Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam linaendesha zoezi maalumu la Ukaguzi wa Mazingira kwa Miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mfumo maalumu wa kidigitali uitwao 'Mazingira App'.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti amesema zoezi hilo litadumu kwa wiki nne na litahusisha kaguzi za Mazingira kwenye miradi ya maendeleo hususani kuangalia uzingatiaji wa matakwa ya Usimamizi wa Mazingira kama vile usimamizi wa taka, matumizi sahihi ya ardhi pamoja na uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Aidha Bw. Jamal Baruti amesema ushirikiano na uongozi wa Jiji la Dar es salaam umelenga kuongeza uelewa na ufanisi kwa maafisa mazingira kuhusu Usimamizi hafifu wa taka ngumu, changamoto ya taka za plastiki, uharibifu wa Mazingira kutokana na uchimbaji holela wa kwenye mito na mabonde na matumizi holela ya ardhi kinyume na taratibu za mipangomiji.
Kwa upande wake Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki (NEMC) Bi. Glory Kombe alipozungumza amewataka Viongozi wa Halmashauri na Serikali za mitaa kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi hili ili kufikia tija tarajiwa kwa maendeleo endelevu ya Mazingira nchini.
Kadhalika Meneja Glory Kombe amefafanua kuwa jukumu la Halmashauri na Mamlaka za Serikali za mitaa ni kuhakikisha Miradi ya maendeleo inazingatia taratibu za Mazingira ikiwemo ufanyikaji wa Tathmini ya Mazingira na Jamii kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Mazingira na Kanuni zake na kusimamia usafi wa Mazingira kwa ujumla pamoja na kuwataka maofisa Mazingira na Kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.
Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki Bi. Glory Kombe (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huoMeneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC)Bw. Hamadi Taimuru (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huo
NEMC imeanzisha mfumo huo wa Mazingira app' ambao ni wa kidigitali ili kurahisisha na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji na uhifadhi wa Taarifa za Miradi pamoja na usajili wa Miradi mipya ambapo zitachangia Baraza na Serikali kupanga na kusimamia Miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.