Ujumbe toka Tanzania wakiwa kwenge kikao cha pamoja na Wawakirishi wa Makampuni mbalimbali yanayojihusisha na utunzaji wa Mazingira |
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar wameshiriki mikutano mbalimbali yenye lengo la kuanzisha mashirikiano katika masuala mbalimbali ya Mazingira na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Akizungumza na ujumbe toka Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa nchini Qatar, Mhe. AbdulAziz Ahmad Abdullah Al-Mahmoud amesema majukumu ya kisheria ya Wizara yake ya Mazingira yanafanana na majukumu ya NEMC hivyo, kuna kila sababu ya kushirikiana hasa katika suala zima la usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Ujumbe wa Tanzania na Qatar wakibadilishana mawazo juu ya utunzaji wa Mazingira
Wengine walioshiriki katika mikutano hiyo ni Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira toka katika Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara kwa ajili ya kujifunza namna bora ya kusimamia mifumo ya maji taka kwa ajili ya kulinda mazingira na viumbe kwa ujumla. Vile vile ujumbe huo wa Tanzania uliweza kufanya mikutano na Taasisi nyingine ikiwemo Public Works Authority waliokuwa wanahusika na miundombinu na mifumo ya maji taka, Qatar General Electric and Water Cooperation wanaohusika na uzalishaji na usambazaji wa maji safi na umeme. Mikutano mingine ambayo NEMC imeshiriki ni pamoja na Qatar Foundation ambao wameonyesha utayari wa kufanya mashirikiano makubwa nchini hasa katika eneo la uhifadhi wa Ziwa Victoria hususani katika kufanya tafiti juu ya uondoshwaji wa gugu maji vamizi lililoshamiri kwa sasa linalosababishwa na ongezeko la virutubisho majini vinavyotokana na shughuli za kibinadamu
Naye Balozi wa Tanzania nchini Qatar Mhe. Habibu Awesi Mohammed amewashukuru NEMC na Mamlaka za maji toka Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara kuonesha utayari wa kujifunza na kushirikiana na Qatar katika suala zima la uhifadhi wa mazingira na usimamizi bora wa mifumo ya maji safi na taka kwa ajili ya maendeleo ya sasa na ya vizazi vijavyo