Nyumbani

NEMC YAADHIMISHA SIKU YA AFYA MAZINGIRA DUNIANI, ELIMU YA MAZINGIRA YATOLEWA SHULENI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuadhimisha Siku ya Afya mazingira Duniani, Leo tarehe 26 Septemba limetembelea  Shule ya Msingi Mikocheni "A" na kutoa elimu ya Afya na Mazingira kwa wanafunzi na walimu ambapo kaulimbiu kwa mwaka huu 2025 ni "Tokomeza taka za plastiki, Jenga jamii yenye afya Bora.

Elimu hiyo imejikita katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira shuleni, pamoja na kuelezea Dhana ya Punguza, Tumia tena na Rejeleza katika Udhibiti wa taka ikiwa ni pamoja na kufundisha kuhusu usafi wa mwili na mazingira ya nyumbani. 

Afisa Mazingira wa NEMC Bi. Rukia Ally akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni "A" katika Maadhimisho ya Siku ya Afya Mazingira Duniani tarehe 26, Septemba.

Wanafunzi walishirikiana kwa kuuliza maswali na kujifunza mbinu rahisi za kuhakikisha mazingira yao yanabaki safi na salama kwa wote.

Aidha, maafisa hao walitoa wito kwa jamii nzima kushirikiana katika kuendeleza jitihada za kulinda mazingira, kwani afya njema haiwezi kupatikana endapo mazingira yanaharibika. Waliwataka wazazi, walimu na viongozi wa jamii kuhakikisha elimu hiyo inapelekwa hadi majumbani na maeneo ya kazi, ili kila mmoja awe balozi wa mazingira bora.

Hivyo basi, maadhimisho ya Siku hii yamekuwa chachu ya kuimarisha mshikamano wa pamoja katika kuyalinda mazingira kwa mustakabali endelevu wa kizazi cha sasa na kijacho.

Maafisa wa NEMC wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni A mara baada ya kutoa elimu ya Mazingira kwa wanafunzi wa Shule hiyo ikiwa ni sehemu ya Kuadhimisha Siku ya Afya Mazingira Duniani

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikocheni A wakifuatilia Elimu iliyotolewa na Maafisa Mazingira kutoka NEMC katika Maadhimisho ya Siku ya Afya Mazingira Duniani

PICHA ZA MATUKIO KATIKA KONGAMANO LA UNESCO LA PROGRAMU YA BINADAMU NA HIFADHI HAI CHINA


NEMC na TANAPA katika Kikao cha Kimataifa cha Kamati ya Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai kinachofanyika jijini Hangzhou nchini China kuanzia tarehe 26-28 Septemba 2025. Pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Dkt. Immaculate Sware Semesi (Kulia) na Meneja wa Tafiti za Mazingira, Dkt. Rose Sallema na Mr. Albert Mziray Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kutoka TANAPA
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kushoto) katika Ukumbi wa Kongamano hilo, kushoto kwake ni Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema pamoja na washiriki wengine wa Kongamano hilo lililofanyika Nchini China
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo mara baada ya majadiliano kuhusu uwezekano wa kupata Fursa za Miradi kwenye Hifadhi Hai katika Kongamano la Dunia la Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai lililofanyika jijini Hangzhou nchini China. Kulia kwake ni Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA KIKANDA NCHINI UGANDA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Warsha ya Kikanda Jijini Kampala (EAC) inayohusu masuala ya upangaji wa maeneo ya ufugaji samaki katika ziwa Victoria.

Akiripoti kutokea Kampala Meneja kutoka NEMC Bw.Jarome Kayombo amesema warsa hiyo imelenga kuainisha vigezo vitalavyotumika kwa nchi zote tatu katika kupanga maeneo ya ufugaji, kutenga maeneo, kusimamia mazingira na usalama w Samaki.

Wajumbe walioshiriki kutoka Tanzania ni pamoja na Wizara ya Mifugo, NEMC, Bonde ziwa Victoria, Jumuia ya wafugaji Samaki, Umoja wa wavuvi, Vyuo vikuu pamoja na Tafiri.

Ujumbe ulioambatana na timu hiyo katika warsha umehusisha Uganda, Kenya, Tanzania, Burundi na Rwanda.

Meneja kutoka NEMC Bw. Jarome Kayombo (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Warsha ya Kikanda Jijini Kampala (EAC) inayohusu masuala ya upangaji wa maeneo ya ufugaji samaki katika ziwa Victoria.

NEMC YATEMBELEA KIWANDA NCHINI NORWAY KUJIFUNZA UZALISHAJI SARUJI ISIYOZALISHA HEWA UKAA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati, PURA na TANESCO, wametembelea Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway, kinachoendeshwa na kampuni ya Norcem chini ya Heidelberg Materials, ambacho ni kiwanda cha kwanza duniani cha saruji kuendesha kituo kamili cha kunasa na kuhifadhi hewa ya ukaa (CCS). Sekta ya saruji ni ngumu kupunguza hewa ya ukaa kwa sababu malighafi yake kuu (chokaa), huzalisha kaboni dioksaidi wakati wa mchakato.

Baadhi ya Wataalamu wa Mazingira wa NEMC na Wataalamu wa Kiwanda cha Saruji cha Brevik kilichopo nchini Norway wakiwa katika picha ya pamoja 

Kiwanda hiki kinatumia teknolojia ya kunasa dioksidi kaboni kwa njia ya amini (amine absorption) ambapo gesi ya ukaa hutenganishwa kutoka kwenye moshi wa mitambo, kisha hubanwa (compressed) na kubadilishwa kuwa kimiminika ili kusafirishwa. Ukaa ulionaswa unasafirishwa kupitia mtandao wa hifadhi wa Northern Lights. Baada ya kubadilishwa kuwa kimiminika, husafirishwa kwa meli hadi kituo cha nchi kavu kisha huingizwa kwenye tabaka za miamba ya ardhini chini ya Bahari ya Kaskazini. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa Longship wa Norway unaolenga kusaidia viwanda kupunguza hewa chafu ili kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Mradi huu wenye thamani ya takriban Euro milioni 400 unategemea ushirikiano wa karibu na msaada mkubwa wa kifedha wa serikali (takriban 75%) kutokana na gharama zake kubwa za kiufundi. Pia mradi huu umewezesha kutengenezwa kwa bidhaa mpya za saruji zenye alama ya “evoZero”, zinazouzwa kama saruji yenye uzalishaji usio na hewa ya ukaa kwa sababu ukaa wake unanaswa na kuhifadhiwa. Mafunzo na uzoefu unaopatikana hapa yanatarajiwa kusaidia katika utekelezaji wa miradi mingine ya CCS Duniani kote.

Kwa ujumla, kituo cha CCS cha Brevik kinaonyesha kuwa inawezekana kupunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa hewa ya ukaa katika sekta ya saruji. Ingawa bado kuna changamoto za gharama na matumizi makubwa ya nishati, mradi huu ni hatua kubwa ya kihistoria katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na ni mfano bora kwa viwanda vingine vizito vinavyolenga kufikia uzalishaji sifuri wa hewa ya ukaa.

WAHANDISI WA NEMC WASHIRIKI MAADHIMISHO YA 22 YA SIKU YA WAHANDISI NCHINI (22ND AED 2025)

Wahandisi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wanashiriki Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi nchini (AED 2025) yanayofanyika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 - 26 Septemba, 2025 chini ya kauli mbiu isemayo "Kufanikisha Dira ya 2025 na Kusonga Mbele kuelekea Dira ya 2050: Nafasi ya Wahandisi."

Tukio hili limewaleta pamoja wahandisi zaidi ya 4,000, watunga sera, na wadau mbalimbali kujadili masuala muhimu ikiwemo maadili katika uhandisi, mabadiliko ya kidijitali, miundombinu ya kijani, nishati, maji, kilimo, ushindani wa viwanda, na maendeleo endelevu.

Kupitia ushiriki huu, wahandisi wa NEMC wanaendelea kuimarisha nafasi yao katika kuunganisha ubunifu wa uhandisi na uwajibikaji katika kusimamia uhifadhi wa mazingira ili kuhakikisha kwamba safari ya Tanzania kuelekea Dira ya 2050 inabaki endelevu, jumuishi, na yenye ustahimilivu.


Wahandisi wa Mazingira (NEMC) wakiwa katika picha ya pamoja nje ya Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam  wakati wa Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi nchini 

NEMC YASHIRIKI KONGAMANO LA UNESCO LA PROGRAMU YA BINADAMU NA HIFADHI HAI CHINA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Kongamano la Dunia la Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai lililofanyika Jijini Hangzhou nchini China kuanzia tarehe 22-25 Septemba 2025.

Kwa upande wa NEMC Kongamano hilo limehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi pamoja na Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema.

Wawakilishi wengine kutoka Tanzania katika kongamano hilo ni kutoka TANAPA

Kongamano hilo limelenga Kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa, kupata maarifa na teknolojia mpya katika kusimamia na kuhifadhi Mazingira nchini, ni fursa katika uendelevu wa Hifadhi za Taifa, fursa za Kutangaza vivutio vya kitalii, kuimarisha Ushirikiano na Jamii, kuitangaza Tanzania kimataifa, kuvutia wawekezaji na kusaidia kufikia malengo ya Maendeleo nchini.


Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kushoto) katika Ukumbi wa Kongamano hilo, kushoto kwake ni Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema pamoja na washiriki wengine wa Kongamano hilo lililofanyika Nchini China

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Tafiti za Mazingira(NEMC) Dkt. Rose Sallema na mshiriki mwingine wa Kongamano hilo

Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema (wa katikati) na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.


NEMC NA TANAPA WAADHIMISHA SIKU YA FARU DUNIANI KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI- KILIMANJARO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na TANAPA wameadhimisha Siku ya Faru Duniani ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Same mkoani Kilimanjaro Septemba 22,2025.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Afisa Mazingira Mwandamizi Bw. Francis Nyamhanga amezungumzia kuhusu umuhimu wa Faru kwenye mfumo wa Ikolojia.

"Kwenye mfumo wa Ikolojia Faru husaidia kufungua njia kwa kuvunja miti kwa ajili ya Wanyama wengine wadogo kuweza kupata malisho lakini pia hula mbegu za mimea mbalimbali hivyo kupitia kinyesi chao husaidia kusambaza mbegu katika mifumo Ikolojia na kinyesi hicho pia hurutubisha mifumo ikolojia bila kusahau wanachangia kukuza pato la Taifa kwani Faru ni kivutio cha utalii" amesema Bw. Francis.

 Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo na Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Bw. Francis Nyamhanga wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomanzi Mkoani Kilimanjaro katika Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani

Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo ameeleza namna wanavyowafikia Jamii kwa kutoa elimu ya Uhifadhi wa Faru.

"Hifadhi Ina programu maalumu inayofahamika kama Rafiki wa Faru ambayo inafikia Jamii kwa kuipa elimu ya jinsi ya Faru hawa walivyotoweka, walivyorejeshwa na jinsi wanavyolindwa na kuzalishwa katika Hifadhi hii. Hadi sasa tumefikia shule 120 na kuwafikia walimu na wanafunzi takribani 3,600 toka Julai 2022" amesema Mhifadhi Lyimo.

Katika kuadhimisha Siku hii pia wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamefika katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kujifunza namna Uhifadhi wa Faru unavyofanyika. Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani hufanyika mnamo Septemba 22 kila mwaka kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusiana na Uhifadhi wa Faru na kuwalinda dhidi ya ujangili.






NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...