Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeshiriki uwasilishaji wa ripoti ya mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni kwenye sera ya Taifa ya Ardhi 1995 (Toleo la 2023) na mchakato wa NDC 3.0V uliofanyika katika ukumbi wa Residence Jijini Dodoma leo.
Akiwasilisha ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na WAHEAL na Tree of Hope, Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia kutoka Women Action Towards Entrepreneurship Development (WATED) Bi. Maria Matui amesema imelenga kuainisha changamoto za wanawake wa vijijini pamoja na kusaidia jitihada za mashirika katika kupaza sauti za wanawake kwenye masuala ya usimamizi wa ardhi na harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema wasilisho hilo lililohusisha pia wanachama wa mtandao wa mabadiliko ya tabianchi limeainisha changamoto nyingi wanazopitia wanawake wa vijijini zikiwemo, mila na desturi, mitazamo na mifumo dume hali inayoathiri masuala ya maendeleo hasa shughuli za uzalishaji.
Malengo makubwa matatu yaliyowasilishwa ni pamoja na kuweka wazi mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni katika utekelezaji wa Sera ya Ardhi ya 1995(Toleo la 2023, kushirikiana na Serikali katika kuboresha mchakato wa NDC.3.0V kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za makundi yote ya jamii pamoja na kutoa mapendekezo Sera shirikishi yatakayohakikisha usimamizi endelevi wa rasilimali na upatikanaji wa haki sawa kwa kila mmoja.
Baadhi ya washiriki wa wasilisho la Asasi ya WATED wakifuatilia wasilisho hilo lililofanyika katika ukumbi wa Residence leo Septemba 17, 2025 Dodoma
Mikoa iliyofikiwa na Asas hizi ni pamoja na Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Geita, Arusha, Mara, Kagera na Tanga.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni