Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na Watanzania wote kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ngazi ya Mkoa yaliyofanyika Mei 1, 2026 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo Kitaifa yamefanyikia Mkoani Njombe
Akizungumza katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu "𝙠𝙖𝙯𝙞 𝙯𝙚𝙣𝙮𝙚 𝙨𝙩𝙖𝙝𝙖 𝙣𝙞 𝙣𝙜𝙪𝙯𝙤 𝙞𝙢𝙖𝙧𝙖 𝙠𝙬𝙖 𝙢𝙖𝙚𝙣𝙙𝙚𝙡𝙚𝙤 𝙚𝙣𝙙𝙚𝙡𝙚𝙫𝙪 𝙠𝙖𝙩𝙞𝙠𝙖 𝙪𝙩𝙚𝙠𝙚𝙡𝙚𝙯𝙖𝙟𝙞 𝙬𝙖 𝘿𝙞𝙧𝙖 𝙮𝙖 2050" Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu kazini na uzalendo miongoni mwa wafanyakazi, akieleza kuwa mafanikio ya maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla yanategemea juhudi za kila mfanyakazi.
Aidha, alihimiza waajiri kuhakikisha wanaboresha mazingira ya kazi na kuwapatia wafanyakazi nyenzo stahiki ili kuongeza ufanisi na tija.
Kupitia risala ya vyama vya wafanyakazi, ilielezwa kuwa kuna umuhimu wa kuendelea kupigania ajira zenye staha kwa wote ili kuwawezesha wananchi kuishi maisha bora ikiwemo kulindwa kwa haki za wafanyakazi, kuboreshwa kwa maslahi yao pamoja na kuhakikisha mazingira salama ya kazi yanazingatiwa wakati wote.
Maadhimisho hayo yamekuwa fursa muhimu kwa wafanyakazi na waajiri kutafakari mchango wao katika maendeleo ya taasisi na Taifa, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisisitiza umuhimu wa kazi zenye staha, ulinzi wa haki za wafanyakazi na utekelezaji wa sheria za kazi kama msingi wa maendeleo endelevu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni