Nyumbani

NEMC YAKUTANA NA KAMATI MBILI ZA KUDUMU ZA BUNGE

📌Yawasilisha Masuala ya Usimamizi wa Taka ngumu na umuhimu wa kuanzisha Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  tarehe 21 Oktoba, 2026 Bungeni Dodoma, limekutana na Kamati mbili za Kudumu za Bunge, ambazo ni Kamati ya Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Maji na Mazingira, na kuwasilisha masuala ya usimamizi wa taka ngumu, fursa za kiuchumi zinazotokana na taka na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria yatakayowezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA).

Wasilisho hilo limeeleza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa taka ngumu ili kulinda afya ya jamii na mazingira, huku taka zikitambuliwa kama rasilimali zinazoweza kuzalisha fursa za kiuchumi kupitia urejelezaji na uchakataji. Aidha, kuanzishwa kwa NEMA kunalenga kuimarisha uwezo wa kisheria wa kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira, pamoja na kurahisisha michakato ya biashara na uwekezaji bila kuathiri matakwa ya kisheria ya utunzaji wa mazingira.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi alisema mabadiliko ya Sheria yanayopendekezwa yanalenga kuiwezesha Taasisi kuwa Mamlaka kamili inayoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwezesha biashara na uwekezaji na kukuza uchumi endelevu na rafiki kwa mazingira. Alifafanua kuwa mabadiliko hayo yanahusisha kubadilika kwa jina kutoka NEMC kwenda NEMA na kuimarisha vipengele vya kisheria ili Taasisi iwe mwezeshaji badala ya kikwazo kwa wawekezaji, hususan katika kutimiza masharti na kupata vibali vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria.

Kikao hicho, kilichohudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, Wajumbe wa Kamati pamoja na Menejimenti ya NEMC, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. John Kiswaga (Mb), na kujadili mapendekezo ya kuboresha mfumo wa Usimamizi wa Mazingira nchini kwa kuzingatia afya ya jamii, uwekezaji na maendeleo endelevu.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

NEMC YAKUTANA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kujadili utekelezaji wa baj...