Nyumbani

WAZIRI MASAUNI AWATAKA WADAU KUTUMIA SOKO LA KABONI KUANZISHA MIRADI YENYE TIJA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amewataka wadau wa maendeleo nchini kutumia Soko la Kaboni kuanzisha miradi inayoweza kufadhilika, mifumo inayotabirika na uwekezaji unaopimika.

Waziri Masauni ameyasema hayo Oktoba 22, 2026 Hyatt Regency akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania lililokuwa na kaulimbiu isemayo "Siku Moja, Soko Moja, Maono ya Pamoja" lililokusanya wadau mbalimbali wa maendeleo kujadili mambo mbalimbali yahusuyo biashara ya Kaboni.

"Jukwaa hili lisiishie kuwa mahali pa kubadilishana mawazo, liwe mwanzo wa ushirikiano unaozaa miradi inayofadhilika, mifumo inayotabirika na uwekezaji unaopimika." Amesema Waziri Masauni.

Aidha, Waziri Masauni ameongeza kwa kusema kuwa kila mdau aliyefika kwenye Jukwaa hilo atoke na hatua mahsusi: mwekezaji  akiwa na mradi wa kuwasilisha, taasisi ya umma ikiwa na fursa ya kutathmini, taasisi ya fedha ikiwa na bidhaa ya kufadhili, na NCMC ikiwa na orodha ya ahadi za kufuatilia.

"Nitaomba NCMC iniletee taarifa ya matokeo ya Jukwaa hili ndani ya siku thelathini. Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa mapato na manufaa yatokanayo na miradi yanaendana na Sheria, mikataba na masharti ya uidhinishaji, huku maslahi ya Taifa na ya jamii yakilindwa." Amesisitiza Waziri Masauni.

NEMC imeshiriki Jukwaa hilo ikiwa ni Taasisi inayosimamia masuala ya Mazingira nchini ambapo Watumishi kadhaa wameshiriki wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira, Dkt. Careen Kahangwa.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kujadili utekelezaji wa baj...