyika Januari 19, 2026 katika jiji la Dodoma.

Kikao hicho, kilichoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora yanayochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya jiji kwa ujumla.

Akitoa mada ya ufunguzi, Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Bw. Novatus Mushi, aliwasilisha juhudi na mikakati inayotekelezwa na Baraza katika kuimarisha usafi wa mazingira Jijini Dodoma. Katika wasilisho lake, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, mamlaka za Serikali za mitaa na wadau wengine wa mazingira ili kufanikisha utekelezaji endelevu wa afua hizo.

Katika kikao hicho, wadau mbalimbali waliwasilisha taarifa na mada zinazohusu utekelezaji wa afua za usafi wa mazingira kwa kuzingatia majukumu yao ya kisheria na kiutendaji. Majadiliano hayo yaliibua mapendekezo muhimu yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira pamoja na kuimarisha uratibu na uwajibikaji wa wadau husika.

Sambamba na hilo, kikao hicho kilibainisha mikakati ya pamoja itakayotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wa mazingira, kwa lengo la kuimarisha na kudumisha usafi wa mazingira kwa namna endelevu katika Jiji la Dodoma.

Wadau wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), TANROADS, TARURA, LATRA pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YATAMBUA USHIRIKIANO KATI YAKE NA JESHI LA POLISI

Yashiriki mahafali ya kumi ya programu za vyuo vya polisi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetambua mchango wa ...