Nyumbani

NEMC YAWATAKA WAMILIKI WA MABASI KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA BARABARANI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri pamoja na abiria kuboresha usafi katika mabasi na maeneo ya usafiri barabarani, kwa kuzuia tabia ya kutupa taka nje ya magari na kukojoa mabarabarani.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipokuwa akiongea na vyombo vya habari kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kusimamia Mazingira nchini. 

Amesema kumekuwepo na mitazamo iliyojengeka kwa abiria wa mabasi makubwa yanayoenda safari ndefu na fupi ya kutokuthamini mazingira na kuwa na tabia ya kutupa taka ovyo na kukojoa barabarani hali inayochafua mazingira, kuharibu hali ya hewa na kuhatarisha afya za jamii. 

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza na vyombo vya Habari wakati akitoa wito wa kuwataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuepuka uchafuzi wa mazingira.

“Mazingira safi ni haki ya kila Mtanzania, na ni jukumu letu sote kuhakikisha tunayahifadhi. Kutupa taka nje ya gari na kukojoa barabarani si tu ni tabia mbaya, bali pia ni ukiukwaji wa Sheria za mazingira. Tunawaomba wasafiri na wamiliki wa mabasi kushirikiana nasi kwa kuweka na kutumia vyombo vya kutupa taka ili tukome uchafuzi huu,” alisema Mkurugenzi Mkuu Dkt. Immaculate Sware Semesi

Aidha, NEMC imetahadharisha kuwa watakaobainika kutupa taka au kukojoa mabarabarani watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo faini na adhabu nyingine zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria za mazingira.

“Ninawahimiza watanzania wote kuwa mabalozi wa usafi katika maeneo wanayopitia. Tukichukua hatua sasa, tunaweza kulinda afya zetu na mazingira kwa vizazi vya sasa na baadae”.

NEMC imeendelea kutoa simu ya bure 0800 110 115 kwa ajili ya kuripoti uchafuzi wa Mazingira unaosababishwa na abiria, shughuli za binadamu, viwanda bubu au raia ili kuimarisha usimamizi na kuleta mabadiliko chanya katika jamii

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...