Nyumbani

BODI MPYA YA NEMC YAKUTANA NA WATUMISHI– YAHIMIZA UWAJIBIKAJI NA USAFI WA MAZINGIRA

Bodi mpya ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imekutana kwa mara ya kwanza na watumishi wa Taasisi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uwajibikaji, mshikamano na ufanisi  katika kutimiza malengo yake ya msingi ya kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini.

Mkutano huo umefanyika kwenye kikao cha kawaida cha kila mwezi cha watumishi, ambapo Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha Tumbo, akiambatana na wajumbe wengine sita wa bodi, aliwasihi watumishi kuwa mstari wa mbele katika kuonesha mfano wa uadilifu, usafi wa mazingira, na utendaji wenye matokeo.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na watumishi hao tangu uteuzi wa bodi hiyo, Mhandisi Mwanasha alisema:

“Ili tuweze kutimiza majukumu yetu ipasavyo kama Taasisi ya mazingira, lazima tuanze na sisi wenyewe kwa kuwa wasafi, wawazi, wenye upendo na tuwe tayari kusikiliza na kushughulikia changamoto za ndani kabla ya kwenda kwa wananchi.”

Amesisitiza kuwa utunzaji wa mazingira unaanzia, majumbani kwa Watoto wadogo na kisha kusambaa kwa jamii nzima. Alisema kuwa bodi itasimamia uwazi katika maamuzi, kushirikiana kwa karibu na menejimenti pamoja na kujenga mazingira bora ya kazi kwa watumishi wote.

Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Bi. Mwanasha Tumbo (aliyesimama) akizungumza na Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Baraza mara baada ya Bodi hiyo kutembelea Ofisi za Baraza  

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, alipopata fursa ya kuzungumza aliikaribisha rasmi Bodi hiyo mpya na kueleza kuwa Menejimenti na watumishi wa NEMC wako tayari kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha taasisi inatekeleza wajibu wake kwa ufanisi.

Bodi hiyo mpya ya Wakurugenzi ya NEMC inatarajiwa kuleta mwelekeo mpya wa kimkakati katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na usimamizi wa taka.



Matukio katika Picha: Bodi ya NEMC, Menejimenti ya NEMC na baadhi ya Watumishi wa NEMC wakiwa katika Kikao mara baada ya Bodi kutembelea Ofisi za Baraza Jijini Dar es Salaam.

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

NEMC YAKOMESHA UENDESHAJI HOLELA WA KIWANDA MTAA WA REGENT ESTATE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekichukulia hatua za kisheria kiwanda bubu cha SUMING kilichopo Mtaa wa Regent Estate katika Kata ya Mikocheni wilayani Kinondoni kinachofanya shughuli za  urejelezaji wa taka hatarishi aina ya simu za   kiganjani chakavu katika eneo la makazi ya watu bila kibali cha kukusanya, kurejeleza, kuhifadhi na kusafirisha taka hizo jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Zoezi hilo limefanyika mara baada ya timu ya wataalamu wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent kukagua kiwanda hicho na kubaini mapungufu yanayokiuka Sheria ya Usimamizi wa Mazingira nchini.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi huo Meneja Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bi. Glory Kombe amesema ni kosa kisheria kuanzisha kiwanda bila kusajili na kufuata taratibu za kimazingira ikiwepo kuzingatia ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kupata vibali vya kukusanya na kurejeleza taka za kielectroniki. Ameutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kufika mara moja Ofisi za NEMC ili waweze kupata taratibu zinazotakiwa kufuata wakati wa kuanzisha Mradi ili kuepuka madhara ya kimazingira na Afya ya viumbe hai.

Maafisa wa NEMC wakitoa maelezo kwa mmoja wa wamiliki wa Kiwanda hicho

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule ameishukuru NEMC kwa kubaini na kukichukulia hatua Kiwanda hicho na amezitaka Taasisi zote zilizoshiriki ukaguzi wa Kiwanda hicho kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria na miongozo ya Taasisi husika.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka Mazingira rafiki yanayovutia uwekezaji nchini hivyo wawekezaji watumie Mazingira hayo vizuri kwa kufuata utaratibu na Sheria ili kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama, kuepusha uharibifu wa Mazingira na upotevu wa mapato ya Serikali.

Baraza linaendelea kutoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaoanzisha Viwanda bila kufuata taratibu (Viwanda bubu) ili kuepusha uharibifu wa Mazingira na kulinda Afya ya mazingira na viumbe hai.

Timu ya maafisa wa NEMC, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, TRA,  pamoja na maafisa wa Serikali ya mtaa wa Regent wakijadiliana mara baada ya Ukaguzi wa Kiwanda hicho

NEMC YASHIRIKI UKAGUZI WA BWAWA LA TOPESUMU ZAMBIA

Wataalam wa miamba na madini kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Bw. Abel Sembeka na Bi. Edika Masisi, wameshiriki katika warsha na ukaguzi wa bwawa la topesumu lililopasuka Februari 15, 2025 kwenye mgodi wa kampuni ya Sino Metal Leach Zambia Limited nchini Zambia.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Jiolojia ya Sweden (SGU) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Lulea kutoka nchini Sweden na Chuo Kikuu cha Copperbelt cha nchini Zambia, huku Wizara ya Madini na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira nchini Zambia (ZEMA) wakiwa wenyeji.

Warsha hiyo umehusisha pia wataalam wa migodi na mazingira kutoka nchi za Afrika Magharibi, Mashariki na Kusini mwa Afrika waliopata mafunzo ya usimamizi wa miamba taka na maji migodini kupitia mradi wa ITP 308 chini ya uratibu wa SGU.

Lengo kuu la warsha hiyo ni kutembelea na kufanya tathmini ya bwawa la topesumu lililopasuka, kujifunza chanzo cha tatizo, mbinu bora za usanifu na usimamizi wa mabwawa ya topesumu, pamoja na hatua za kupunguza madhara kwa mazingira na jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.






NEMC YASHIRIKI WARSHA YA KUJADILI UREJESHWAJI IKOLOJIA YA MATUMBAWE

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Warsha ya kujadili namna bora ya urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya matumbawe iliyofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 16-17 Septemba 2025. 

NEMC imewakilishwa na Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC), Dkt. Rose Sallema Mtui, ambaye pia ni Mratibu wa Kikosi kazi cha Taifa cha kuhifadhi na kutunza matumbawe. 

Kikao hicho kimeratibiwa na shirika la Uhifadhi Mazingira la “The Nature Conservancy”

Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema akiwasilisha mada katika Warsha hiyo

Baadhi ya washiriki wa Warsha hiyo wakifuatilia mada zilizowasilishwa katika Warsha hiyo




Baadhi ya wawasilishaji wakiwasilisha mada katika Warsha hiyo


Washiriki wa Warsha ya kujadili namna bora ya urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya matumbawe wakiwa katika picha ya pamoja, Warsha hiyo imefanyika Zanzibar kuanzia tarehe 16-17 Septemba 2025. 

NEMC YASHIRIKI WASILISHO LA RIPOTI YA MAKUNDI MAALUM KUTOKA KWA ASASI YA WATED JIJINI DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limeshiriki uwasilishaji wa ripoti ya mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni kwenye sera ya Taifa ya Ardhi 1995 (Toleo la 2023) na mchakato wa NDC 3.0V  uliofanyika katika ukumbi wa Residence Jijini Dodoma leo.

Akiwasilisha ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na WAHEAL na  Tree of Hope, Mkurugenzi wa Asasi ya Kiraia kutoka Women Action Towards Entrepreneurship Development (WATED) Bi. Maria Matui amesema imelenga kuainisha changamoto za wanawake wa vijijini pamoja na kusaidia jitihada za mashirika katika kupaza sauti za wanawake kwenye masuala ya usimamizi wa ardhi na harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Walioshiriki katika uwasilishaji wa ripoti Asasi ya WATED ya mchango wa wanawake, wasichana na makundi wakiwa katika picha ya pamoja .

 
Amesema wasilisho hilo lililohusisha pia wanachama wa mtandao wa mabadiliko ya tabianchi limeainisha changamoto nyingi wanazopitia wanawake wa vijijini zikiwemo, mila na desturi, mitazamo na mifumo dume hali inayoathiri masuala ya maendeleo hasa shughuli za uzalishaji.
Baadhi ya washiriki wa wasilisho la Asasi ya WATED wakiwa 
 katika ukumbi wa Residence leo Septemba 17, 2025  Dodoma 

Malengo makubwa matatu yaliyowasilishwa ni pamoja na kuweka wazi mchango wa wanawake, wasichana na makundi yaliyo pembezoni katika utekelezaji wa Sera ya Ardhi ya 1995(Toleo la 2023, kushirikiana na Serikali katika kuboresha mchakato wa NDC.3.0V kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na haki za makundi yote ya jamii pamoja na kutoa mapendekezo Sera shirikishi yatakayohakikisha usimamizi endelevi wa rasilimali na upatikanaji wa haki sawa kwa kila mmoja.

Baadhi ya washiriki wa wasilisho la Asasi ya WATED wakifuatilia wasilisho hilo lililofanyika  katika ukumbi wa Residence leo Septemba 17, 2025  Dodoma 

Mikoa iliyofikiwa na Asas hizi ni pamoja na Ruvuma, Morogoro, Kilimanjaro, Geita, Arusha, Mara, Kagera na Tanga.

NEMC NA TAASISI MBALIMBALI WAADHIMISHA SIKU YA MIKOKO DUNIANI KWA KUPANDA MICHE 1000

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Taasisi za umma na binafsi waadhimisha siku ya mikoko duniani kwa kupanda miche takribani 1,000 ya miti ya  Mikoko eneo la Kilongawima lililopo pembezoni mwa fukwe ya 'Mbezi beach'  Halmashauri  ya Kinondoni Manispaa ya Jijini Dar es.

Akizungumza mara baada ya zoezi la upandaji wa miche hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amewataka wananchi kulinda na kithamini mikoko kwani Inamanufaa mkubwa katika kulinda ikolojoa ya bahari na viumbe hai waishio majini. 

Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema akiwa ameshika mche wa Mkoko tayari kwa kuupanda katika zoezi la upandaji Mikoko eneo la Kilongawima

Naye Dkt.Rose Sallema, Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) alipozungumza alisema mikoko ni rasilimali ya bahari inayotakiwa kutunzwa kwani inafaida kiuchumi,kijamii na kimazingira.

Viongozi na wadau wa Mazingira wakitazama hati miliki ya TFS kuashiria ulinzi wa eneo la Kilongawima lililopandwa takribani miti ya Mikoko 1,000

Naye Mkurugenzi Msaidizi, Maendeleo ya Misitu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ndugu. Seleboni Mushi alipozungumza aliitaka  jamii kuzingatia Uhifadhi wa misitu ya Mikoko kwani husaidia kuhifadhi fukwe na hewa ukaa hivyo kusaidia kuhimili mabadiliko ya tabianchi.

Afisa Mazingira Mkuu Bi. Ritha Said akipanda mche wa Mkoko wakati wa zoezi la upandaji Mikoko eneo la Kilongawima 

Ameongeza kuwa ni Hifadhi ya viumbe hai na husaidia jamii hasa za Pwani katika kujipatia kipato.

Taasisi zilizoshiriki Maadhimisho hayo ni pamoja na TFS, WWF, IUCN, Wetland, Mwambao International Wawakilishi kutoka maeneo ya Pwani ya Kibiti, Kilwa na Mafia.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ndugu. Saad Mtambule akizungumza na washiriki wote waliopanda miche ya Mikoko katika eneo la Kilongawimakatika kuadhimisha Siku ya Mikoko duniani


Zoezi la upandaji miti katika eneo la kilongawima likifanyika ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mikoko Duniani inayoadhimishwa tarehe 26 Julai kila mwaka ambapo kwa Tanzania imeadhimishwa tarehe 4 kwa kupanda Mikoko.

NEMC INAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WANAFUNZI NA WANANCHI KATIKA MAONESHO YA NANENANE JIJI MBEYA

Elimu ya Utunzaji wa Mazingira ikiendelea kutolewa kwa wananchi na wanafunzi wa Sekondari ya Lyoto waliotembelea Banda la NEMC lililopo katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.





NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...