Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani tarehe 20 Septemba ya kila mwaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, akiwemo DEPO, limefanya usafi Hospitali ya Mwananyamala na maeneo mengine nchi nzima ambapo Kanda 13 zipo zikitoa huduma za Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira.
Zoezi hilo limehusisha watumishi wa NEMC, wawakilishi kutoka DEPO, pamoja na baadhi ya wananchi wa maeneo ya jirani, ambapo usafi mkubwa umefanyika katika mazingira ya hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuondoa taka, kufagia, na kusafisha mitaro ya maji taka.
Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, tarehe 20 Septemba.
Akizungumza katika zoezi hilo, Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwa na mazingira safi, salama na endelevu kwa afya na maendeleo ya Taifa.
"Siku hii si ya kusherehekea tu, bali ni ya kutafakari na kuchukua hatua. Mazingira safi ni msingi wa afya bora, ukiangalia taka zilizookotwa hapa nyingi ni za majumbani, kunamifuko ya plastiki, chupa, mabaki ya vyakula ambazo zingetakiwa kutenganishwa kutokea nyumbani. Tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema.
Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya zoezi hiloKwa upande wake, mwakilishi wa DEPO, Bw. Humphrey Milinga alieleza kuwa ushirikiano kati ya mashirika ya mazingira na Taasisi za afya ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inapata huduma katika mazingira rafiki na salama.
"Tumeona ni vyema kufanya usafi hospitalini kwani ni maeneo ya kuhudumia afya, na mazingira yake yanapokuwa safi, yanasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa," aliongeza.
Katika maadhimisho hayo, kanda mbalimbali za NEMC pia zilitekeleza shughuli za usafi katika maeneo yao husika, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya usafi inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jamii nzima katika kulinda mazingira.
Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, 20 Sepemba.Siku ya Usafi Duniani huadhimishwa duniani kote kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira, kuondoa taka, na kuelimisha jamii juu ya athari za uchafuzi wa mazingira.
NEMC imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye mazingira safi na salama kwa wote.
Picha ya pamoja ya watumishi wa NEMC, DEPO, Hospitali ya Mwananyamala na wakazi wa Mwananyamala mara baada ya zoezi la Usafi wa Mazingira ya Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu katika kuadhimisha siku ya Usafi Duniani.