Nyumbani

NEMC YAJIPAMBANUA ELIMU YA MAZINGIRA NANENANE DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutumia Maonesho ya Kilimo ya Nanenane viwanja vya Nzuguni Dodoma, kama jukwaa muhimu la kutoa elimu ya mazingira kwa vitendo, likiwaelimisha wananchi kuhusu mbinu salama na endelevu katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.

Elimu ya mazingira inayotolewa inasisitiza matumizi ya mbinu kama kilimo hifadhi, uvuvi usioharibu makazi ya viumbe wa majini, pamoja na ufugaji usiochafua vyanzo vya maji na ardhi.

Timu ya maafisa wa NEMC wakimsikiliza mgeni aliyetembelea banda la NEMC katika maonesho ya Wakulima, nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Wa nne kushoto ni Kaimu Meneja Kanda ya Kati Bw. Novatus Mushi

“Tunafundisha wakulima kutumia mbinu za kuongeza tija bila kuharibu ardhi au kuchangia mmomonyoko wa udongo. Wafugaji pia wanapata maarifa juu ya ufugaji wa kisasa unaozingatia kanuni za kimazingira,” alisema mmoja wa maafisa walioko kwenye banda hilo.

Pamoja na elimu hiyo, NEMC inawakumbusha wananchi kuhusu wajibu wa kutekeleza Sheria ya Mazingira, ikiwa ni pamoja na kuzingatia Tathmini ya Athari kwa Mazingira kabla ya kuanzisha miradi mikubwa ya kilimo au ufugaji.

Mgeni aliyetembelea banda la NEMC akisaini kitabu cha wageni

Katika upande wa uvuvi, wananchi wanapewa maelezo kuhusu athari za uvuvi haramu na matumizi ya zana hatarishi kwa maisha ya majini, huku wakihimizwa kutumia mbinu salama zinazowezesha uvunaji endelevu wa rasilimali za maji.

Wakazi waliofika kwenye banda hilo wameonesha mwitikio chanya, wengi wakikiri kuwa elimu wanayopata imewafumbua macho kuhusu nafasi yao katika kulinda mazingira wanayoyategemea kwa maisha yao ya kila siku.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanaendelea kuvutia taasisi mbalimbali za umma na binafsi, huku kaulimbiu ikisisitiza uchaguzi wa viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi

Elimu ya Mazingira katika kilimo endelevu na rafiki kwa Mazingira inaendelea kutolewa katika maonesho ya wakulima, nanenane 2025 katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma

PROFESA MSOFE ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA NEMC

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akimkabidhi zawadi Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe mara baada ya Kikao na watumishi wa Baraza

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira)  Profesa Peter  Msofe  ameonekana kuridhishwa na utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika utekelezaji wa majukumu ya Mazingira hasa usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Nchini.

Hayo yamedhihirika wakati alipotembelea Ofisi za Baraza jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza toka kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Mazingira.

Amesema "NEMC pamoja na changomoto zote, bado mmepiga hatua katika suala Zima la usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira nchini.

Mapokezi ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe alipotembelea Ofisi za NEMC tarehe 31 Julai, 2025 Jijini Dar es Salaam

Amesema "NEMC  mnafanya kazi, watu wanaona na mnaonekana, licha ya changamoto mnazokumbana nazo, lakini endeleeni kufanya  kazi kwa ajili ya manufaa ya Taifa la Tanzania,  huku mkilinda Afya zenu dhidi ya  Mazingira hatarishi katika Utekelezaji wa majukumu yenu" amesema Prof.Msofe.

Aidha ameainisha mambo matano ambayo watumishi wa NEMC wanatakiwa  kuyazingatia katika utekelezaji wa majukumu ambayo ni kuweka uwiano kati ya vihatarishi binafsi na vihatarishi vya Mazingira ya kazi ili kuepuka madhara ya kiafya katika Utekelezaji wa majukumu, kujifunza na kushirikishana ujuzi wa utendaji kazi, ushirikiano mkubwa katika kazi na uvumbuzi katika maswala ya Mazingira ili kuweza kufanya kazi kwa kuendana na ulimwengu wa sasa

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe akizungumza katika kikao na watumishi alipotembelea Ofisi za NEMC tarehe 31 Julai, 2025. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Msofe akizungumza wakati wa Kikao na watumishi wa NEMC

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza ameesema bado NEMC inakabiliana na changamoto katika kutekeleza majukumu yake kutokana na kukosekana kwa Sheria inayotoa Mamlaka kamili ya Utekelezaji ambapo bado mchakato wa kuifanya NEMC kuwa Mamlaka unaendelea.

Amesema Baraza linatumia Vyombo vya ulinzi na usalama katika Utekelezaji wa baadhi ya majukumu kutokana na kukosekana kwa Mamlaka kamili.

Baadhi ya watumishi wa NEMC wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe wakati wa Kikao hicho

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi wakifuatilia wasilisho kuhusu kazi na majukumu mbalimbali ya NEMC lililowasilishwa na mmoja wapo wa watumishi 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Profesa Peter Msofe (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa NEMC mara baada ya Kikao na watumishi. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (NEMC) Bw. Dickson Mjinja

NEMC YASHIRIKI UZINDUZI WA MFUMO WA KIDIGITALI WA KUFUTILIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA ULIOFANYIKA MJINI ACCRA NCHINI GHANA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kufuatilia uchafuzi wa mazingira (Online Continuous Emissions Monitoring System) ambao umelenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa za uchafuzi.

Uzinduzi huo uliofanyika tarehe 29 Julai 2025 mjini Accra nchini Ghana umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi pamoja na Bi. Jackline Nyantori, Afisa Sheria Mkuu.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (katikati) akiwa na baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa mfumo huo


Washiriki wa uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kufuatilia uchafuzi wa Mazingira wakiwa katika Ukumbi ulipofanyika uzinduzi huo

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa katikati) akiwa na baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa Mfumo huo


Picha ya pamoja ya baadhi ya washiriki wa uzinduzi wa Mfumo huo 


NEMC YAPIGA MARUFUKU UCHIMBAJI WA MCHANGA MTO MPIJI KUEPUSHA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC leo 30 Julai, 2025 limepiga maarufu zoezi la Uchimbaji mchanga katika bonde la mto Mpigi unaotenganisha Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani ambalo limekuwa likiharibu Mazingira na kuhatarisha makazi ya watu wa eneo hilo kutokana na mmomonyoko wa udongo.\

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa mto huo, Meneja Uzingatiaji wa Sheria NEMC Bw. Hamadi Taimuru amesema ni marufuku wote wanaojihusisha na Uchimbaji wa mchanga katika mto huo kwa kigezo cha kusafisha mto. Amewataka kuacha mara moja uchimbaji na kuwataka wafike katika Ofisi za NEMC ili wapatiwe vibali vyenye vigezo vya kusafisha mto na si Uchimbaji wa mchanga kwa mustakabali wa utunzaji wa Mazingira.


Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamadi Taimuru akitoa maelekezo ya marufuku ya uchimbaji mchanga katika mto mpiji wakati wa ziara ya ukaguzi wa mto huo

Amesema kwa mujibu wa Sheria, ni maarufu kuchimba mchanga mita sitini ndani mtoni kwani husababisha athari kubwa kwa Mazingira na hatari kwa makazi zikiwemo kuhama kwa mto, mmomonyoko wa udongo na kusababisha mafuriko ambayo ni hatari kwa makazi ya watu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Baraza la wazee Bw. Lazaro Silla amesema kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo hawahitaji Uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo kwani unasababisha uharibifu wa Mazingira na kuhatarisha usalama wa makazi yao hivyo ameiomba NEMC kudhibiti swala hilo ili lisiendelee kuleta madhara.

Timu ya NEMC ikiwa katika ziara ya ukaguzi wa mto Mpiji

Aidha, Bw. Taimuru ameongeza kuwa marufuku hii si tu kwa mto mpiji bali ni mito yote na maeneo yote nchini ambayo wanajihusisha na uchimbaji mchanga na kusababisha uharibifu wa Mazingira na kuhatarisha makazi ya watu.

Sambamba na hayo amesisitiza wote wanaojihusisha na Uchimbaji mchanga holela kote nchini kutii agizo hilo ili kuepusha uharibifu wa Mazingira na hatari ya kuharibika kwa makazi ili kujiepusha na adhabu kali inayoweza kutolewa.

Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamadi Taimuru akitoa maelekezo ya marufuku kwa baadhi ya wachimbaji mchanga katika mto Mpiji 




NEMC NA ECCT WAHITIMISHA WANAFUNZI WA MRADI WA ECOWEAR

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC kwa kushirikiana na Taasisi ya ECCT (Environment Conservation Community of Tanzania) wamehitimisha takribani wanafunzi 22 wa Mradi wa '𝗘𝗰𝗼𝘄𝗲𝗮𝗿' waliokuwa wakipatiwa mafunzo yaliyobeba agenda ya mazingira kwenye ubunifu na Sanaa ya mitindo yenye lengo la kujenga ujasiliamali wa kijani, kupambana na taka ngumu za Sekta ya nguo na mitindo sambamba na matumizi endelevu ya rasilimali.

Mafunzo ya Mradi huo yalijikita kufundisha juu ya ubunifu wa bidhaa mbalimbali kupitia nguo zilizotumika na mabaki ya vitambaa ambapo ni  Utekelezaji wa dhana ya 𝗣𝘂𝗻𝗴𝘂𝘇𝗮, 𝗧𝘂𝗺𝗶𝗮 𝘁𝗲𝗻𝗮 𝗻𝗮 𝗥𝗲𝗷𝗲𝗹𝗲𝘇𝗮  kwa mustakabali wa utunzaji wa Mazingira na fursa za kiuchumi.

Akizungumza katika mahafali hiyo, mgeni rasmi, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi ameipongeza Taasisi ya ECCT na wahitimu wote kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuwataka kuyazingatia kwa manufaa ya kiuchumi na Mazingira.


Picha ya pamoja ya wahitimu, mgeni rasmi pamoja na viongozi wa Mradi huo mara baada ya kumalizika kwa hafla ya mahafali hayo

"Mmepata elimu, ujuzi, maarifa, mmeelewa changamoto za mazingira, sasa ni wakati wa kupeleka hayo yote kwa jamii zetu.Tuna matarajio makubwa kwenu kama mabalozi wa mitindo endelevu na watetezi wa mazingira. endeleeni kushirikiana, kushirikishana maarifa na kuamini kuwa sauti zenu na kazi zenu zinaweza kuleta mabadiliko." Alisisitiza Bi. Amina.

Bi. Amina pia ametumia fursa hii kutoa elimu kuhusu katazo la vifungashio vya plastiki kwa mujibu wa kanuni ya katazo hilo na kuwataka wahitimu wa Mradi huo kubuni na kutengeneza vifungashio vinavyoenda sambamba na mustakabali wa utunzaji wa Mazingira.

Mgeni rasmi, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akizungumza katika mahafali hayo

Baadhi ya wahitimu wa Mradi wa ECOWEAR katika mahafali hayo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa ECCT, Bi. Lucky Michael amelishukuru Baraza kwa mchango wake kufanikisha kuhitimisha wanafunzi hao huku akiainisha mafanikio ya Mradi huo ikiwa ni pamoja na kujengea uwezo wanafunzi hao ubunifu na mitindo,kukusanya takribani tani 2 za mabaki ya nguo na vitambaa kuzigeuza kuwa bidhaa zenye ubora pamoja na kuhamasisha jamii kupunguza taka na kutumia mitindo endelevu.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya ECCT Bi. Lucky Michael akizungumza katika mahafali hayo


Wahitimu wa Mradi wa ECOWEAR wakionesha baadhi ya kazi zao ambazo ni matokeo ya mafunzo ya Mradi 




NEMC YASHIRIKI MAFUNZO YA MBINU ZA KIJOGRAFIA KATIKA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA KIMAZINGIRA NA MABADILIKO YA TABIANCHI

Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki mafunzo ya muda mfupi yaliyolenga  kukuza uelewa kwa wataalamu katika umuhimu wa kutumia mbinu za Kijiografia (Geospatial Methods) kwenye uchambuzi wa taarifa za Kimazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi (Advanced GIS Training) yaliyoratibiwa na Shirika la Grumeti Fund Trust kupitia Programu ya Utafiti na Ubunifu kwa Mfumo Ikolojia wa Serengeti (Research and Innovation for the Serengeti Ecosystem-RISE).

Mafunzo haya yaliyoendeshwa kwa ushirikiano wa RISE, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Pennsylvania na Chuo Kikuu cha Montana yamefanyika ndani ya Hifadhi ya Grumeti, Magharibi mwa Serengeti kuanzia tarehe 14 hadi 20 Julai, 2025.






NEMC NA MAZINGIRA PLUS WAFANIKISHA PROGRAMU YA TAKA SIFURI KWA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA YA DAR ES SALAAM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo  25 Julai, 2025 kwa kushirikiana na Taasisi ya Mazingira Plus wamekabidhi Mradi wa Taka Sifuri kwa Shule ya Sekondari  maalumu ya wasichana ya Dar es Salaam ambapo takribani wanafunzi 200 wamehitimu na kukabidhiwa vyeti vya mafunzo ya Mradi huo.

Hafla hiyo ya kukabidhi Mradi huo iliambatana na maonesho mbalimbali ya matokeo ya mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na bustani za kioganiki zilizotengenezwa na wanafunzi, utengenezaji wa mbolea kupitia mabaki ya chakula, mabanda ya kuhifadhi na kutenganisha taka pamoja na sanaa ya vinyago vilivyoonesha namna viumbe hai wanavyoathirika na uharibifu wa Mazingira.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi Mradi huo, Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola amewapongeza wanafunzi hao kwa kuhitimu mafunzo hayo adhimu huku akiwasisitiza kuzingatia mafunzo hayo kwani yamebeba fursa za kiuchumi sambamba na Utunzaji wa Mazingira.

Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akielezea dhana ya 'Punguza, Tumia tena na Rejeleza' katika hafla hiyo 

Aidha, Bi. Amina amewasisitiza kuzingatia dhana ya punguza, tumia tena na rejeleza ambayo ni msingi wa kudhibiti uchafuzi wa Mazingira na pia ni dhana ya kuibua fursa za kiuchumi kupitia urejelezaji wa taka na uchakataji wa taka kuwa malighafi kama vile mbolea.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Taka Sifuri mashuleni Bw. Suleman Mang'uro amewataka walimu wa Shule hiyo kusimamia na kuhakikisha Mradi huo unaendelea kwa manufaa ya kiuchumi na utunzaji wa Mazingira.


Afisa wa Taasisi ya Mazingira Plus akielezea maonesho ya sanaa za vinyago vinavyoonesha namna Uchafuzi wa Mazingira unavyoathiri viumbe hai

Picha ya pamoja baada ya hafla ya kukabidhi Mradi wa Taka Sifuri 



NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...