NEMC YASHIRIKI KIKAO KAZI CHA KUPITIA MPANGO WA KITAIFA WA KUPAMBANA NA UKAME
NEMC YACHOTA HAZINA KUBWA YA NAMNA YA KUHIFADHI NA KUSIMAMIA MAZINGIRA KUTOKA KWA DKT. MPANGO
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Novemba 11, 2025 limefanya ziara maalum nyumbani kwa Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, eneo la Mayamaya mkoani Dodoma, ambapo mazungumzo yenye tija kubwa kuhusu hali ya mazingira nchini yamefanyika.
Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mpango ameelezea kwa kina wasiwasi wake kuhusu kasi ya uharibifu wa mazingira unaoendelea kushamiri nchini, huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa msukumo mkubwa zaidi katika kulinda maeneo ya hifadhi na kusimamia matumizi bora ya ardhi.
Amesema kuwa maeneo mengi ya hifadhi yamekuwa yakivamiwa, mito mingi imechepushwa kinyume na taratibu, huku mabwawa ya kuzalisha umeme yakikumbwa na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu. Vilevile, biashara ya mbao na mkaa imeendelea kuchangia ongezeko la ukataji miti na hivyo kuongeza kasi ya uharibifu wa misitu nchini.
Dkt. Mpango amebainisha kuwa changamoto za mifugo isiyo na utaratibu mzuri, uchimbaji holela wa mashamba, pamoja na tatizo la mimea vamizi, vinahitaji mikakati madhubuti ya kitaifa. Amesisitiza kuwa NEMC inapaswa kupewa nguvu zaidi katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni za mazingira, akisema: “Sauti ya NEMC isiwe tena sauti ya mtu aliye nyikani.”
“Ni lazima tujiulize kama Taifa, kama miji, tumechukua hatua gani za kulinda na kurejesha uoto wa asili? Inawezekana kabisa kuwa na mazingira mazuri kama tukidhibiti shughuli zetu kwa kufuata sheria na mipango tuliyojiwekea,” amesisitiza Dkt. Mpango.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza alipongeza maono na ushauri uliotolewa Dkt. Mpango, huku akiahidi kuendelea kutumia maarifa hayo katika kuimarisha juhudi za Hifadhi na Usimamizi endelevu wa mazingira nchini.
Ziara hiyo iliyofanywa na Menejimenti ya Baraza imekuwa ni ya muhimu katika kujenga mashirikiano kati ya Taasisi za Serikali na viongozi wastaafu wenye uzoefu mkubwa, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye mazingira safi, salama, na yenye uendelevu wa kiikolojia.
Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, wakati Uongozi wa NEMC ulipomtembelea nyumbani kwake mjini Dodoma
NEMC YAJINASIBU KUFANYA MAKUBWA SHIMMUTA 2025, YAPOKEA VIFAA KUTOKA MRADI WA ADAPTATION FUND
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limejipanga kisawasawa kushiriki mashindano ya michezo yanayoratibiwa na Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) ambapo tarehe 28 Oktoba, 2025 limezindua rasmi vifaa vilivyofadhiliwa na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation fund) vitakavyotumika na wanamichezo katika mashindano hayo.
Akizungumza wakati kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema michezo ni muhimu kwa Afya ya binadamu kwani hupelekea uwezo wa kufanya kazi vizuri huku akisisitiza usimamizi na uhifadhi wa Mazingira nchini
Ameongeza kuwa ushiriki wa NEMC katika michezo hiyo ni fursa muhimu ya kuifikia jamii, kuimarisha ushirikiano baina ya watumishi wa Umma na Sekta binafsi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo - NEMC Bw. Fortinatus Patrick amesema timu za NEMC ziko tayari kwenda kupambana katika michezo yote na wamejiandaa kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (NEMC) Bw. Dickson Mjinja ambaye ni mlezi qa timu hiyo, alipozungumza amesema NEMC imejipanga kisawasawa kuwa washindani na si washiriki katika michezo yote iliyo jisajili.
NEMC kwa kushirikiana na Mradi wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi umefanikisha Mandalizi hayo ya SHIMMUTA 2025 yanayotarajiwa kuafanyika jijini Mwanza November 13 - 29, 2025 huku ikilenga kuelimisha umma wa watanzania kuhusu mazingira na masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi
NEMC KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YAENDESHA MAFUNZO YA UHIFADHI NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA, NJOMBE
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia ofisi yake ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wametoa Mafunzo ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa Viongozi na Kamati za Mazingira za Wanawake na Samia katika Mkoa wa Njombe.
Mafunzo hayo yamelenga kupata Wadau na Mabalozi wazuri watakao saidia kusimamia, kutunza na kuelimisha wananchi na jamii kwa ujumla maswala ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira katika Mkoa wa Njombe
Elimu iliyotolewa ni pamoja na Umuhimu wa kutunza Mazingira na faida zake, Umuhimu wa Kutumia Nishati safi ya Kupikia na faida zake.
Kupitia mafunzo hayo, NEMC imewafahamisha washiriki wa mafunzo changamoto nane za kimazingira zilizoainishwa katika Sera ya Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2021 ambazo ni pamoja na Mabadiliko ya Tabianchi, Uharibifu wa Ardhi, Uharibifu wa Misitu, Uharibifu wa Vyanzo vya Maji na kupelekea uhaba na maji yenye ubora mijini na vijijini.
NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA UTEKELEZAJI WA MKATABA WA BIOANUAI, PANAMA 2025
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeungana na ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Utekelezaji wa Mkataba wa Bioanuai unaoendelea Jijini Panama kuanzia tarehe 20 hadi 30 Novemba 2025.
Tanzania, ikiwa ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Bioanuai (Convention on Biological Diversity – CBD), imeendelea kuonesha dhamira yake ya kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya bioanuai. Mkutano huu unafanyika katika Ukumbi wa Atlapa Convention Center na unahusisha mikutano miwili mikubwa: SABSTTA-27, inayojadili masuala ya kisayansi, kiufundi na kiteknolojia kuhusu bioanuai; na SB8J-1, inayohusiana na haki na mchango wa jamii za wenyeji katika hifadhi ya bioanuai.
Kupitia ushiriki wake, NEMC imeungana na wadau mbalimbali wakiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, taasisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (TFS na TAWA), pamoja na Shirika la The Nature Conservancy (TNC). Majadiliano katika mikutano hii yamejikita kwenye utekelezaji wa Mkakati wa Dunia wa Kuhifadhi Bioanuai (Kunming–Montreal Global Biodiversity Framework – KMGBF) uliopitishwa mwaka 2022, yakilenga kuweka miongozo ya kuboresha sera, sheria na programu za kitaifa kuhusu hifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Aidha, mada kuu zinazojadiliwa ni pamoja na bioanuai na mabadiliko ya tabianchi, bioanuai na afya, viumbe vamizi, bioanuai na kilimo, pamoja na tathmini za athari za viumbe hai vilivyobadilishwa kijenetiki (LMOs).
Kwa Tanzania, ushiriki huu ni fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu na mataifa mengine kuhusu njia bora za kudhibiti upotevu wa bioanuai na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kupitia jukwaa hili, NEMC inaimarisha nafasi yake katika kuunganisha taaluma, sayansi, na jamii katika utekelezaji wa KMGBF, sambamba na kuandaa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji bora wa sera za mazingira nchini.
Vilevile, majadiliano haya yanatoa nafasi ya kuandaa msimamo wa pamoja wa kikanda kuelekea Mkutano wa 17 wa Mkataba wa Bioanuai utakaofanyika Jijini Yerevan, Armenia mwaka 2026.
Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika mkutano huu ni ushahidi wa dhamira ya Tanzania katika kulinda mazingira na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za asili. Unasisitiza kuwa uhifadhi wa bioanuai ni nyenzo muhimu katika kulinda afya ya jamii, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha usalama wa chakula.
NEMC inaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuhakikisha malengo ya kimataifa ya bioanuai yanatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya taifa na dunia kwa ujumla.
𝗞𝗔𝗠𝗜𝗦𝗛𝗡𝗔 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗞𝗪𝗔 𝗨𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗙𝗨 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔 𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗠𝗠𝗔
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao na watumishi wa NEMC alipozuru Ofisi za Baraza 23 Oktoba, 2025 ikiwa ni ziara yake ya kikazi
Akizungumza leo 23 Oktoba, 2025 jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi ofisi za Baraza Dkt. Laurean Ndumbaro amesema uadilifu uliooneshwa na Baraza hilo ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine za Umma katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa kikao hicho kilichokuwatanisha watumishi wa Baraza na Ugeni kutoka Tume ya Utumishi wa Umma ukiongozwa na Kamishna Dkt. Laurean Ndumbaro.
Amesisitiza kuwa uadilifu ndio nguzo kuu ya utumishi wa umma na ndio msingi wa kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi.
Ameongeza kuwa mafanikio ya NEMC katika utekelezaji wa miradi ya kimazingira pamoja na usimamizi wa Sheria na Kanuni za Mazingira ni ushahidi kwamba viongozi na watumishi wake wameweka maslahi ya Taifa mbele kuliko maslahi binafsi.
Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa akizungumza wakati wa kikao hicho.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amemshukuru Kamishna kwa Tathmini hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu zaidi kwani pongezi hizo ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika ziara yake Kamishna Dkt. Ndumbaro ameambatana na wataalamu wengine akiwemo Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa.
NEMC NA MWAKILISHI KUTOKA ULAYA WAJADILI NA MJUMBE KUTOKA ULAYA USIMAMIZI WA MAZINGIRA KATIKA SEKTA YA MADINI
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na muwakilishi wa ujumbe wa Umoja wa nchi za Ulaya (EU) nchini Tanzania na kujadili namna Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii zinavyofanyika kwa Tanzania na jinsi wanavyoweza kushirikiana na Baraza hususani katika masuala ya kimazingira kwa upande wa Sekta ya madini hasa madini muhimu (Critical Minerals)
Kikao hiki kilijadili miongozo iliyopo na kuainisha maeneo yanayohitaji usaidizi wao ili kuwezesha uzingatiaji wa Sheria kwa miradi ya madini inayowekezwa nchini.
NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...
-
🟢 MAZINGIRA CHALLENGE 📍 Uko wapi Tanzania? 📸 Tuma Picha Bora ya Mazingira Ulipo! 🌍 Lengo la Kampeni: Kuibua uzalendo na uhamasishaji wa ...
-
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha mafunzo maalum ya kuwajengea uelewa kuhusu Tathmini ya Athari kwa ...
-
Msitu wa Kagunga uliopo kijiji cha Kagunga kata ya Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoa wa Tatavi zimepigwa na Mawiti Ufukwe wa bahari ya ...