Nyumbani

NEMC KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO KWA WAKANDARASI WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Katika kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Ofisi ya Kanda ya Kati, leo tarehe 10 Oktoba, 2025, limetoa mafunzo kwa wakandarasi wa ujenzi waliosajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya CRB, jengo la Mkandarasi House jijini Dodoma, yalilenga kuwaongezea wakandarasi uelewa kuhusu taratibu za Usimamizi wa Mazingira na umuhimu wa kutumia mifumo endelevu katika miradi ya ujenzi, ikiwemo udhibiti wa taka ngumu, taka maji na taka hatarishi.    

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Bw. Novatus Mushi, alisisitiza umuhimu wa wakandarasi kuzingatia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kufuata viwango vya ujenzi vinavyokidhi changamoto za kimazingira, hususan mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kuathiri miundombinu.

Kaimu Meneja wa Kanda ya Kati (NEMC) Bw. Novatus Mushi akitoa elimu kwa Wakandarasi wa ujenzi katika mafunzo hayo

    Baadhi ya wakandarasi wakifuatilia mafunzo hayo

NEMC KANDA YA BAGAMOYO YATOA ELIMU YA MAZINGIRA SHULE YA MSINGI NIA NJEMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia ofisi yake ya Kanda ya Bagamoyo, limetoa elimu ya mazingira kwa Shule ya Msingi Nia Njema, tarehe 9 Oktoba 2025. 

Elimu hiyo iliyotolewa kwa walimu na wanafunzi imelenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Meneja wa Kanda ya Bagamoyo Bi. Ndimbumi Joram (wa pili kushoto) akitoa elimu ya Mazingira kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nia njema, kulia kwake ni Mhandisi wa Mazingira (NEMC) Bw. Jerusalem Bagaza 

Katika mafunzo hayo, Meneja wa Kanda ya Bagamoyo, Bi. Ndimbumi Joram, amewahimiza wanafunzi kuwa mabalozi wa mazingira bora kwa kuhakikisha usafi wa mazingira ya shule na majumbani mwao. Amesisitiza kuwa jukumu la kulinda mazingira sio la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja, hasa watoto ambao ni viongozi wa kesho.

Aidha, Bi. Ndimbumi amezungumzia athari za utupaji hovyo wa taka ngumu na matumizi ya mifuko ya plastiki, akieleza kuwa plastiki ni moja ya changamoto kubwa inayoathiri mazingira duniani.

 Amehimiza matumizi ya mifuko mbadala inayoweza kutumika mara nyingi kama njia mojawapo ya kupunguza taka za plastiki na kulinda afya ya mazingira.

Menejeja wa Kanda ya Bagamoyo Bi. Ndimbumi Joram akigawa zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingingi Nia njema mara baada ya kutoa elimu ya Mazingira katika shule hiyo

Kwa kutambua juhudi za wanafunzi na walimu katika kushiriki kikamilifu mafunzo hayo, Meneja huyo ametoa zawadi za mifuko mbadala kama motisha na mfano wa vitendo vya ulinzi wa mazingira.

Shule ya Msingi Nia Njema imeahidi kuendeleza elimu hiyo kwa vitendo kwa kuanzisha klabu ya mazingira itakayosaidia kutunza mazingira ya shule na jamii kwa ujumla.




NEMC NA WIOMSA WAENDESHA KONGAMANO LA WADAU WA BAHARI NCHINI KENYA

Timu ya wataalam wa Sayansi ya bahari kutoka Tanzania ikiongozwa na  Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambaye ni mratibu wa WIOMSA wameshiriki kongamano la wadau wa masuala ya bahari lililohusisha Watunga sera, wanasayansi ya bahari, wanasheria, wahandisi wa Mazingira, wanauchumi, wafanyabiashara, watafiti, wanavyuo na wazawa wanajamii ya pwani ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Wanasayansi ya bahari magharibi mwa Bahari ya Hindi kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika masuala ya Uhifadhi wa bahari ya Hindi.

Kongamano hilo la kumi na tatu (13 WIOMSA scientific symposium) limefanyika kuanzia tarehe 27 Septemba mpaka 3 Oktoba 2025 Mombasa nchini Kenya.

Timu ya NEMC ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi na timu ya WIOMSA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya awamu ya kwanza ya Kongamano hilo

Ushiriki wa Baraza kwenye kongamano hilo kumesaidia kuongeza  uelewa au kukuza taaluma ya Sayansi ya Bahari kwa wataalam wa bahari katika nyanja za Uhifadhi wa Mazingira, kupata fursa  za kukutana na wadau wanaotoa fedha za kusaidia miradi au tafiti za Mazingira ya Bahari na Bioanuai zake pamoja na kupata taasisi na mashirika mbalimbali ya kushirikiana katika tafiti na miradi ya Uhifadhi wa Mazingira ya Bahari.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akiwasilisha mada katika Kongamano hilo

Aidha ushiriki huo pia utasaidia kuanzisha na kuimarisha mashirikiano kati ya Maafisa/Wanasayansi ya Bahari katika nchi za ukanda wa Magharibi ya Bahari ya Hindi, kutambua fursa za uwekezaji katika tafiti, teknolojia, biashara na uwekezaji katika sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na  kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi wanachama wa WIOMSA.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa WIOMSA Dkt.Arthur Tude na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo

Mawasilisho na majadiliano ya mada katika Kongamano hilo
Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini (NEMC) Bi. Glory Kombe akichangia mada wakati wa Kongamano hilo


Picha mbalimbali za washiriki wa Kongamano hilo zikijumuisha watumishi wa NEMC na wa WIOMSA 

NEMC NA ZEMA ZAKUBALIANA KATIKA USIMAMIZI NA UHIFADHI WA MAZINGIRA NCHINI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) wameimarisha ushirikiano wao kuingia  makubaliano ya pamoja ya usimamizi na uhifadhi wa mazingira nchini. 

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao cha siku mbili kilichofanyika kuanzia tarehe 7 hadi 8 Oktoba 2025, ambapo wajumbe wa Bodi na wataalamu kutoka taasisi zote mbili walikutana kujadiliana na kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati wa kikao hicho

Kupitia kikao hicho, taasisi hizo zimeweka msingi wa ushirikiano madhubuti katika maeneo mbalimbali, yakiwemo matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika usimamizi wa mazingira, ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria na Kanuni za mazingira, pamoja na kuimarisha mawasiliano ya mara kwa mara kati ya pande hizo mbili.

Aidha  wamekubaliana pia kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar inazingatia mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA).

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa Kikao hichoMwenyekiti wa Bodi ya ZEMA Bi. Asha Ali Khatib akizungumza wakati wa Kikao hicho

Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya NEMC na ZEMA wakifuatilia kikao hicho

Akizungumza na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2020/2050, ambayo inaweka mazingira kama mojawapo ya nguzo kuu za maendeleo ya Taifa.

 Amesisitiza kuwa mashirikiano hayo yataongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusaidia kufanikisha malengo ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira kwa maslahi ya wananchi na vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ZEMA, Bi. Asha Ali Khatib, amesema kikao hicho kimetoa fursa kwa wataalamu wa pande zote mbili kujifunza kutoka kwa wenzao, na pia kuibua mbinu mpya za kuboresha utendaji.

Ameongeza kuwa ushirikiano huu utawezesha uwiano wa kisera na kiutekelezaji katika masuala ya mazingira baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Picha ya pamoja ya Menejimenti ya NEMC na ZEMA mara baada ya Kikao hicho. Wa nne kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi ya ZEMA Bi. Asha Ali Khatib, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa ZEMA Sheha Mjaja Juma


NEMC NA ZEMA ZAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo Oktoba 7,2025 limepokea ugeni wa Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) na kufanya kikao Cha kujengeana uwezo ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za kuimarisha ushirikiano katika kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini

Akifafanua lengo la kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema kimejikita katika kujadiliana mikakati, kutoa ushauri na kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za mazingira kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo na kuongeza tija katika sekta ya mazingira.

Pichani ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (Kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa ZEMA Bw. Sheha Mjaja Juma mara baada ya kikao cha kujengeana uwezo kati ya Taasisi hizo mbili

Viongozi hao pia wamejadili utekelezaji wa taratibu walizojiwekea katika kufuatilia na kusimamia Sheria za mazingira ili kuhakikisha rasilimali asilia zinatunzwa ipasavyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZEMA, Bw. Sheha Mjaja Juma amesisitiza umuhimu wa wananchi kutimiza wajibu wao kwa kufuata Sheria na taratibu za mazingira, sambamba na Taasisi za maendeleo kuhakikisha miradi yao inazingatia usimamizi endelevu wa mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Itakumbukwa kuwa NEMC na ZEMA wamekuwa na mashirikiano ya muda mrefu na mara kadhaa wamekuwa wakitembeleana na kupeana uzoefu kwa maslahi mapana ya Mazingira nchini Tanzania.

Baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya NEMC na ZEMA wakifuatilia kikao hicho
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya Kikao hicho
Mkurugenzi Mkuu wa ZEMA Bw. Sheha Mjaja Juma  akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya Kikao hicho



NEMC YAADHIMISHA WIKI YA HUDUMA KWA MTEJA KWA VITENDO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa mteja yenye kaulimbiu " Mission Possible" limeweka banda maalum katika ofisi zake ili kurahisisha  huduma kwa wateja wake moja kwa moja. 

Banda hilo limelenga kuboresha mawasiliano na kujenga mahusiano bora yenye kutoa fursa kwa wadau  kutoa maoni, changamoto, pamoja na kupatiwa majibu ya papo kwa papo kuhusu huduma za mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi akiwa katika banda maalum la kuhudumia wateja lililopo Ofisi za NEMC katika msimu wa Wiki ya Huduma kwa Mteja inayoadhimishwa kuanzia tarehe 6 hadi 10 Oktoba, 2025  

Wateja waliofika Ofisi za NEMC wakipatiwa huduma katika Wiki ya Huduma kwa Mteja 
Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (NEMC) Bw. Dickson Mjinja akifuatilia utoaji wa huduma kwa wateja waliofika katika banda maalum la NEMC katika Maadhimisho ya Wiki ya huduma kwa Mteja 

Katika hatua nyingine Baraza Kupitia Kanda zake 13  limeendelea kutoa elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa wanachi

Ikiwa ni pamoja na kufanya ziara za ukaguzi (site visits) kwa wadau wake kujiridhisha na utekelezaji wa Kanuni za mazingira na kushughulikia changamoto zinazoibuliwa na wananchi


WATAALAM ELEKEZI WA MAZINGIRA KANDA YA MAGHARIBI (NEMC) WAPATIWA MAFUNZO YA TATHMINI YA ATHARI KWA MAZINGIRA

 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia kurugenzi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii imetoa mafunzo ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa wataalamu elekezi wa mazingira na watumishi wa Baraza waliopo Kanda ya Magharibi inayohusisha mikoa mitatu (Kigoma, Katavi na Tabora) kuanzia tarehe 1-3 Oktoba, 2025.

Mafunzo haya ni endelevu na lengo kuu ni kuboresha ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) na upitiaji wa taarifa za TAM zinazowasilishwa Baraza.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...