Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wake kuhusu Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), michakato ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba huo (COP), pamoja na nafasi ya NEMC katika kuendeleza vipaumbele vya kitaifa vya Tanzania kuhusu mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa mazingira, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama (COP31).
Mafunzo hayo yalijikita katika michakato muhimu ya UNFCCC, vipaumbele vya Tanzania kuelekea COP31, nafasi na majukumu ya NEMC katika mikutano ya COP, pamoja na fursa za ushiriki wa kimkakati katika majadiliano na maamuzi ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo, Bw. Fredrick Mulinda kutoka NEMC na Dkt. Sixbert Mwanga kutoka Shirika la Climate Action Network (CAN) Tanzania, waliwajengea uwezo watumishi kuhusu maeneo muhimu ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, vipaumbele vya kitaifa katika majadiliano pamoja na fursa zinazoweza kuwepo kwa maslahi yaTanzania. Aidha, wawezeshaji waliangazia mikakati ya kutumia fursa za upatikanaji wa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga mashirikiano na kuimarisha ushiriki wa kitaasisi katika kutekeleza vipaumbele vya taifa.
NEMC, ikiwa ni taasisi ya kitaifa yenye jukumu la kusimamia na kudhibiti masuala ya mazingira, na taasisi yenye ithibati ya kupata na kusimamia fedha kutoka Mifuko ya Kimataifa ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund (AF) na Green Climate Fund – GCF), ina nafasi muhimu katika kuhamasisha na kuratibu upatikanaji wa fedha za tabianchi, kuimarisha usimaizi wa mazingira na kusaidia jamii za Kitanzania kuongeza uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Usimamizi wa Mazingira, Dkt. Caren Kahangwa, aliwashukuru washiriki kwa ushiriki wao mzuri na kuwasisitiza kuendelea kujenga uelewa, kufuatilia maendeleo ya majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kujiandaa kikamilifu kwa ushiriki wenye tija katika mikutano ya COP unaokaribia kuanza.

.jpeg)

.jpeg)

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni