Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Utekelezaji wa Mkataba wa Bioanuai unaoendelea Jijini Panama kuanzia tarehe 20 hadi 30 Novemba 2025.
Tanzania, ikiwa ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Bioanuai (Convention on Biological Diversity – CBD), imeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya bioanuai. Mkutano huu unafanyika katika Ukumbi wa Atlapa Convention Center na unahusisha mikutano miwili mikubwa: SABSTTA-27, inayojadili masuala ya kisayansi, kiufundi na kiteknolojia kuhusu bioanuai; na SB8J-1, inayohusiana na haki na mchango wa jamii za wenyeji katika hifadhi ya bioanuai.
Kupitia ushiriki wake, NEMC imeungana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (TFS na TAWA), pamoja na Shirika la The Nature Conservancy (TNC). Majadiliano katika mikutano hii yamejikita kwenye utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai (Kunming–Montreal Global Biodiversity Framework – KMGBF) uliopitishwa mwaka 2022, yakilenga kuweka miongozo ya kuboresha sera, sheria na programu za kitaifa kuhusu hifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Aidha, mada kuu zinazojadiliwa ni pamoja na bioanuai na mabadiliko ya tabianchi, bioanuai na afya, viumbe vamizi, bioanuai na kilimo, pamoja na tathmini za athari za viumbe hai vilivyobadilishwa kijenetiki (LMOs).
Kwa Tanzania, ushiriki huu ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na mataifa mengine kuhusu njia bora za kudhibiti upotevu wa bioanuai na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia jukwaa hili, NEMC inaimarisha nafasi yake katika kuunganisha taaluma, sayansi, na jamii katika utekelezaji wa KMGBF, sambamba na kuandaa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji bora wa sera za mazingira nchini.
Vilevile, majadiliano haya yanatoa nafasi ya kuandaa msimamo wa pamoja wa kikanda kuelekea Mkutano wa 17 wa Mkataba wa Bioanuai utakaofanyika Jijini Yerevan, Armenia mwaka 2026.
Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika mkutano huu ni ushahidi wa dhamira ya Tanzania katika kulinda mazingira na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za asili. Unasisitiza kuwa uhifadhi wa bioanuai ni nyenzo muhimu katika kulinda afya ya jamii, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha usalama wa chakula.
NEMC inaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuhakikisha malengo ya kimataifa ya bioanuai yanatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa na dunia kwa ujumla.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni