Nyumbani

NEMC YAKABIDHIWA CHETI NA MAKAMU WA RAIS MHE.BALOZI DKT. EMMANUEL NCHIMBI, USHIRIKI WA SHEREHE ZA USIKU WA MUUNGANO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhiwa cheti na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt.Emmanuel Nchimbi cha shukrani ya ushiriki katika sherehe za Usiku wa Muungano zenye kaulimbiu isemayo " Miaka 62 ya Muungano: Amani, Umoja na Mshikamano ni msingi wa maendeleo endelevu zilizofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre Jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi cheti hicho, Mhe. Nchimbi alieleza umuhimu wa Taasisi mbalimbali za umma kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaifa zinazolenga kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, ushiriki wa NEMC katika hafla hiyo umeakisi dhamira ya Taasisi hiyo katika kuendeleza juhudi za kuunga mkono shughuli za Uhifadhi wa mazingira sambamba na kushirikiana na Serikali katika kutekeleza ajenda za kitaifa.








𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗡𝗔 𝗦𝗪𝗘𝗖𝗢 𝗬𝗔𝗦𝗔𝗜𝗡𝗜 𝗠𝗞𝗔𝗧𝗔𝗕𝗔 𝗪𝗔 𝗨𝗣𝗘𝗠𝗕𝗨𝗭𝗜 𝗬𝗔𝗞𝗜𝗡𝗜𝗙𝗨-𝗠𝗜𝗥𝗔𝗗𝗜 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗞𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔 𝗡𝗜𝗦𝗛𝗔𝗧𝗜

NEMC kwa kushirikiana na Kampuni ya SWECO AB ya Sweden, wamesaini mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu kwa mradi wa kubadili taka kuwa nishati tarehe 16 Aprili 2026 katika ofisi za NEMC, jijini Dar es Salaam. 

Upembuzi huo yakinifu utatekelezwa katika Mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza na unafadhiliwa na Shirika la maendeleo la Swedfund AB kutoka Sweden. 

Lengo la mradi huu ni kuchochea ukuaji wa uchumi rejelezi na kufanya taka kuwa fursa, hususan taka ozo, kwa kuzigeuza kuwa rasilimali yenye kuweza kutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme au kuzalisha mafuta ya kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo magari katika maeneo ya mijini.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika kukabiliana na changamoto ya ongezeko la taka zinazozalishwa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali. Kupitia mradi huu, NEMC inaendelea kusisitiza usimamizi endelevu wa taka, utenganishi wa taka katika vyanzo na matumizi bora ya rasilimali kwa ajili ya kulinda mazingira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kijani.

𝐖𝐀𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄 𝐖𝐀𝐂𝐇𝐀𝐑𝐔𝐊𝐀 𝐁𝐔𝐍𝐆𝐄𝐍𝐈, 𝐖𝐀𝐓𝐀𝐊𝐀 𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐊𝐔𝐏𝐄𝐖𝐀 𝐌𝐄𝐍𝐎

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameibuka na hoja nzito wakichangia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), wakitaka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa mamlaka kamili pamoja na rasilimali za kutosha ili liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Wakichangia kwa nyakati tofauti baada ya hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, wabunge hao walisema licha ya NEMC kupewa jukumu la kusimamia na kulinda mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), bado haina nguvu ya kisheria ya kutosha kuchukua hatua kali dhidi ya waharibifu wa mazingira.
Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora, Mhe. Christina Mndeme, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha NEMC kupata maabara inayotembea, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi katika udhibiti wa mazingira kwa kutumia ushahidi wa kisayansi. Aidha, alisisitiza kuwa endapo NEMC itapewa mamlaka kamili, uwajibikaji utaongezeka, ufanisi utaimarika na taasisi hiyo itakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kisheria bila muingiliano wowote kutoka taasisi nyingine.
Naye Mbunge wa Katavi, Mhe. Thomas Kampala, alipoongea alisisitiza kuwa ipo haja ya haraka ya kuipa NEMC “meno” ili iweze kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyoongezeka nchini. Alieleza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inakosa nguvu ya kisheria hata inapobaini ukiukwaji mkubwa wa Sheria za mazingira.
Kadhalika Mbunge wa Bumbuli, Mhandisi Ramadhan Hamza Singano, aliongeza kuwa pamoja na NEMC kufanya kaguzi katika sekta mbalimbali ikiwemo migodi, gesi na mafuta, bado inakabiliwa na uhaba wa rasilimali kutokana na mgao mdogo wa bajeti.

Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Mhe. Joshua Nassari, aliunga mkono hoja hiyo akitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi kuimarisha NEMC ili iweze kusimamia kikamilifu uhifadhi wa mazingira. 

Wabunge hao walisisitiza kuwa bila kuipa NEMC mamlaka kamili na rasilimali za kutosha, jitihada za kulinda mazingira nchini zitabaki kuwa dhaifu.




NEMC YATOA TUZO KWA MSHINDI WA JUMLA WA UTUNZAJI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekabidhi tuzo kwa Mkoa wa Njombe ikiwa ni Mshindi wa Jumla wa Shindano la Afya na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka 2024.


Tuzo hiyo imekabidhiwa na Mgeni Rasmi wa Mkutano Maalum wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba Aprili 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC).

Akimkabidhi Tuzo hiyo Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Silas Shemdoe amesema tuzo hiyo imetolewa na NEMC kwa kuthamini mchango wa Mkoa wa Njombe katika Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira.


Akizungumza na baadhi ya Waheshimiwa Wenyeviti na Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Njombe mara baada ya zoezi hilo la utoaji wa Tuzo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amewapongeza kwa kuchukulia suala la Mazingira kwa umuhimu mkubwa na kutoa rai kwa Halmashauri nyingine Nchi nzima kuiga mfano wa Mkoa wa Njombe.


Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya Mkoa wa Njombe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Makete, Mhe. Rabson A. Mahenge ameishukuru NEMC kwa kuthamini mchango wao katika kutunza mazingira na amesisitiza kuwa NEMC iendelee kutoa maelekezo Mkoa wa Njombe utatekeleza na matokeo yataonekana.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo NEMC huendesha mashindano ya Afya na Usafi wa Mazingira kila mwaka. Mwaka 2024, na miaka mingine Mkoa wa Njombe umekuwa kinara katika uimarishaji wa huduma za usafi wa Mazingira.


Mkoa huo umekuwa ukiongoza kwa kuwa na kaya zenye vyoo bora, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika ngazi ya kaya, Shule na Vituo vya kutolea huduma za afya. Aidha, mkoa umekuwa mfano na darasa kujifunza kwa Halmashauri nyingine katika masuala ya udhibiti wa taka ngumu na maji taka. Hali hii ya Mkoa inachangiwa na viongozi ngazi zote kuamua pamoja na wananchi kuyapa kipaumbele masuala ya usafi wa mazingira, hali inayochangia Mkoa kutopata visa vya ugonjwa wa kipindipundu kwa muda mrefu na wananchi kuendelea kujishughulisha na shughuli za kiuchumi.










NEMC YAKUTANA NA TAASISI ZA SERIKALI NA WADAU WA SEKTA YA MADINI GEITA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefanya mkutano na wadau wa mazingira tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.


Mkutano huo uliwakutanisha wadau wa sekta ya madini kutoka Mkoa wa Geita pamoja na viongozi mbalimbali kutoka taasisi za serikali.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kukumbusha wadau kuhusu haki na wajibu wao katika kuzingatia Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake. Katika mkutano huo, viongozi wa NEMC waliwasilisha mada mbalimbali zilizolenga kuimarisha uelewa wa utekelezaji sahihi wa sheria hiyo, ili kuhakikisha kuwa shughuli za kiuchumi haziathiri mazingira.


Aidha, wawekezaji walisisitizwa umuhimu wa kufanya usajili na kukamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (ESIA) kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao. Hatua hii inalenga kulinda mazingira, afya za binadamu na viumbe hai wengine, pamoja na kuepusha hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya miradi isiyozingatia taratibu.


Kwa upande mwingine, taasisi za serikali zilihimizwa kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na utekelezaji wa sheria za mazingira. NEMC imeeleza kuwa itaendelea kuandaa mikutano kama hii katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa na uwajibikaji kuelekea maendeleo endelevu ya taifa.


Taasisi za serikali zilizoshiriki katika mkutano huo ni pamoja na Halmashauri za Geita, Kahama na Shinyanga, Tume ya Madini, Ofisi ya Bonde la Ziwa Victoria, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)

TAKA SI UCHAFU TENA, TAKA NI FURSA!


📌 Waziri Masauni aipongeza NEMC kwa kubadilisha mitazamo ya watu juu ya Taka

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Y. Masauni, ameipongeza NEMC kwa kushirikiana na wadau wa mazingira katika juhudi za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu taka na kuzigeuza kuwa fursa yenye manufaa ya kiuchumi na kimazingira.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Taka Duniani yaliyofanyika leo, Machi 30, 2026, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Mhe. Masauni amesisitiza umuhimu wa kuendeleza dhana ya kupunguza, kutumia tena na kurejeleza taka (Reduce, Reuse, Recycle), sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “kupunguza taka katika sekta ya chakula.”

"Taka siyo uchafu bali ni fursa; tukizisimamia vizuri tunaweza kuzigeuza kuwa rasilimali yenye thamani kwa maendeleo endelevu.” Amesema Waziri Masauni.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, amesisitiza kuendelea kwa utoaji wa elimu ya mazingira hususan shuleni kuanzia ngazi ya msingi, pamoja na kuimarisha mafunzo kwa makampuni ya ukusanyaji taka kwa kushirikiana na NEMC ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa jamii ili kuongeza uelewa juu ya usimamizi bora wa taka na kuchochea ushiriki wa wananchi katika kulinda mazingira.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuhamasisha jamii kutambua thamani ya taka na kuzitumia kama rasilimali kwa maendeleo endelevu, huku yakiwakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira.













𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗢𝗡𝗚𝗢𝗭𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗔𝗡𝗢- 𝗪𝗔𝗥𝗦𝗛𝗔 𝗬𝗔 𝗞𝗜𝗞𝗔𝗡𝗗𝗔 𝗞𝗔𝗧𝗜 𝗬𝗔𝗞𝗘 𝗡𝗔 𝗖𝗦𝗘 𝗡𝗔 𝗜𝗡𝗗𝗜𝗔



 𝗡𝗶 𝗞𝗮𝘁𝗶𝗸𝗮 𝗙𝘂𝗿𝘀𝗮 𝘇𝗶𝗹𝗶𝘇𝗼𝗽𝗼 𝗸𝘄𝗲𝗻𝘆𝗲 𝗨𝘀𝗶𝗺𝗮𝗺𝗶𝘇𝗶 𝘄𝗮 𝘁𝗮𝗸𝗮 𝘇𝗮 𝗠𝗮𝘁𝗮𝗶𝗿𝗶 𝗖𝗵𝗮𝗸𝗮𝘃𝘂

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Machi 25, 2026, limeendelea kuongoza majadiliano katika siku ya pili ya warsha ya Kikanda kuchochea fursa mpya katika Usimamizi wa taka za matairi chakavu ambapo mawasilisho ya kanuni za Usimamizi wa matairi chakavu (End-of-Life Tyres – ELTs) katika nchi zinazotekeleza mfumo wa Extended Producer Responsibility (EPR) yalifanyika.

Aidha, wasilisho la kitaalamu kutoka kituo cha Afrika Kusini cha kukuza uzalishaji wa kijani kuhusu umuhimu wa usimamizi wa matairi chakavu katika kulinda mazingira, kuchochea uchumi wa kijani na kuunda ajira, huku washiriki kutoka Ghana wakishirikisha uzoefu wa matumizi mbadala ya matairi chakavu na mbinu za kuwaunganisha wakusanyaji wadogo katika mfumo rasmi.

Kadhalika, mwakilishi kutoka Much Asphalt - Afrika Kusini aliwasilisha kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa zinazotumia matairi chakavu katika ujenzi wa barabara kama njia ya kuongeza thamani ya taka na kuboresha uimara wa barabara.

Kupitia warsha hiyo, NEMC imeongeza uelewa wa kuhusu mbinu bora za kuthibiti taka zitokanazo na matairi chakavu na kukuza uchumi rejeleshi.

SERIKALI YASISITIZA UWAJIBIKAJI WA MAZINGIRA KWA VIWANDA NA WADAU WA TAKA HATARISHI

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria za mazingira kwa sekta ya viwanda, kampuni za uteketezaji taka pamoja na wadau w...