Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Asasi Binafsi ya Bora Women Go Green limeandaa Kongamano la uzinduzi wa mtambo wa Nishati safi ya kupikia aina ya haidrojeni likiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini lililofanyika leo Machi 25, 2026 katika Ukumbi wa Nkurumah Hall wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi wa mtambo huo, Mgeni rasmi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Festo Dugange amesema uzinduzi wa mtambo huo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Aidha Dkt. Dungage amesisitiza kuwa ili kukabiliana na changamoto na athari za mazingira na zile za mabadiliko ya tabianchi, ni lazima kuongeza jitihada za Utunzaji na Usimamizi wa mazingira, kuwekeza kwenye vyanzo vya nishati mbadala na kuwa na mifumo ya kusaidia kustahimili mabadiliko ya tabianchi.
Ameeleza kuwa Serikali inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2030, akitaja vyanzo kama umeme, bayogesi, haidrojeni, gesi asilia, nishati ya jua, majiko banifu na mkaa mbadala kuwa ni suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema uzinduzi huo sio tu ishara ya maendeleo ya teknolojia, bali pia ni uwekezaji katika ubunifu na uwezo wa vijana wa Kitanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni