Nyumbani

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa kufanyika Septemba 15–16, 2026 Ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujadili mikakati ya kuhakikisha unaleta tija katika ajenda ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amesema ushirikiano kati ya NEMC na TGS ni muhimu katika kuongeza uelewa, ubunifu na ushiriki wa wadau, hususan vijana, katika kutafuta suluhisho la changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

"NEMC, kama mlezi wa Tanzania Green Summit, ataendelea kuunga mkono majukwaa yanayochochea uendelevu wa mazingira, hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na ushiriki wa vijana katika ajenda ya mazingira na maendeleo endelevu" amesisitiza Dkt.Sware Semesi

Tanzania Green Summit 2026 yenye kaulimbiu “𝙆𝙪𝙜𝙚𝙪𝙯𝙖 𝙃𝙖𝙩𝙪𝙖 𝙯𝙖 𝙏𝙖𝙗𝙞𝙖𝙣𝙘𝙝𝙞 𝙆𝙪𝙬𝙖 𝙁𝙪𝙧𝙨𝙖” inatarajiwa kuwakutanisha washiriki takribani 1,000 kutoka sekta mbalimbali kujadili na kuibua fursa za ubunifu, uwekezaji, ajira, ushirikiano na maendeleo endelevu zinazotokana na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ushirikiano kati ya NEMC na TGS unaendana na Mpango Mkakati wa NEMC pamoja na malengo ya Dira ya Tanzania ya 2050, hususan katika kujenga uchumi endelevu, thabiti, wa kibunifu na jumuishi unaozingatia fursa zinazotokana na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗬𝗔𝗞𝗨𝗧𝗔𝗡𝗔 𝗡𝗔 𝗪𝗔𝗔𝗡𝗗𝗔𝗔𝗝𝗜 𝗪𝗔 𝗧𝗔𝗡𝗭𝗔𝗡𝗜𝗔 𝗚𝗥𝗘𝗘𝗡 𝗦𝗨𝗠𝗠𝗜𝗧 𝟮𝟬𝟮𝟲

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa waandaaji wa Tanzania Green Summit (TGS), inayotarajiwa ...