Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) amewataka Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali pamoja na wadau wengine wa Elimu kwa Umma kutumia nafasi zao kuwaunganisha Watanzania kwa kutoa taarifa zenye kuleta tija kwa jamii kwa kuzingatia weledi, ujuzi na ubunifu.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ametoa wito huo alipokuwa akifungua Mkutano wa 110 wa Wadau wa Elimu kwa Umma unaofanyika jijini Arusha kuanzia Machi 23 hadi 27, 2025 katika Ukumbi wa PAPU akiwa ndiye Mgeni Rasmi ambapo amewataka wadau hao wa elimu kwa Umma ambao asilimia kubwa ni Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano wa Serikali kuhakikisha wanaongeza ubunifu katika kufikisha taarifa zenye kuwaunganisha Watanzania.
"Tumieni nafasi zenu kuunganisha Watanzania na kupitia mada zinazofundishwa ni imani yangu kwamba zitaongeza weledi na ujuzi, hivyo tumieni vizuri kuongeza ubunifu katika kuwaeleza wananchi kuhusu mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali" Amesema Dkt. Mwigulu.
Pia Dkt. Mwigulu amesisitiza Wadau hao wa elimu kwa Umma kujenga utamaduni wa kufanya Tafiti kupata taarifa sahihi kabla ya kupeleka kwa wananchi huku akiwataka wadau hao kuhakikisha wanatoa taarifa wakiwa na uelewa juu ya taarifa hizo wanazozitoa.
"Ni lazima msome na kuelewa kile mnachokipeleka kwa wananchi, huku mkihakikisha kwamba mnalinda Taswira za Taasisi zenu" Amesisitiza Dkt. Mwigulu.
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ni moja kati ya Taasisi zinazoshiriki Mkutano huo kwa kuwakilishwa na Afisa Uhusiano na Mawasiliano wake, Bw. Tajiri Kihemba ikizingatiwa kwamba NEMC ni kati ya wadau Muhimu wa masuala ya utoaji wa elimu kwa Umma katika eneo la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini.
Mkutano huu umeandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa wadau wa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kutimiza jukumu hilo muhimu ili kufanikisha kufikisha taarifa kwa Watanzania na wadau wengine wa maendeleo nchini.






.jpeg)



Hakuna maoni:
Chapisha Maoni