Nyumbani

𝐌𝐈𝐀𝐊𝐀 𝟒𝟎 𝐘𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂: 𝐒𝐀𝐅𝐀𝐑𝐈 𝐘𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀 𝐊𝐔𝐄𝐋𝐄𝐊𝐄𝐀 𝐌𝐔𝐒𝐓𝐀𝐊𝐀𝐁𝐀𝐋𝐈 𝐖𝐀 𝐊𝐈𝐉𝐀𝐍𝐈 𝐍𝐀 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐎 𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐕𝐔

Katika dunia inayokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na kupungua kwa rasilimali asilia, Tanzania inaendelea kuwa mfano wa matumaini na uthabiti kupitia juhudi zake za kulinda mazingira. Maadhimisho ya miaka 40 ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yanaonesha dhamira ya Taifa kulinda mazingira huku likiendeleza uchumi.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1986, NEMC imekuwa mhimili wa usimamizi wa mazingira nchini. Zaidi ya miradi 35,000 imepitia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), hatua iliyosaidia kuoanisha maendeleo ya kiuchumi na ulinzi wa mazingira. Pia, utoaji wa vibali zaidi ya 28,000 umeimarisha uzingatiaji wa viwango vya mazingira na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania kimataifa, huku juhudi za kudhibiti uchafuzi zikiepusha gharama kubwa za kurekebisha madhara.

Katika kujenga uwezo, wataalamu zaidi ya 12,000 wamepata mafunzo, na hivyo kuimarisha usimamizi wa mazingira katika sekta mbalimbali. Hii inaonesha kuwa mazingira si suala la pembeni bali ni msingi wa uchumi wa taifa, hasa katika sekta kama kilimo na utalii zinazotegemea rasilimali asilia.

Hata hivyo, changamoto bado zipo. Uharibifu wa misitu, kilimo kisicho endelevu na matumizi ya nishati zisizo rafiki vinaendelea kuathiri mazingira. Aidha, athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mafuriko zinaathiri maisha ya wananchi na uzalishaji. Hali hii inahitaji si sera pekee bali pia mabadiliko ya mtazamo, matumizi ya teknolojia na ushirikiano wa wadau wote.

Kupitia ushirikiano huo, wananchi zaidi ya milioni 4.2 wamefikiwa na elimu ya mazingira, huku sekta binafsi ikiongeza uwekezaji katika teknolojia safi na uzalishaji endelevu. Maboresho ya sera na sheria pia yameiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kimataifa katika masuala ya mazingira.

Kuelekea kilele cha maadhimisho tarehe 29 Mei 2026, shughuli kama upandaji wa miti 40,000 na utoaji wa elimu zinaonesha dhamira ya kuchukua hatua zaidi. Huu ni wakati wa kutafakari urithi tunaotaka kuacha kwa vizazi vijavyo.

Kwa ujumla, mafanikio ya miaka 40 ya NEMC yanaonesha kuwa Tanzania ina uwezo wa kufikia maendeleo endelevu. Hata hivyo, mafanikio ya baadaye yatategemea maamuzi ya sasa, ambapo kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda mazingira kwa vitendo.

“𝑴𝒂𝒛𝒊𝒏𝒈𝒊𝒓𝒂 𝒔𝒊 𝒖𝒓𝒊𝒕𝒉𝒊 𝒕𝒖𝒍𝒊𝒐𝒖𝒑𝒐𝒌𝒆𝒂 𝒃𝒂𝒍𝒊 𝒏𝒊 𝒅𝒉𝒂𝒎𝒂𝒏𝒂 𝒕𝒖𝒍𝒊𝒚𝒐𝒂𝒛𝒊𝒎𝒂 𝒌𝒖𝒕𝒐𝒌𝒂 𝒌𝒘𝒂 𝒗𝒊𝒛𝒂𝒛𝒊 𝒗𝒊𝒋𝒂𝒗𝒚𝒐.”

NEMC NA ZEMA KUIMARISHA MASHIRIKIANO KATIKA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  na Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) wamekutana Zanzibar Aprili 27,2026 katika ziara ya mafunzo, kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu ya kimazingira, hasa mchakato wa ufanyaji wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na jamii katika miradi mikubwa na mchakato wa kupata vyeti vya kimazingira ili kuhakikisha maendeleo yanaendana na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, iliyohusisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya pande zote mbili, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo, alisema Bara na Visiwani ni wamoja na hasa ikizingatiwa suala la mazingira ni mtambuka linalohitaji ushirikiano wa karibu kati ya pande zote mbili hatuna budi kutekeleza kwani mashirikiano katika sekta ya mazingira ni muhimu na kwakuwa limepewa kipaumbele katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha mazingira yanasimamiwa na kuhifadhiwa kwa ufanisi. 

Naye  Mwenyekiti wa Bodi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar (ZEMA) Bi. Asha Ali Khatib alipozungumza alisema ni muhimu masuala ya mchakato wa ufanyaji wa  Tathmini ya Athari kwa Mazingira kuzingatiwa na wawekezaji  kuanzia hatua za awali hadi kukamilika kwa miradi ili kulinda mazingira huku akisistiza umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji wa jamii pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuhakikisha usimamizi na uhifadhi wa mazingira unafanyika kwa ufanisi.

Katika ziara hiyo, washiriki pia walipata wasilisho la kina kuhusu mchakato wa Tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wake kwa pande zote mbili yaliyotoa fursa ya majadiliano yenye kujenga kwa maendeleo endelevu ya mazingira.

Aidha, wajumbe hao walitembelea maeneo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri pamoja na Hoteli ya Verde iliyofanyiwa ufukiaji (reclamation) hali  iliyowasaidia washiriki kuona kwa karibu jinsi tathmini za mazingira zinavyotekelezwa katika miradi mikubwa na umuhimu wake katika kulinda rasilimali za asili.

Ziara hii ni kufuatia makubaliano ya awali yaliyowakutanisha katika kikao cha Tarehe 08/10/2025 chenye maazimio ya kuimarisha mashirikiano katika sekta ya Uhifdhi na Usimamizi wa Mazingira.









NEMC YAKABIDHIWA CHETI NA MAKAMU WA RAIS MHE.BALOZI DKT. EMMANUEL NCHIMBI, USHIRIKI WA SHEREHE ZA USIKU WA MUUNGANO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhiwa cheti na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi cha shukrani ya ushiriki katika sherehe za Usiku wa Muungano zenye kaulimbiu isemayo " Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja na Mshikamano ni msingi wa maendeleo endelevu zilizofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre Jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi cheti hicho, Mhe. Nchimbi alieleza umuhimu wa Taasisi mbalimbali za umma kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaifa zinazolenga kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, ushiriki wa NEMC katika hafla hiyo umeakisi dhamira ya Taasisi hiyo katika kuendeleza juhudi za kuunga mkono shughuli za Uhifadhi wa mazingira sambamba na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ajenda za kitaifa.








𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗡𝗔 𝗦𝗪𝗘𝗖𝗢 𝗬𝗔𝗦𝗔𝗜𝗡𝗜 𝗠𝗞𝗔𝗧𝗔𝗕𝗔 𝗪𝗔 𝗨𝗣𝗘𝗠𝗕𝗨𝗭𝗜 𝗬𝗔𝗞𝗜𝗡𝗜𝗙𝗨-𝗠𝗜𝗥𝗔𝗗𝗜 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗞𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔 𝗡𝗜𝗦𝗛𝗔𝗧𝗜

NEMC kwa kushirikiana na Kampuni ya SWECO AB ya Sweden, wamesaini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa kubadili taka kuwa nishati tarehe 16 Aprili 2026 katika ofisi za NEMC, jijini Dar es Salaam. 

Upembuzi huo yakinifu utatekelezwa katika Mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza na unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Swedfund AB kutoka Sweden. 

Lengo la mradi huu ni kuchochea ukuaji wa uchumi rejelezi na kufanya taka kuwa fursa, hususan taka ozo, kwa kuzigeuza kuwa rasilimali yenye kuweza kutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme au kuzalisha mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo magari katika maeneo ya mijini.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika kukabiliana na changamoto ya ongezeko la taka zinazozalishwa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Kupitia mradi huu, NEMC inaendelea kusisitiza usimamizi endelevu wa taka, utenganishi wa taka katika vyanzo na matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijani.

𝐖𝐀𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐖𝐀𝐂𝐇𝐀𝐑𝐔𝐊𝐀 𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄𝐍𝐈, 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐊𝐔𝐏𝐄𝐖𝐀 𝐌𝐄𝐍𝐎

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameibuka na hoja nzito wakichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wakitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa mamlaka kamili pamoja na rasilimali za kutosha ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wakichangia kwa nyakati tofauti baada ya hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, wabunge hao walisema licha ya NEMC kupewa jukumu la kusimamia na kulinda mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), bado haina nguvu ya kisheria ya kutosha kuchukua hatua kali dhidi ya waharibifu wa mazingira.
Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Mhe. Christina Mndeme, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha NEMC kupata maabara inayotembea, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi katika udhibiti wa mazingira kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Aidha, alisisitiza kuwa endapo NEMC itapewa mamlaka kamili, uwajibikaji utaongezeka, ufanisi utaimarika na taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kisheria bila muingiliano wowote kutoka taasisi nyingine.
Naye Mbunge wa Katavi, Mhe. Thomas Kampala, alipoongea alisisitiza kuwa ipo haja ya haraka ya kuipa NEMC “meno” ili iweze kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyoongezeka nchini. Alieleza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inakosa nguvu ya kisheria hata inapobaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria za mazingira.
Kadhalika Mbunge wa Bumbuli, Mhandisi Ramadhan Hamza Singano, aliongeza kuwa pamoja na NEMC kufanya kaguzi katika sekta mbalimbali ikiwemo migodi, gesi na mafuta, bado inakabiliwa na uhaba wa rasilimali kutokana na mgao mdogo wa bajeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassari, aliunga mkono hoja hiyo akitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kuimarisha NEMC ili iweze kusimamia kikamilifu uhifadhi wa mazingira. 

Wabunge hao walisisitiza kuwa bila kuipa NEMC mamlaka kamili na rasilimali za kutosha, jitihada za kulinda mazingira nchini zitabaki kuwa dhaifu.




NEMC YATOA TUZO KWA MSHINDI WA JUMLA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi tuzo kwa Mkoa wa Njombe ikiwa ni Mshindi wa Jumla wa Shindano la Afya na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2024.


Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mgeni Rasmi wa Mkutano Maalum wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba Aprili 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).

Akimkabidhi Tuzo hiyo Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Silas Shemdoe amesema tuzo hiyo imetolewa na NEMC kwa kuthamini mchango wa Mkoa wa Njombe katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.


Akizungumza na baadhi ya Waheshimiwa Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Njombe mara baada ya zoezi hilo la utoaji wa Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza kwa kuchukulia suala la Mazingira kwa umuhimu mkubwa na kutoa rai kwa Halmashauri nyingine Nchi nzima kuiga mfano wa Mkoa wa Njombe.


Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makete, Mhe. Rabson A. Mahenge ameishukuru NEMC kwa kuthamini mchango wao katika kutunza mazingira na amesisitiza kuwa NEMC iendelee kutoa maelekezo Mkoa wa Njombe utatekeleza na matokeo yataonekana.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo NEMC huendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kila mwaka. Mwaka 2024, na miaka mingine Mkoa wa Njombe umekuwa kinara katika uimarishaji wa huduma za usafi wa Mazingira.


Mkoa huo umekuwa ukiongoza kwa kuwa na kaya zenye vyoo bora, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika ngazi ya kaya, Shule na Vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, mkoa umekuwa mfano na darasa kujifunza kwa Halmashauri nyingine katika masuala ya udhibiti wa taka ngumu na maji taka. Hali hii ya Mkoa inachangiwa na viongozi ngazi zote kuamua pamoja na wananchi kuyapa kipaumbele masuala ya usafi wa mazingira, hali inayochangia Mkoa kutopata visa vya ugonjwa wa kipindipundu kwa muda mrefu na wananchi kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.










NEMC YAKUTANA NA TAASISI ZA SERIKALI NA WADAU WA SEKTA YA MADINI GEITA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya mkutano na wadau wa mazingira tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukumbusha wadau kuhusu haki na wajibu wao katika kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake. Katika mkutano huo, viongozi wa NEMC waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuimarisha uelewa wa utekelezaji sahihi wa sheria hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira.


Aidha, wawekezaji walisisitizwa umuhimu wa kufanya usajili na kukamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao. Hatua hii inalenga kulinda mazingira, afya za binadamu na viumbe hai wengine, pamoja na kuepusha hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya miradi isiyozingatia taratibu.


Kwa upande mwingine, taasisi za serikali zilihimizwa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za mazingira. NEMC imeeleza kuwa itaendelea kuandaa mikutano kama hii katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji kuelekea maendeleo endelevu ya taifa.


Taasisi za serikali zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Halmashauri za Geita, Kahama na Shinyanga, Tume ya Madini, Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

MWENYEKITI WA BODI YA NEMC AZUNGUMZA NA WADAU WA MAZINGIRA, NEMC@40

Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC, Mhandisi Mwanasha Tumbo akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka Arobaini (40) ya Baraza la Taifa la Hifadhi n...