Nyumbani

KATIBU MKUU DR. RICHARD MUYUNGI AKUTANA NA MENEJIMENTI YA NEMC

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo amekutana na Menejimenti ya Baraza kwa lengo la kujitambulisha na kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.



Katika kikao kilichohusisha pia Mameneja wa Kanda 13 nchi nzima kiliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Baraza, ikiwemo mafanikio yaliyofikiwa, changamoto za mazingira zinazojitokeza pamoja na hali ya mazingira kwa ujumla. 

Aidha, ziliainishwa pia fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya mazingira  hususani eneo la urejelezaji wa taka zinazoweza kuvutia uwekezaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi endelevu wa mazingira.

Dkt. Richard Muyungi alipozungumza  ameishukuru NEMC kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi na kusimamia mazingira ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sheria

Amesisitiza umuhimu wa Baraza  kuzingatia mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya sasa ya jamii ili kuendana na ulimwengu wa kidigitali katika kufikisha elimu ya  Mazingira kwa jamii.

Katika maelekezo yake, Dkt. Muyungi ameitaka NEMC kuanzisha kitengo cha Ubunifu  kitakachokuwa na jukumu la kubuni na kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mazingira, ikiwemo kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia bunifu na endelevu.

Vilevile amesisitiza kuzingatiwa kwa weledi katika uchakataji na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na misingi ya uhifadhi wa mazingira.

Sambamba na hilo, aliagiza kuimarishwa kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa itakayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na za haraka za mazingira, jambo litakalosaidia katika kufanya maamuzi yenye tija na kulinda rasilimali za taifa.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Dkt. Muyungi kufika na kuzungumza na Menejimenti ya NEMC tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na imeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na uratibu wa masuala ya mazingira nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YATAMBUA USHIRIKIANO KATI YAKE NA JESHI LA POLISI

Yashiriki mahafali ya kumi ya programu za vyuo vya polisi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetambua mchango wa ...