Nyumbani

ππ„πŒπ‚ π˜π€πˆπ‹π€π™π€ 𝐖𝐂𝐅 πŸ“ ππˆπ‹π€ π’π‡πˆπŒπŒπ”π“π€ πŸπŸŽπŸπŸ“

Timu ya mpira wa miguu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeilaza timu ya WCF kwa jumla ya magoli matano kwa sifuri.

Mchezo huo uliochezwa Novemba 27, 2025, katika uwanja wa Highland mkoani Morogoro, ulianza kwa kasi kubwa ambapo dakika ya 15 Fortinatus Patrick alifungua ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penati, na kufanya “mazingira ya uwanja” kuanza kuwa safi. Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 33 ambapo mfungaji huyo huyo, Fortinatus Patrick, alipachika bao la pili lililoipeleka NEMC mapumzikoni wakiwa kifua mbele, huku “mazingira” yakiendelea kupendeza uwanjani.

Kipindi cha pili kilipoanza dakika ya 46, Fortinatus Patrick aliendeleza ubabe kwa kufunga bao la tatu, kabla ya kiungo Ismail Jemba kuongeza la nne dakika ya 51.

Kama ilivyo desturi ya NEMC kutoridhishwa na uchafuzi wa mazingira nchini na kuendelea kuhimiza usafi kote nchini, vivyo hivyo hawakuridhika na matokeo hayo ya 4–0. Dakika ya 62, Emmanuel Mlungwana alipiga shuti kali kutoka katikati ya uwanja lililopenya kati ya miguu ya golikipa wa WCF na kutinga wavuni, likiwa bao la tano kwa NEMC.

NEMC ipo mkoani Morogoro kushiriki michezo ya SHIMMUTA 2025 kama sehemu ya kuimarisha afya za watumishi wake pamoja na kuendelea kutoa hamasa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini. Kwa mwaka huu, timu za NEMC zimefadhiliwa jezi na vifaa vya michezo kupitia miradi yake miwili — Adaptation Fund na EHPMP — huku zikitumia jezi hizo kueneza jumbe mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi na udhibiti wa matumizi ya zebaki (mercury).




NEMC YAELIMISHA UMMA UDHIBITI WA KELELE CHAFUZI NA MITETEMO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuimarisha juhudi za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kufuatia ongezeko la malalamiko katika maeneo ya mijini na vijijini. 

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Bw. Hamadi Taimuru, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC), amesema kelele zimeendelea kuwa changamoto kubwa kwa afya na ustawi wa wananchi kutokana na shughuli za burudani, ujenzi, biashara na matumizi ya vifaa vya sauti vinavyokiuka viwango vya kisheria.


Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria (NEMC) Bw. Hamadi Taimuru akizungumza na vyombo vya habari alipokuwa akitoa taarifa kwa umma kuhusu kelele chafuzi na mitetemo

Bw. Taimuru amefafanua kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (Sura 191) na Kanuni za Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za mwaka 2015 zimeweka viwango maalumu vya kelele kwa maeneo ya makazi, biashara, viwanda na Taasisi muhimu kama Hospitali na shule, sambamba na kuainisha utaratibu wa utoaji vibali kwa shughuli zinazoweza kusababisha kelele kubwa. 

Amesema athari za kelele za muda mrefu ni pamoja na kupoteza usikivu, msongo wa mawazo, shinikizo la damu na kuathiri umakini wa watoto shuleni, hivyo kulifanya suala la udhibiti kuwa muhimu kwa kulinda afya ya umma".

Aidha, amebainisha uwepo wa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Kanuni za udhibiti, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kupimia kelele kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, uelewa mdogo wa wananchi kuhusu athari za kelele, pamoja na baadhi ya biashara na maeneo ya burudani kutokufuata sheria na muda wa utulivu. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viwango vinavyoruhusiwa ni 70dBA mchana na 60dBA usiku kwa maeneo ya viwandani; 50dBA mchana na 35dBA usiku kwa makazi, 60dBA mchana na 50dBA usiku kwa makazi yenye viwanda vidogo,  55dBA mchana na 45dBA usiku kwa maeneo ya makazi, biashara na burudani; na 45dBA mchana na 35dBA usiku kwa Hospitali, Shule, Kumbi za mikutano na maeneo ya mapumziko.

Katika kuimarisha usimamizi, Bw. Taimuru alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya OSHA, Polisi, BASATA, Serikali za Mitaa, nyumba za ibada na wamiliki wa kumbi za burudani katika kutekeleza majukumu yao, ikiwemo kusimamia vibali, kutoa elimu, kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa vya sauti na kufanya kaguzi za mara kwa mara.

Aliongeza kuwa ramani za viwango vya kelele, kampeni za uelimishaji na mifumo rahisi ya utoaji taarifa za malalamiko ni hatua muhimu zinazohitajika kuimarishwa.

Akihitimisha, Bw. Hamadi Taimuru amesema Tanzania ina mfumo madhubuti wa kisheria wa kudhibiti kelele na mitetemo, na kwamba ushirikiano wa wadau wote, sekta binafsi, Taasisi za umma na wananchi ni msingi muhimu wa kulinda afya, utulivu na ustawi wa jamii.

ππ„πŒπ‚ π˜π€π„ππƒπ„π’π‡π€ πŒπ€π…π”ππ™πŽ π˜π€ ππƒπ€ππˆ 𝐉𝐔𝐔 π˜π€ πŒπ€ππˆπ“πˆπŽ π˜π€ π“π€π€π‘πˆπ…π€ 𝐙𝐀 π“π€π“π‡πŒπˆππˆ π˜π€ π€π“π‡π€π‘πˆ πŠπ–π€ πŒπ€π™πˆππ†πˆπ‘π€ 𝐍𝐀 π‰π€πŒπˆπˆ 𝐍𝐀 πŠπ€π†π”π™πˆ 𝐙𝐀 πŒπ€π™πˆππ†πˆπ‘π€

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kurugenzi ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii limeendelea kujenga uwezo kwa watumishi wake kwa kuendesha mafunzo ya ndani yahusuyo mapitio ya taarifa za Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) pamoja na kaguzi za mazingira. 

Mafunzo hayo ya siku nne yalifanyika kuanzia tarehe 18 hadi 21 Novemba 2025 yakilenga kuongeza weledi na kuimarisha utendaji katika kupitia taarifa na kufanya kaguzi za miradi inayowasilishwa kwa Baraza, kuimarisha umahiri wa watumishi hao na kuandaa timu madhubuti yenye uwezo wa kushughulikia kwa haraka na kwa ubora wa juu taarifa za tathmini na kaguzi za mazingira zinazowasilishwa na wawekezaji kwa Baraza.

Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (NEMC) Bi. Lilian Lukambuzi akiwasilisha mada katika mafunzo hayo
Mafunzo haya yalifunguliwa rasmi na Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii, Bi. Lilian Lukambuzi, na kuendeshwa na wataalamu kutoka ndani ya Kurugenzi hiyo wakiwemo Eng. Luhuvilo Mwamila "Kaimu Meneja Mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii" na Bi. Edika Masisi "Meneja Usajili wa Wataalamu Elekezi wa Mazingira". Washiriki walipata nafasi ya kujifunza kwa undani namna bora za kufanya mapitio ya taarifa za TAM, vigezo vya tathmini, na hatua muhimu katika ukaguzi wa mazingira ili kuhakikisha miradi inazingatia sheria ya Mazingira.

Aidha, mafunzo hayo yaliwalenga watumishi wa NEMC kutoka kanda za Mashariki Kaskazini, Mashariki Kusini, Ilala, Temeke, Bagamoyo pamoja na Makao Makuu.














NEMC YASHIRIKI UNFCCC COP- 30, BELEM, NCHINI BRAZIL, USHIRIKI WAKE KULETA MANUFAA KWENYE MIRADI NA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Mkutano wa thelathini wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC COP-30), unaoendelea jijini BΓ©lem, nchini Brazil kuanzia tarehe 03/11/2025 na unatarajiwa kukamilika tarehe 21/11/2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo (wa pili kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya NEMC iliyoshiriki Mkutano huo na baadhi ya washiriki kutoka mataifa mengine. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi

Akiongoza ujumbe wa NEMC katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mhandisi Mwanasha Tumbo aliyeambatana pia na Makamu Mwenyekiti, Wakili Alex G. Mgongolwa aliwataka watumishi wa Baraza kuhakikisha wanatumia vyema jukwaa la mkutano huo kupata fursa za fedha za miradi ili kuweza kuhakikisha unaleta matokeo chanya katika kutekeleza vyema nguzo ya mazingira katika Dira ya Taifa ya 2050.

Katika kutekeleza hilo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, ameongoza ujumbe wa NEMC kwenye Mikutano mbalimbali ya uwili ili kuimarisha ushirikiano na wadau katika sekta ya Mazingira. 

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza katika Mkutano huo
Baadhi ya Mikutano hiyo ni pamoja na mkutano wa uwili na Benki ya Maendeleo ya Africa (African Development Bank), uliohusu kuanza kwa mradi uliowasilishwa na Baraza na kupitishwa na benki hiyo. Mradi huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 15 unatarajiwa kutatua changamoto za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya pwani yaani Dar es Salaam, Pwani na Pemba. 

Aidha, Dkt. Semesi alikutana pia na Sekretarieti ya Mfuko wa Kimataifa wa kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund-AF) ambapo aliweza kuwahimiza Adaptation Fund kukamilisha taratibu za kulipatia Baraza ithibati ya pili (reaccreditation) sambamba na kukamilisha mapitio ya miradi iliyowasilishwa yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani milioni 35. Katika mazungumzo hayo, mfuko wa  Adaptation Fund umelihakikishia Baraza kwamba taratibu za ithibati zitakamilika ndani ya wiki chache kuelekea mwishoni mwa mwaka huu. 

Hata hivyo Adaptation Fund umeidhinisha ripoti za mwaka za miradi ya SWAHAT na Bunda inayosimamiwa na Baraza Pamoja na kuachilia kiasi cha takribani Dola za Marekani laki 4 ili kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Mtaalam wa Mazingira (NEMC) ndugu. Paul Kalokola akifafanua jambo katika Mkutano huo
Sambamba na hayo, Dkt. Semesi ameongoza ushiriki katika vikao mbalimbali vya kitaalam, mikutano ya pembezoni pamoja na kuanzisha mchakato wa mashirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kupanua wigo wa kujipatia fedha za kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya taasisi hizo ni pamoja na Mfuko wa Kitaifa wa Maji (National Water Fund), Pew Charitable Trust, Benki ya Dunia, Global Climate Mobility, Global Methen Hub, IUCN na Ocean Vision.

Timu ya wataalam iliyoambatana na ujumbe wa Bodi kwenye Mkutano huo ni pamoja na Dkt Careen Kahangwa, Bw. Fredrick Mulinda, Bw, Paul Kalokola, Bi. Jackline Nyantori na Bw. Rahim Kantinga.

NEMC YASHIRIKI KIKAO KAZI CHA KUPITIA MPANGO WA KITAIFA WA KUPAMBANA NA UKAME

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikao kazi cha kupitia Mpango wa Kitaifa wa kupambana na ukame kilichofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), mkoani Morogoro.
Akizungumza katika kikao hicho, muwakilishi kutoka NEMC ambaye pia ni Afisa Mazingira Mkuu Bi.Marlene Moshi amesema ushiriki wa NEMC ni muhimu katika kuhakikisha kuwa mikakati ya kitaifa inakwenda sambamba na malengo ya kimataifa ya kupunguza athari za ukame na kulinda mazingira.

Kikao hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais (VPO) kupitia Idara ya Mazingira, kikilenga kuhakikisha utekelezaji wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame Duniani.


NEMC YACHOTA HAZINA KUBWA YA NAMNA YA KUHIFADHI NA KUSIMAMIA MAZINGIRA KUTOKA KWA DKT. MPANGO

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akimkabidhi zawadi Makamu wa Rais mstaafu Dkt. Philip Isdor Mpango (wa katikati) alipoambatana na timu ya NEMC na kumtembelea nyumbani kwake Mayamaya jijini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira Dkt. Menan Jangu (NEMC).

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Novemba 11, 2025 limefanya ziara maalum nyumbani kwa Makamu wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, eneo la Mayamaya mkoani Dodoma, ambapo mazungumzo yenye tija kubwa kuhusu hali ya mazingira nchini yamefanyika.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Mpango ameelezea kwa kina wasiwasi wake kuhusu kasi ya uharibifu wa mazingira unaoendelea kushamiri nchini, huku akisisitiza haja ya kuwepo kwa msukumo mkubwa zaidi katika kulinda maeneo ya hifadhi na kusimamia matumizi bora ya ardhi.

Amesema kuwa maeneo mengi ya hifadhi yamekuwa yakivamiwa, mito mingi imechepushwa kinyume na taratibu, huku mabwawa ya kuzalisha umeme yakikumbwa na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu. Vilevile, biashara ya mbao na mkaa imeendelea kuchangia ongezeko la ukataji miti na hivyo kuongeza kasi ya uharibifu wa misitu nchini.

Dkt. Mpango amebainisha kuwa changamoto za mifugo isiyo na utaratibu mzuri, uchimbaji holela wa mashamba, pamoja na tatizo la mimea vamizi, vinahitaji mikakati madhubuti ya kitaifa. Amesisitiza kuwa NEMC inapaswa kupewa nguvu zaidi katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni za mazingira, akisema: “Sauti ya NEMC isiwe tena sauti ya mtu aliye nyikani.”

Makamu wa Rais mstaafu Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza wakati alipotembelewa na timu ya NEMC nyumbani kwake Mayamaya jijini Dodoma

Aidha, Dkt. Mpango ametoa wito kwa Serikali na jamii kwa ujumla kutekeleza kwa vitendo mpango wa Kijanisha mazingira  “Greening the Environment”, huku akipendekeza kuanzishwa kwa green parks na botanical gardens katika Majiji na Miji mikuu ya nchi, kama sehemu ya kujenga miji yenye mazingira rafiki na yenye afya.

“Ni lazima tujiulize kama Taifa, kama miji, tumechukua hatua gani za kulinda na kurejesha uoto wa asili? Inawezekana kabisa kuwa na mazingira mazuri kama tukidhibiti shughuli zetu kwa kufuata sheria na mipango tuliyojiwekea,” amesisitiza Dkt. Mpango.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alipozungumza alipongeza maono na ushauri uliotolewa Dkt. Mpango, huku akiahidi kuendelea kutumia maarifa hayo katika kuimarisha juhudi za Hifadhi na Usimamizi endelevu wa mazingira nchini.

Ziara hiyo iliyofanywa na Menejimenti ya Baraza imekuwa ni ya muhimu katika kujenga mashirikiano kati ya Taasisi za Serikali na viongozi wastaafu wenye uzoefu mkubwa, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inabaki kuwa nchi yenye mazingira safi, salama, na yenye uendelevu wa kiikolojia.

Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Isdor Mpango akipokea zawadi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, wakati Uongozi wa NEMC ulipomtembelea nyumbani kwake mjini Dodoma

Makamu wa rais mstaafu Dkt. Philip Isdor Mpango (wa tisa kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya NEMC iliyoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi ilipomtembelea nyumbani kwake Mayamaya jijini Dodoma Novemba 11, 2025.

NEMC YAJINASIBU KUFANYA MAKUBWA SHIMMUTA 2025, YAPOKEA VIFAA KUTOKA MRADI WA ADAPTATION FUND


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limejipanga kisawasawa kushiriki mashindano ya michezo yanayoratibiwa na  Shirikisho la Michezo la Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni binafsi Tanzania (SHIMMUTA) ambapo tarehe 28 Oktoba, 2025 limezindua rasmi vifaa vilivyofadhiliwa na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation fund) vitakavyotumika na wanamichezo katika mashindano hayo.

Akizungumza wakati kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi amesema michezo ni  muhimu kwa Afya ya binadamu  kwani hupelekea uwezo wa kufanya kazi vizuri huku akisisitiza usimamizi na uhifadhi wa Mazingira nchini


Ameongeza kuwa ushiriki wa NEMC katika michezo hiyo ni fursa muhimu ya kuifikia jamii, kuimarisha ushirikiano baina ya watumishi wa Umma na Sekta binafsi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Michezo - NEMC Bw. Fortinatus Patrick amesema timu za NEMC ziko tayari kwenda kupambana katika michezo yote na wamejiandaa kufanya vizuri katika mashindano ya mwaka huu.





Naye Mkurugenzi wa Utawala na Fedha (NEMC) Bw. Dickson Mjinja ambaye ni mlezi qa timu hiyo, alipozungumza amesema NEMC imejipanga kisawasawa kuwa washindani na si washiriki katika michezo yote iliyo jisajili.

NEMC kwa kushirikiana na Mradi wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi umefanikisha Mandalizi hayo ya SHIMMUTA 2025 yanayotarajiwa kuafanyika jijini Mwanza November 13 - 29, 2025 huku ikilenga kuelimisha umma wa watanzania  kuhusu mazingira na masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi






NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...