Nyumbani

NEMC YASHIRIKI ZIARA YA NAIBU WAZIRI DKT. DUGANGE KAGERA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Festo Dugange kukagua Miradi ya Mazingira katika Halmashauri za Wilaya ya Karagwe na Misenyi Mkoni Kagera.




Ziara hiyo ililenga kuweka bayana Miradi ya kimazingira inayotekelezwa nchini Tanzania ili kufundisha umma wa watanzania namna ambavyo rasilimali za Mazingira zinaweza kuwa fursa za kiuchumi.

Miradi iliyotembelewa inajumuisha Mradi wa Vijana wa kuchakata taka za plastiki, Mradi wa biashara ya kaboni kupitia kilimo mseto (Kinoni Agroforestry Farm) unaotekelezwa na kampuni ya KADERES, Mradi wa Nishati safi ya kupikia na Mradi wa ujenzi wa Dampo la kuhifadhia maji taka Wilayani Karagwe.

Akizungumza na wananchi wakati wa ukaguzi wa Maeneo mbalimbali ya Miradi hiyo, Dkt.  Dugange amehamasisha jamii kuhusu fursa za kiuchumi zinazotokana na Mazingira ikiwemo Biashara ya kaboni pamoja usimamizi sahihi wa taka ngumu kwa ajili ya uchakataji na Urejelezaji. 

"Taka si taka tu bali ni rasilimali muhimu inayoweza kuleta manufaa ya kiuchumi, taka zinazooza zinaweza kutumika kutengeneza gesi na mbolea ya asili inayoweza kutumika kutengenezea bustani za kioganiki na kupata mazao asilia yasiyo na kemikali na kutunza rutuba ya udongo" Amesema Dkt. Dugange.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi (NEMC) Bw. Boniphace Guni amesema NEMC inaendelea na Usimamizi wa Miradi inayotekelezwa katika Kanda hiyo ikiwemo Mkoa wa Kagera na pia itaendelea kuongeza juhudi za kuhakikisha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira inatekelezwa nchini kote ili kuhakikisha Mazingira yanalindwa na kutunzwa.

Aidha, ameisisitiza Jamii kuendelea kutunza Mazingira ili kudhibiti majanga ya kimazingira na kiafya yanayoendelea kushamiri  yakiwemo ongezeko la joto, Upungufu wa Mvua, ukame, na magonjwa.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YASHIRIKI ZIARA YA NAIBU WAZIRI DKT. DUGANGE KAGERA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. ...