Nyumbani

NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA 48 CHA KAMATI YA URITHI WA DUNIA YA UNESCO - BUSAN KOREA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Dkt. Immaculate Semesi, linashiriki katika Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO (48th Session of the World Heritage Committee) kinachofanyika jijini Busan, Jamhuri ya Korea.

Kikao hicho kinawakutanisha wajumbe kutoka Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, pamoja na wadau mbalimbali wa kimataifa, kwa lengo la kupitia, kujadili na kufanya maamuzi kuhusu masuala ya uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya maeneo ya Urithi wa Dunia. Vilevile, kikao kinatoa fursa ya kutathmini hali ya uhifadhi wa maeneo yaliyopo kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia, kuzingatia mapendekezo ya maeneo mapya yanayostahili kuorodheshwa, pamoja na kujadili changamoto zinazoathiri urithi wa asili na wa kiutamaduni duniani, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za kibinadamu na uendelezaji usiozingatia misingi ya uhifadhi.

Ushiriki wa NEMC katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuendelea kutekeleza kikamilifu Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, kuimarisha usimamizi wa maeneo ya urithi wa dunia nchini, na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kuhifadhi urithi wa asili na wa kiutamaduni wenye thamani ya kipekee kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Katika mkutano huo, Dkt. Semesi anawakilisha Tanzania katika mijadala mbalimbali inayohusu uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia, usimamizi wa mifumo ya ikolojia, uhifadhi wa bioanuwai, pamoja na matumizi ya mbinu za kisayansi na mifumo bora ya usimamizi wa mazingira ili kuhakikisha maeneo hayo yanaendelea kuhifadhiwa kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.

Aidha, ushiriki wa Tanzania ukiongozwa na Mheshimiwa Balozi Saidi Yakubu,Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu UNESCO na kuhudhuriwa pia na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera na Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ( Mb),unatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na taasisi za kimataifa kama UNESCO na IUCN, kubadilishana uzoefu na nchi nyingine kuhusu mbinu bora za uhifadhi wa maeneo ya urithi, pamoja na kutafuta fursa za ushirikiano wa kiufundi na kifedha kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa maeneo ya Urithi wa Dunia nchini Tanzania.

Tanzania ni miongoni mwa Mataifa Wanachama wa Mkataba wa Urithi wa Dunia na inajivunia kuwa na maeneo kadhaa yaliyotambuliwa na UNESCO kuwa ni Urithi wa Dunia kutokana na thamani yake ya kipekee ya kimataifa. Ushiriki wa NEMC katika kikao hiki unaimarisha nafasi ya Tanzania katika mijadala ya kimataifa kuhusu uhifadhi wa mazingira na urithi wa dunia, sambamba na kuendeleza diplomasia ya mazingira na kukuza mchango wa nchi katika utekelezaji wa ajenda za maendeleo endelevu duniani.

NEMC NA IUCN WAKUSANYA MAONI YA WADAU KUHUSU RASIMU YA KANUNI ZA WAJIBU WA MZALISHAJI WA BIDHAA (EPR)

 


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na IUCN, limeanza mkutano wa siku mbili wa wadau kuhusu Rasimu ya Kanuni ya Wajibu wa Mzalishaji wa Bidhaa (Extended Producer Responsibility - EPR) katika Usimamizi wa Taka na Uhifadhi wa Mazingira. Mkutano huo umeanza rasmi tarehe 21 Julai 2026 mkoani Dodoma na unalenga kukusanya maoni ya wadau ili kuboresha rasimu ya kanuni hiyo kabla ya kukamilishwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bw. Fredrick Mulinda, ambaye ni Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC, amesema mkutano huo ni muhimu katika kujadili na kutoa maoni kuhusu Rasimu ya Kanuni za Wajibu wa Mzalishaji wa Bidhaa (EPR) katika Usimamizi wa Taka na Uhifadhi wa Mazingira. Amesema mkutano huo unaonesha dhamira ya pamoja ya Serikali na wadau mbalimbali katika kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira nchini kupitia mfumo utakaoweka wajibu kwa wazalishaji wa bidhaa katika usimamizi wa taka zinazotokana na bidhaa zao.

Aidha, Bw. Mulinda ameishukuru IUCN kwa ushirikiano wake wa karibu na NEMC katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi na kusimamia mazingira. Pia amewapongeza wataalamu wa NEMC na wadau wote walioshiriki maandalizi ya mkutano huo muhimu, akisisitiza kuwa ushirikiano wao utachangia kupatikana kwa kanuni imara zitakazoboreshwa kupitia maoni ya wadau.

KWAGILWA AFUNGIA KIWANDA CHA HANGJIN STEEL MKURANGA KWA UKIUKWAJI WA SHERIA ZA MAZINGIRA

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amesimamisha shughuli za Kiwanda cha Hangjin Steel kinachojihusisha na uzalishaji wa nondo kwa kutumia vyuma chakavu, kilichopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, baada ya kubainika kukiuka masharti ya Sheria ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa Sheria na Kanuni za Mazingira, ambapo ilibainika kuwa shughuli za kiwanda hicho zilikuwa zinasababisha athari kwa mazingira kutokana na kutokuzingatia masharti yaliyowekwa na mamlaka husika za usimamizi wa mazingira.

Miongoni mwa dosari zilizobainika ni kutokuwepo kwa mfumo wa udhibiti wa taka ndani ya kiwanda, kushindwa kudhibiti mafuta machafu yanayotumika kama chanzo cha nishati na hivyo kuchanganyika na maji na kutiririka kwenye makazi ya wananchi pamoja na mabonde ya maji. Aidha, kiwanda hicho kilibainika kutokuwa na mfumo madhubuti wa kudhibiti hewa chafu inayozalishwa na shughuli zake, pamoja na kukosa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) kinachotakiwa kisheria.

Mhe. Kwagilwa ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na mamlaka za mazingira kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake. Maelekezo hayo yanajumuisha kurekebisha dosari zote zilizobainika, kuweka mifumo madhubuti ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira na kutimiza matakwa yote ya kisheria yanayohusu usimamizi wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema amepokea maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Naibu Waziri na kuahidi kuwa Baraza hilo litayatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili kuhakikisha sheria inazingatiwa na mazingira yanaendelea kulindwa.

NEMC YASHIRIKI HAFLA YA KUKABIDHI MALI ZA MRADI WA KUHIMILI MABADILIKO YA TABIANCHI - KONGWA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika hafla ya kufunga na kukabidhi mali za Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Enhancing Climate Change Adaptation for Agro-Pastoral Communities in Kongwa District).

Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) umekuwa ukitekelezwa katika Kata za Ugogoni na Mtanana, ukinufaisha jumla ya vijiji 12 chini ya usimamizi wa NEMC na utekelezaji wa Foundation for Energy, Climate and Environment (FECE) pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Kongwa.

Mradi umewezesha afua mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu, mifugo na kilimo, ujenzi wa miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji wa matone, josho, manywesheo ya mifugo pamoja na upandaji miti.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amelipongeza shirika la FECE pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kusimamia mradi huo. Amesema mradi huo unachangia katika kutekeleza Dira ya Taifa ya 2025-2050, agenda ya kukijanisha Tanzania pamoja na Sera na Sheria za usimamizi wa mazingira.

Akizindua kisima cha maji kilichojengwa na mradi huo katika kiiji cha Mautya A, Dkt. Semesi amewapongeza wananchi kuwa sehemu ya wanufaika wa mradi huo na kutoa wito kwao kulinda miundombinu ya kisima hicho na kukichukulia kama mali yao.

Aidha, kwa nyakati tofauti tofauti, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa, Diwani wa Kata ya Ugogoni pamoja na viongozi wengine wameishukuru NEMC kwa usimamzi wa mradi huu pamoja na kuahidi kuulinda ili uweze kutoa huduma endelevu.

NEMC YATUNUKU TUZO WASHINDI WA MAZINGIRA CHALLENGE, YAINGIA MAKUBALIANO NA MABALOZI WA MAZINGIRA SABASABA


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), tarehe 11 Julai, 2026, limeadhimisha Siku ya Mazingira katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyofanyika katika Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam, ambapo liliwatunuku vyeti na tuzo washindi wa Mazingira Challenge, kusaini Hati za Makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) pamoja na Mabalozi wa Mazingira. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Serikali, wadau wa mazingira, washirika wa maendeleo, sekta binafsi, wasanii na wananchi.

Shindano la Mazingira Challenge ni sehemu ya mkakati wa NEMC wa kuibua na kuhamasisha ubunifu unaochochea utunzaji wa mazingira, hususan miongoni mwa vijana na makundi mbalimbali ya jamii. Vilevile, kusainiwa kwa Hati za Makubaliano (MoU) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) pamoja na Mabalozi wa Mazingira kunalenga kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa elimu ya mazingira, kuendesha kampeni za uhamasishaji na kuongeza ushiriki wa wananchi katika juhudi za uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira nchini.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kulinda mazingira na kuhimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa sera, mipango na programu za uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi, alisema maadhimisho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kutoa elimu kwa umma, kutambua mchango wa wadau mbalimbali na kuhamasisha ubunifu katika usimamizi wa mazingira. Alibainisha kuwa NEMC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuimarisha utoaji wa elimu ya mazingira, kuhamasisha matumizi endelevu ya rasilimali za mazingira na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Maadhimisho hayo yalipambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali waliotumia sanaa kuhamasisha utunzaji wa mazingira, huku wananchi waliotembelea Kijiji cha Mazingira wakiendelea kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya mazingira na huduma zinazotolewa na NEMC pamoja na wadau wake. Hafla hiyo imeonesha dhamira ya Serikali na NEMC ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali katika kujenga jamii inayowajibika kwa mazingira na kuendeleza ajenda ya maendeleo endelevu nchini.




DKT. MUYUNGI AIPONGEZA NEMC KUHUSISHA VIJANA WENYE UBUNIFU - KIJIJI CHA MAZINGIRA


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi amevutiwa na Kijiji cha Mazingira katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Dkt. Muyungi amesema kilichomvutia zaidi ni kuona namna ambavyo vijana wabunifu wamepewa nafasi ya kuonesha ujuzi wao katika kutumia fursa zinazopatikana kwenye Mazingira kupitia kampeni ya Taka ni Fursa.

Dkt. Muyungi amesema kuna haja ya kuwawezesha vijana wenye mitaji midogo ili waweze kufanya mambo makubwa kupitia ubunifu wao kwenye kutumia fursa mbalimbali za urejelezaji na uchakataji taka ili kujipatia kipato na kusafisha Mazingira.

Dkt. Muyungi aliambatana na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipotembelea Kijiji cha Mazingira mara baada ya kushiriki hafla ya ufunguzi waaonesho hayo Julai 3,2026.

NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA 48 CHA KAMATI YA URITHI WA DUNIA YA UNESCO - BUSAN KOREA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Dkt. Immaculate Semesi, linashiriki katika Kikao ...