Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) – Kanda ya Ziwa Victoria Magharibi, limeshiriki ziara ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, iliyofanyika mkoani Kagera tarehe 16.03.2026, kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira.
Katika ziara hiyo, Dkt. Muyungi alitembelea Shule ya Sekondari Rugambwa iliyopo Manispaa ya Bukoba pamoja na Shule ya Msingi Hosiana iliyopo Wilaya ya Karagwe. Lengo la ziara hizo lilikuwa kujionea namna taasisi za elimu zinavyotekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuhamia matumizi ya nishati safi ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaochangia mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, Katibu Mkuu alitembelea mradi wa Kaderes Enterprise uliopo Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera, ambapo alipata fursa ya kujionea juhudi za wadau katika utekelezaji wa miradi ya kaboni (carbon credit) inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kuchangia katika uhifadhi wa mazingira.
Katika ziara hiyo, Dkt. Muyungi alisisitiza masuala mbalimbali kama vipaumbele vya kitaifa:
- Matumizi ya Nishati Safi: Kuimarisha matumizi ya nishati mbadala kama vile majiko banifu, gesi asilia, nishati ya jua na umeme safi ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda misitu, na kuboresha afya ya jamii.
- Udhibiti wa Hewa Ukaa: Kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi (GHGs) kupitia teknolojia rafiki kwa mazingira, ufanisi wa matumizi ya nishati, na utekelezaji wa miradi ya upandaji miti na uhifadhi wa misitu.
- Biashara ya Kaboni: Kukuza uelewa na ushiriki wa wadau katika miradi ya Kaboni kama fursa ya kiuchumi, ambapo jamii na taasisi zinaweza kunufaika kifedha kupitia uhifadhi wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
- Ushirikishwaji wa Taasisi zenye zaidi ya watu 100: Kuhamasisha taasisi za serikali na zisizokuwa za serikali zenye watu zaidi ya 100 kuwa vinara wa matumizi ya nishati safi na elimu ya mazingira kwa vitendo.
-Pamoja na Uzingatiaji wa Sera na Sheria: Kusisitiza uzingatiaji wa miongozo na Sheria za Mazingira.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni