Nyumbani

NEMC YASISITIZA UWEKEZAJI ENDELEVU UNAOZINGATIA UHIFADHI WA MAZINGIRA; MKUTANO WA USHIRIKIANO WA URUSI NA AFRIKA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika Mkutano wa “Russia–Africa Summit” pamoja na Jukwaa la Business to Business (B2B) ulioanza Oktoba 22 hadi 29, 2026 na kufunguliwa rasmi na Rais wa Urusi, Vladmir Putin katika jiji la Moscow nchini Urusi. Mkutano huo umezikutanisha nchi 48 za Afrika na wawekezaji kutoka Urusi kwa mazungumzo ya kibiashara na uwekezaji, ikiwemo kuingia ubia na Tanzania.

NEMC ilieleza nafasi yake kama taasisi inayosimamia uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini, huku ikitangaza fursa za uwekezaji katika sekta ya mazingira na kusisitiza umuhimu wa uwekezaji unaozingatia ulinzi wa mazingira, pamoja na kujenga mahusiano ya kibiashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Urusi. NEMC, kwa kushirikiana na TIB Development Bank na Jitegemee Holdings, ilishiriki kikao cha pamoja na Uralsib Bank nchini Urusi na kujadili juu ya miradi inayolenga kubadilisha taka kuwa nishati na nishati jadidifu.

Katika Mkutano huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba, aliwakilisha ujumbe wa Tanzania kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ujumbe huo ulihusu kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia na Urusi, hasa katika teknolojia ya kidijitali, nishati na madini, pamoja na kuvutia uwekezaji wa Urusi katika mbolea, madawa na elimu ya ufundi. Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana, hivyo uchumi wa kidijitali ni kipaumbele cha taifa, na Tanzania inatarajia kuendeleza ushirikiano na Urusi katika nyanja hizo.

Kwa ujumla, ushiriki wa NEMC katika kongamano hilo umeleta manufaa kwa taasisi, ikiwemo kupanua mtandao wa kitaasisi na ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya mazingira, kuimarisha uwezo wake wa kusimamia masuala ya mazingira nchini, na kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika utekelezaji wa sera za mazingira. Aidha, ushiriki huo umeimarisha nafasi ya NEMC kama taasisi muhimu katika kuvutia uwekezaji endelevu na kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania yanaenda sambamba na ulinzi wa mazingira kwa manufaa ya sasa na baadae.








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

𝐍𝐄𝐌𝐂 𝐘𝐀𝐍𝐆'𝐀𝐑𝐀 𝐊𝐖𝐄𝐍𝐘𝐄 𝐑𝐈𝐀𝐃𝐇𝐀 - 𝐒𝐇𝐈𝐌𝐌𝐔𝐓𝐀 𝟐𝟎𝟐𝟔

📌𝐘𝐚𝐭𝐢𝐧𝐠𝐚 𝐍𝐮𝐬𝐮 𝐟𝐚𝐢𝐧𝐚𝐥𝐢 𝐌𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐌𝐢𝐭𝐚 𝟏𝟎𝟎, 𝐌𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐯𝐢𝐣𝐢𝐭𝐢, 𝐦𝐛𝐢𝐨 𝐳𝐚 𝐦𝐚𝐠𝐮𝐧𝐢𝐚 𝐧𝐚 𝐟𝐚𝐢...