Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) wameimarisha ushirikiano wao kuingia makubaliano ya pamoja ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha siku mbili kilichofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 8 Oktoba 2025, ambapo wajumbe wa Bodi na wataalamu kutoka taasisi zote mbili walikutana kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati wa kikao hichoKupitia kikao hicho, taasisi hizo zimeweka msingi wa ushirikiano madhubuti katika maeneo mbalimbali, yakiwemo matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika usimamizi wa mazingira, ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria na Kanuni za mazingira, pamoja na kuimarisha mawasiliano ya mara kwa mara kati ya pande hizo mbili.
Aidha wamekubaliana pia kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar inazingatia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa Kikao hicho
Mwenyekiti wa Bodi ya ZEMA Bi. Asha Ali Khatib akizungumza wakati wa Kikao hicho
Akizungumza na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2020/2050, ambayo inaweka mazingira kama mojawapo ya nguzo kuu za maendeleo ya Taifa.
Amesisitiza kuwa mashirikiano hayo yataongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusaidia kufanikisha malengo ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira kwa maslahi ya wananchi na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ZEMA, Bi. Asha Ali Khatib, amesema kikao hicho kimetoa fursa kwa wataalamu wa pande zote mbili kujifunza kutoka kwa wenzao, na pia kuibua mbinu mpya za kuboresha utendaji.
Ameongeza kuwa ushirikiano huu utawezesha uwiano wa kisera na kiutekelezaji katika masuala ya mazingira baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Picha ya pamoja ya Menejimenti ya NEMC na ZEMA mara baada ya Kikao hicho. Wa nne kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya ZEMA Bi. Asha Ali Khatib, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa ZEMA Sheha Mjaja Juma