Nyumbani

NEMC YAKABIDHIWA RASMI MAABARA INAYOTEMBEA KUIMARISHA KAGUZI ZA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhiwa rasmi Maabara inayotembea na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) mahususi kwa ajili ya Kaguzi za Mazingira hususan kupima sampuli za kimazingira zikijumuisha za Ubora wa maji, Kelele, udongo, kemikali, madini tembo, hewa na sampuli nyinginezo za kimazingira.

Maabara hiyo ni manufaa ya Mradi wa kujenga uwezo kwa Taasisi za Serikali na binafsi (EMA Project) unaotekelezwa na NEMC kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la watu wa Sweden (SIDA).

Akizungumza wakati wa mapokezi ya Maabara hiyo yaliyofanyika katika Ofisi za NEMC Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema Maabara hiyo itasaidia kupunguza gharama na muda uliokuwa ukitumika kusafirisha sampuli kwenda maabara nyingine zilizoidhinishwa, ambapo gharama ya kipimo kimoja ilikuwa inaweza kufikia kati ya Shilingi za kitanzania milioni 5 hadi 10 kulingana na aina ya sampuli.

Ameongeza kuwa "kwa sasa NEMC itaweza kufanya uchunguzi ndani ya muda mfupi na kuchukua hatua stahiki mara moja, hali itakayoongeza ufanisi katika kulinda mazingira".

Akikabidhi Maabara hiyo kwa niaba ya Shirika la SIDA, Meneja Miradi ya Nishati na Mazingira, Stephen Mwalufamba kutoka Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania ameeleza kuwa lengo kubwa la Miradi huo ni kuchangia juhudi za Serikali katika maswala ya Maendeleo na kuchangia Mazingira endelevu Kwa ajili ya ustawi wa wananchi huku akiipongeza NEMC kwa jitihada wanazofanya katika kutekeleza jukumu la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa EMA (NEMC) Bw. Paul Kalokola amesema "Maabara hiyo inavifaa vya kisasa vinavyoweza kutoa matokeo ya kisayansi kwa usahihi. Pia Maabara hiyo ina Kamera ya juu (Drone) inayoweza kusafiri umbali mrefu na kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi".

Mradi wa huo ulianza mnamo Juni 2020 na unatarajiwa kuisha mwezi Juni 2026 ambapo ulilenga kujenga uwezo kwa Taasisi za Serikali na binafsi kutekeleza Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 sura namba 191 ipasavyo.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YAKABIDHIWA RASMI MAABARA INAYOTEMBEA KUIMARISHA KAGUZI ZA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhiwa rasmi Maabara inayotembea na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA)...