Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa kushirikiana na Taasisi ya ECCT (Environment Conservation Community of Tanzania) wamehitimisha takribani wanafunzi 22 wa Mradi wa '𝗘𝗰𝗼𝘄𝗲𝗮𝗿' waliokuwa wakipatiwa mafunzo yaliyobeba agenda ya mazingira kwenye ubunifu na Sanaa ya mitindo yenye lengo la kujenga ujasiliamali wa kijani, kupambana na taka ngumu za Sekta ya nguo na mitindo sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali.
Mafunzo ya Mradi huo yalijikita kufundisha juu ya ubunifu wa bidhaa mbalimbali kupitia nguo zilizotumika na mabaki ya vitambaa ambapo ni Utekelezaji wa dhana ya 𝗣𝘂𝗻𝗴𝘂𝘇𝗮, 𝗧𝘂𝗺𝗶𝗮 𝘁𝗲𝗻𝗮 𝗻𝗮 𝗥𝗲𝗷𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮 kwa mustakabali wa utunzaji wa Mazingira na fursa za kiuchumi.
Akizungumza katika mahafali hiyo, mgeni rasmi, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi ameipongeza Taasisi ya ECCT na wahitimu wote kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuwataka kuyazingatia kwa manufaa ya kiuchumi na Mazingira.
Picha ya pamoja ya wahitimu, mgeni rasmi pamoja na viongozi wa Mradi huo mara baada ya kumalizika kwa hafla ya mahafali hayo
"Mmepata elimu, ujuzi, maarifa, mmeelewa changamoto za mazingira, sasa ni wakati wa kupeleka hayo yote kwa jamii zetu.Tuna matarajio makubwa kwenu kama mabalozi wa mitindo endelevu na watetezi wa mazingira. endeleeni kushirikiana, kushirikishana maarifa na kuamini kuwa sauti zenu na kazi zenu zinaweza kuleta mabadiliko." Alisisitiza Bi. Amina.
Bi. Amina pia ametumia fursa hii kutoa elimu kuhusu katazo la vifungashio vya plastiki kwa mujibu wa kanuni ya katazo hilo na kuwataka wahitimu wa Mradi huo kubuni na kutengeneza vifungashio vinavyoenda sambamba na mustakabali wa utunzaji wa Mazingira.
Mgeni rasmi, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akizungumza katika mahafali hayo
Baadhi ya wahitimu wa Mradi wa ECOWEAR katika mahafali hayo
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ECCT, Bi. Lucky Michael amelishukuru Baraza kwa mchango wake kufanikisha kuhitimisha wanafunzi hao huku akiainisha mafanikio ya Mradi huo ikiwa ni pamoja na kujengea uwezo wanafunzi hao ubunifu na mitindo,kukusanya takribani tani 2 za mabaki ya nguo na vitambaa kuzigeuza kuwa bidhaa zenye ubora pamoja na kuhamasisha jamii kupunguza taka na kutumia mitindo endelevu.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya ECCT Bi. Lucky Michael akizungumza katika mahafali hayo
Wahitimu wa Mradi wa ECOWEAR wakionesha baadhi ya kazi zao ambazo ni matokeo ya mafunzo ya Mradi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni