Nyumbani

NEMC YASHIRIKI MAPOKEZI YA BALOZI LUVANDA OFISI YA MAKAMU WA RAIS – DAR ES SALAAM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika hafla ya mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira), Mhe. Balozi Baraka Haran Luvanda, aliyepokelewa rasmi leo Februari 09, 2026 katika Ofisi za Makamu wa Rais baada ya kuapishwa Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira)Mhe. Balozi Baraka Haran Luvanda akipokea maua kutoka kwa Afisa Mazingira Mkuu Bi. Upendo Ntunguja wakati wa mapokezi katika Ofisi za Makamu wa Rais baada ya kuapishwa Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Hafla hiyo ya mapokezi imeongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Festo Dugange, pamoja na Viongozi na  Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mhe. Dkt. Dugange alimkaribisha rasmi Balozi Luvanda huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Taasisi zake katika kutekeleza agenda ya kitaifa ya Muungano na Uhifadhi wa Mazingira.

Kwa upande wake, Balozi Luvanda alishukuru kwa mapokezi mazuri aliyopatiwa na kuahidi kufanya kazi bega kwa bega na Taasisi zote zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, hususan katika kuimarisha Usimamizi na Uhifadhi wa mazingira nchini. 

Ameeleza kuwa, utekelezaji wa majukumu yake utaongozwa na maono ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuzingatia Sera, Sheria na Mikakati ya Taifa inayolenga Maendeleo Endelevu.

Aidha, Balozi Luvanda ameeleza dhamira yake ya kutumia uzoefu alionao katika kuimarisha Usimamizi wa Muungano, kulinda na kuhifadhi mazingira, pamoja na kuhakikisha Dira ya Taifa ya Muungano na Mazingira inatekelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Meneja wa Kanda ya Temeke, Bw. Abel Sembeka, alimpongeza Balozi Luvanda kwa kuteuliwa kwake na kumhakikishia ushirikiano wa karibu kutoka NEMC katika kutekeleza majukumu ya Usimamizi, Uhifadhi na ulinzi wa mazingira nchini.

Bw. Sembeka alieleza kuwa NEMC itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu, kusimamia utekelezaji wa Sheria za Mazingira, pamoja na kuimarisha elimu na uhamasishaji wa masuala ya mazingira kwa jamii na wadau mbalimbali, sambamba na mwelekeo na vipaumbele vya Dira ya Taifa ya 2050






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

BODI YA WAKURUGENZI NEMC YAFANYA MAPITIO YA MPANGO MKAKATI WA UTEKELEZAJI WA MIAKA MITANO

Bodi ya Wakurugenzi wa NEMC pamoja na Menejimenti wamefanya kikao katika Ukumbi wa Hoteli ya Adden Palace jijini Mwanza kufanya mapitio ya p...