Nyumbani

NEMC YASHIRIKI KONGAMANO LA UNESCO LA PROGRAMU YA BINADAMU NA HIFADHI HAI CHINA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki Kongamano la Dunia la Programu ya UNESCO ya Binadamu na Hifadhi Hai lililofanyika Jijini Hangzhou nchini China kuanzia tarehe 22-25 Septemba 2025.

Kwa upande wa NEMC Kongamano hilo limehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza Dkt. Immaculate Sware Semesi pamoja na Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema.

Wawakilishi wengine kutoka Tanzania katika kongamano hilo ni kutoka TANAPA

Kongamano hilo limelenga Kuimarisha ushirikiano wa Kimataifa, kupata maarifa na teknolojia mpya katika kusimamia na kuhifadhi Mazingira nchini, ni fursa katika uendelevu wa Hifadhi za Taifa, fursa za Kutangaza vivutio vya kitalii, kuimarisha Ushirikiano na Jamii, kuitangaza Tanzania kimataifa, kuvutia wawekezaji na kusaidia kufikia malengo ya Maendeleo nchini.


Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa pili kushoto) katika Ukumbi wa Kongamano hilo, kushoto kwake ni Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema pamoja na washiriki wengine wa Kongamano hilo lililofanyika Nchini China

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi (wa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Tafiti za Mazingira(NEMC) Dkt. Rose Sallema na mshiriki mwingine wa Kongamano hilo

Meneja Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema (wa katikati) na baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo.


NEMC NA TANAPA WAADHIMISHA SIKU YA FARU DUNIANI KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI- KILIMANJARO

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na TANAPA wameadhimisha Siku ya Faru Duniani ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Same mkoani Kilimanjaro Septemba 22,2025.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Afisa Mazingira Mwandamizi Bw. Francis Nyamhanga amezungumzia kuhusu umuhimu wa Faru kwenye mfumo wa Ikolojia.

"Kwenye mfumo wa Ikolojia Faru husaidia kufungua njia kwa kuvunja miti kwa ajili ya Wanyama wengine wadogo kuweza kupata malisho lakini pia hula mbegu za mimea mbalimbali hivyo kupitia kinyesi chao husaidia kusambaza mbegu katika mifumo Ikolojia na kinyesi hicho pia hurutubisha mifumo ikolojia bila kusahau wanachangia kukuza pato la Taifa kwani Faru ni kivutio cha utalii" amesema Bw. Francis.

 Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo na Afisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC Bw. Francis Nyamhanga wakiwa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomanzi Mkoani Kilimanjaro katika Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani

Afisa Uhifadhi wa TANAPA, Bw. Jackson Lyimo ameeleza namna wanavyowafikia Jamii kwa kutoa elimu ya Uhifadhi wa Faru.

"Hifadhi Ina programu maalumu inayofahamika kama Rafiki wa Faru ambayo inafikia Jamii kwa kuipa elimu ya jinsi ya Faru hawa walivyotoweka, walivyorejeshwa na jinsi wanavyolindwa na kuzalishwa katika Hifadhi hii. Hadi sasa tumefikia shule 120 na kuwafikia walimu na wanafunzi takribani 3,600 toka Julai 2022" amesema Mhifadhi Lyimo.

Katika kuadhimisha Siku hii pia wanafunzi kutoka shule mbalimbali wamefika katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kujifunza namna Uhifadhi wa Faru unavyofanyika. Maadhimisho ya Siku ya Faru Duniani hufanyika mnamo Septemba 22 kila mwaka kwa lengo la kuelimisha Umma kuhusiana na Uhifadhi wa Faru na kuwalinda dhidi ya ujangili.






NEMC YAADHIMISHA SIKU YA USAFI DUNIANI KWA KUFANYA USAFI HOSPITAL YA MWANANYAMALA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), katika kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani tarehe 20 Septemba ya kila mwaka kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, akiwemo DEPO, limefanya usafi Hospitali ya Mwananyamala na maeneo mengine nchi nzima ambapo Kanda 13 zipo zikitoa huduma za Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira.

Zoezi hilo limehusisha watumishi wa NEMC, wawakilishi kutoka DEPO, pamoja na baadhi ya wananchi wa maeneo ya jirani, ambapo usafi mkubwa umefanyika katika mazingira ya hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuondoa taka, kufagia, na kusafisha mitaro ya maji taka.

Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, tarehe 20 Septemba.

Akizungumza katika zoezi hilo, Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuwa na mazingira safi, salama na endelevu kwa afya na maendeleo ya Taifa.

"Siku hii si ya kusherehekea tu, bali ni ya kutafakari na kuchukua hatua. Mazingira safi ni msingi wa afya bora, ukiangalia taka zilizookotwa hapa nyingi ni za majumbani, kunamifuko ya plastiki, chupa, mabaki ya vyakula ambazo zingetakiwa kutenganishwa kutokea nyumbani. Tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho," alisema.

Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki Kaskazini, Bi. Glory Kombe akizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya zoezi hilo

Kwa upande wake, mwakilishi wa DEPO, Bw. Humphrey Milinga alieleza kuwa ushirikiano kati ya mashirika ya mazingira na Taasisi za afya ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inapata huduma katika mazingira rafiki na salama.

"Tumeona ni vyema kufanya usafi hospitalini kwani ni maeneo ya kuhudumia afya, na mazingira yake yanapokuwa safi, yanasaidia kuzuia maambukizi ya magonjwa," aliongeza.

Katika maadhimisho hayo, kanda mbalimbali za NEMC pia zilitekeleza shughuli za usafi katika maeneo yao husika, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya usafi inayolenga kuhamasisha ushiriki wa jamii nzima katika kulinda mazingira.

Watumishi wa NEMC, DEPO na baadhi ya wakazi wa Mwananyamala wakifanya Usafi kwenye Mazingira ya Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala katika Maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani, 20 Sepemba.

Siku ya Usafi Duniani huadhimishwa duniani kote kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira, kuondoa taka, na kuelimisha jamii juu ya athari za uchafuzi wa mazingira.

NEMC imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi yenye mazingira safi na salama kwa wote.

Picha ya pamoja ya watumishi wa NEMC, DEPO, Hospitali ya Mwananyamala na wakazi wa Mwananyamala mara baada ya zoezi la Usafi wa Mazingira ya Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu katika kuadhimisha siku ya Usafi Duniani.

NEMC YAINGIA MTAANI KIDIGITALI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Mkoa wa Dar es salaam  linaendesha zoezi maalumu la Ukaguzi wa Mazingira kwa Miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mfumo maalumu wa kidigitali uitwao 'Mazingira App'.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti amesema zoezi hilo litadumu kwa wiki nne na litahusisha kaguzi za Mazingira kwenye miradi ya maendeleo hususani kuangalia uzingatiaji wa matakwa ya Usimamizi wa Mazingira kama vile usimamizi wa taka, matumizi sahihi ya ardhi pamoja na  uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti (wa kwanza kushoto) akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu zoezi maalumu la Ukaguzi wa Mazingira kwa Miradi yote ya maendeleo kwa kutumia mfumo maalumu wa kidigitali uitwao 'Mazingira App'.

Ameongeza kwa kutumia mfumo wa Mazingira App pia utawawezesha kuchunguza uzingatiaji wa Sheria zinazohusu afya ya jamii, usalama wa kazi na mipango miji  ambazo kwa kutokutekelezwa kwake huchangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi au uharibifu wa mazingira.

Aidha Bw. Jamal Baruti amesema ushirikiano na uongozi wa Jiji la Dar es salaam umelenga kuongeza uelewa na ufanisi kwa maafisa mazingira kuhusu Usimamizi hafifu wa taka ngumu, changamoto ya taka za plastiki, uharibifu wa Mazingira kutokana na uchimbaji holela wa kwenye mito na mabonde na matumizi holela ya ardhi kinyume na taratibu za mipangomiji.

Kwa upande wake Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki (NEMC) Bi. Glory Kombe alipozungumza amewataka Viongozi wa Halmashauri na Serikali za mitaa kutoa ushirikiano wakati wote wa zoezi hili ili kufikia tija tarajiwa kwa maendeleo endelevu ya Mazingira nchini.

Kadhalika Meneja Glory Kombe amefafanua  kuwa jukumu la Halmashauri na Mamlaka za Serikali za mitaa ni kuhakikisha Miradi ya maendeleo inazingatia taratibu za Mazingira ikiwemo ufanyikaji wa Tathmini ya Mazingira na Jamii kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Mazingira na Kanuni zake na kusimamia usafi wa Mazingira kwa ujumla pamoja na kuwataka maofisa Mazingira na Kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.

Meneja Kanda ya Kaskazini Mashariki Bi. Glory Kombe (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huo
Meneja Uzingatiaji wa Sheria (NEMC)Bw. Hamadi Taimuru (wa kulia) akichangia mada katika Mkutano huo

 NEMC imeanzisha mfumo huo wa Mazingira app' ambao ni wa kidigitali ili kurahisisha na kuongeza  ufanisi katika ukusanyaji na uhifadhi wa Taarifa za Miradi pamoja na usajili wa Miradi mipya ambapo zitachangia Baraza na Serikali kupanga na kusimamia Miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.



NEMC YAKAGUA MGODI WA 'URANIUM' MKOANI RUVUMA UNAOTARAJIWA KUANZA 2026

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilifika na kukagua Mgodi wa madini aina ya Uranium uliopo katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambao ulikuwa katika Uchimbaji mdogo wa majaribio huku Uchimbaji mkubwa ukitarajiwa kuanza mwaka 2026.

NEMC ilifika na kufanya Ukaguzi katika Mgodi huo na kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha shughuli za Uchimbaji katika Mgodi huo haziathiri Mazingira, Viumbe hai na wakazi wa jirani na Mgodi huo ikiwa ni agizo la Serikali.

Awali NEMC ilianza kwa kutoa elimu ya Mazingira na Afya kwa wakazi wa vijiji vilivyo karibu na Mgodi huo ili kuwajengea uelewa kuhusiana na madini ya 'Uranium' jinsi yanavyoweza kuhatarisha afya na Mazingira ikiwa hayata chakatwa na kudhibitiwa kwa umakini.

Akizungumza katika Ukaguzi huo Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Bw. Jamal Baruti alisema NEMC ilifika katika Mgodi huo kufanya Ukaguzi ili kutathmini ikiwa wawekezaji katika Mgodi huo wamekidhi na kuzingatia miondombinu ya Mazingira ambayo haita haribu Mazingira, kuhatarisha usalama wa wakazi na wafanyakazi katika Mgodi huo kabla Uchimbaji mkubwa haujaanza.

Timu ya wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Kampuni ya Uchimbaji ya MANTRA wakikagua moja ya mlima wenye madini ya  'Urunium' wakati wa ukaguzi wa Mgodi huo. Wa pili kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti.

Aidha Bw. Baruti alieleza kuwa Mradi wa Mgodi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani elfu 27 kwa siku na utakuwa ni Mradi mkubwa wa Uchimbaji madini nchini ukilinganisha na Miradi mingine nchini Tanzania.

Aliongeza kuwa Tanzania  itakuwa nchi ya nne ya uzalishaji wa madini ya 'Uranium' Duniani huku akiwasisitiza wawekezaji na wananchi kuzingatia uhifadhi Mazingira na si tu kuangalia manufaa ya Mgodi huo.

Meneja wa Kampuni ya MANTRA Bw. Beria Vorster akitoa maelezo kwa wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC wakati wa ukaguzi wa mtambo wa kuchenjua madini ya 'Urunium' ikiwa ni sehemu ya Ukaguzi wa Mgodi huo.

Kwa upande wake Meneja Kanda ya Kusini (NEMC) Bw. Boniface Guni alisema ziara hiyo iliwasaidia NEMC kupata picha ya Mradi huo ambayo itawasaidia kusimamia Mpango wa Usimamizi wa Mazingira na jamii ipasavyo.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buchushu Kijiji cha Iguseka Bw. Omary Rashid aliishukuru NEMC kwa kuwapatia elimu hiyo adhimu ya Mazingira wakazi wa vijiji hivyo ambayo ni muhimu katika utunzaji wa Mazingira na Afya ya binadamu.

Timu ya wataalamu wa Mazingira kutoka NEMC na Kampuni ya Uchimbaji ya MANTRA wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ukaguzi wa Mgodi wa madini ya 'Urunium' katika eneo la Mto Mkuju Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma. Wa katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti na kushoto kwake ni Meneja wa Mradi Bw. Beria Vorster

RUVUMA YAFIKIWA ELIMU YA MAZINGIRA- MADINI YA URANIUM

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitoa elimu ya kimazingira na afya kwa vijiji viwili vya Mtonya na Mandela-Likuyu katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma kufuatia Mradi wa Uchimbaji wa Madini aina ya 'Uranium'  ulitarajiwa kuanza katika mgodi ulio karibu na vijiji hivyo.

Elimu hiyo ilitolewa kwa wananchi kuanzia 8-9 Septemba, 2025 kwa vijiji hivyo huku ikifuatiwa na ukaguzi uliofanyika katika mgodi huo ambapo ilikuwa hatua ya awali ya kuelimisha jamii na wawekezaji kabla ya Mradi huo kuanza ambapo  ni maagizo yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha jamii inatambua uwepo wa Mradi huo na kuhakikisha  jamii haiathiriki na Mradi huo.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti akizungumza wakati wa utoaji wa elimu ya ya Mazingira na Afya kwa wanakijiji wa Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Meneja Kanda ya Kusini NEMC Bw. Boniface Guni akiwasilisha mada kwa wanakijiji wa Mandela-Likuyu Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wakati wa utoaji wa elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Meneja Kanda ya Kusini NEMC Bw. Boniface Guni akiwasilisha mada kwa wanakijiji wa Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wakati wa utoaji wa elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

Akizungumza katika utoaji wa elimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti aliutaka Uongozi wa vijiji hivyo kutumia Kamati za Mazingira na kushirikiana na Serikali kuendelea kuelimisha jamii juu ya maswala ya Mazingira na Afya ya jamii yanayoweza kusababishwa na Mradi huo.

Kwa upande wake, Meneja Kanda ya Kusini (NEMC) Bw. Boniface Guni aliwataka wakazi wa vijiji hivyo kuchangamkia fursa za ajira katika Mradi huo huku wakizingatia ulinzi wa Afya zao na Mazingira.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria NEMC Bw. Jamal Baruti alisema NEMC itaendelea na ufuatiliaji wa maswala ya kimazingira kwa kushirikiana na Taasisi nyingine huku akiitaka Kampuni ya Mantra TZ LTD ya Uchimbaji katika mgodi huo kutambua haki za wakazi wa vijiji hivyo na kuchangia shughuli za maendeleo ya wakazi wa vijiji hivyo kama manufaa ya Mradi huo.

Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bw. Jamal Baruti (wa tatu kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanakijiji na Viongozi wa Kijiji cha Mtonya Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma mara baada ya kuwapatia elimu ya Mazingira na Afya kufuatia Uchimbaji mkubwa wa madini ya 'Urunium' utakaoanza mwakani 2026

NEMC YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI KUSINI

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Uwekezaji Kusini (Kusini International Trade Fair and Festival) yanayofanyika kuanzia tarehe 14-21, Septemba, 2025 katika eneo la fukwe ya Matema Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya.

Maonesho hayo yamelenga kutangaza fursa za kibiashara zilizopo katika mikoa ya Kusini ambapo NEMC inatumia fursa hiyo kutoa elimu ya Mazingira.


Maafisa Mazingira wa NEMC Kanda ya Kusini wakitoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda lao katika maonesho hayo.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...