Nyumbani

𝗞𝗔𝗠𝗜𝗦𝗛𝗡𝗔 𝗔𝗜𝗣𝗢𝗡𝗚𝗘𝗭𝗔 𝗡𝗘𝗠𝗖 𝗞𝗪𝗔 𝗨𝗔𝗗𝗜𝗟𝗜𝗙𝗨 𝗞𝗔𝗧𝗜𝗞𝗔 𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗪𝗔 𝗨𝗠𝗠𝗔

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (aliyesimama) akizungumza wakati wa kikao na watumishi wa NEMC alipozuru Ofisi za Baraza 23 Oktoba, 2025 ikiwa ni ziara yake ya kikazi

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro amelipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)  kwa kuendelea kuonesha uadilifu na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini.

Akizungumza leo 23 Oktoba, 2025 jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi  ofisi za Baraza  Dkt. Laurean Ndumbaro amesema uadilifu uliooneshwa na Baraza hilo ni mfano wa kuigwa na Taasisi nyingine za Umma katika kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya kazi.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akizungumza wakati wa kikao hicho kilichokuwatanisha watumishi wa Baraza na Ugeni kutoka Tume ya Utumishi wa Umma ukiongozwa na Kamishna Dkt. Laurean Ndumbaro. 

Amesisitiza kuwa uadilifu ndio nguzo kuu ya utumishi wa umma na ndio msingi wa kuaminika kwa Serikali mbele ya wananchi.

Ameongeza kuwa mafanikio ya NEMC katika utekelezaji wa miradi ya kimazingira pamoja na usimamizi wa Sheria na Kanuni za Mazingira ni ushahidi kwamba viongozi na watumishi wake wameweka maslahi ya Taifa mbele kuliko  maslahi binafsi.

Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa akizungumza wakati wa kikao hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi amemshukuru  Kamishna kwa Tathmini hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na ubunifu zaidi kwani pongezi hizo ni chachu ya kuongeza ari ya watumishi kulinda rasilimali za Taifa na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika ziara yake Kamishna Dkt. Ndumbaro ameambatana na wataalamu wengine akiwemo Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti kutoka Tume ya Utumishi wa Umma Ndugu Peleleja Masesa.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Immaculate Sware Semesi akimkabidhi zawadi Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Dkt. Laurean Ndumbaro mara baada ya kikao hicho.




   Baadhi ya watumishi wa Baraza wakifuatilia kikao hicho


NEMC NA MWAKILISHI KUTOKA ULAYA WAJADILI NA MJUMBE KUTOKA ULAYA USIMAMIZI WA MAZINGIRA KATIKA SEKTA YA MADINI


Mkurugenzi wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii Bi. Lilian Lukambuzi (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na muwakilishi wa ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Meneja wa Programu (Utawala wa kiuchumi) Bw. Sebastian Schaber. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Meneja wa Mapitio ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (NEMC) Mha. Luhuvilo Mwamila. Wa kwanza kulia ni Meneja Usajili wa Wataalam elekezi wa Mazingira (NEMC) Bi. Edika Masisi. 

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na muwakilishi wa ujumbe wa Umoja wa nchi za Ulaya (EU) nchini Tanzania na kujadili namna Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii zinavyofanyika kwa Tanzania na jinsi wanavyoweza kushirikiana na Baraza hususani katika masuala ya kimazingira kwa upande wa Sekta ya madini hasa madini muhimu (Critical Minerals) 

Kikao hiki kilijadili miongozo iliyopo  na kuainisha maeneo yanayohitaji usaidizi wao ili kuwezesha uzingatiaji wa Sheria kwa miradi ya madini inayowekezwa nchini.


NEMC NA IUCN WAJADILI NAMNA YA KUKABILIANA NA UCHAFUZI WA PLASTIKI UKANDA WA BAHARI

Meneja wa Tafiti za Mazingira (NEMC) Dkt. Rose Sallema akizungumza wakati wa kikao kazi hicho

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN) limefanya kikao kazi kujadili namna bora ya kukabiliana na tatizo la uchafuzi unaotokana na taka za plastiki katika ukanda wa bahari. Kikao hicho kimekusudia kuweka mikakati endelevu ya kudhibiti matumizi na utupaji holela wa plastiki, pamoja na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya baharini kwa manufaa ya viumbe vya majini na ustawi wa binadamu kwa ujumla.






NEMC YAWANOA MAAFISA FORODHA KIGOMA - ELIMU YA USIMAMIZI WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa Forodha katika kituo cha mpakani cha Kigoma, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa programu ya kujenga uelewa kuhusu usimamizi wa bidhaa hatarishi kwa mazingira zinazovuka mipaka.


Akifungua mafunzo hayo Oktoba 20, 2025 katika ofisi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Meneja wa Bandari Kigoma Bw. Edward Mabula amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa taasisi mbalimbali katika kulinda mazingira na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizo rafiki kwa mazingira.

“Ushirikiano baina ya taasisi kama NEMC, TRA, TPA, TBS, TMDA na wadau wengine ni muhimu sana katika kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini haziwezi kuathiri mazingira yetu,” amesema Bw. Mabula.


Kwa upande wa wawakilishi kutoka NEMC, wameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Baraza katika kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191.

Aidha, wamefafanua kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Maafisa Forodha ili waweze kutambua mapema bidhaa hatarishi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Mafunzo hayo ni mwendelezo wa programu inayoendeshwa na NEMC katika vituo vya mipakani vya Mtukula, Rusumo, Kigoma na Tunduma, ikilenga kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia au kutoka nchini zinakidhi matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Washiriki wa mafunzo ya Usimamizi wa Bidhaa hatarishi mipakani wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mafunzo hayo





NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA TEKNOLOJIA ZA UREJESHAJI MAZINGIRA NCHINI AUSTRIA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki kikao cha kutathmini mapungufu na changamoto za teknolojia za kimazingira zinazotumika kwenye kurejesha mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa (remediation technologies).

Afisa Mazingira Mwandamizi Bi. Kuruthumu Shushu (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Kikao hicho kilifanyika katika makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Nyuklia (IAEA) yaliyopo jijini Vienna, Austria kuanzia tarehe 13-17 Oktoba, 2025.

Lengo la kikao ni kukutanisha wawakilishi kutoka nchi mbalimbali wanaohusika na Udhibiti na Tafiti katika Sekta ya Nishati ya nyuklia ili kujadili njia bora za urejeshaji wa mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa.

Njia mbalimbali za urejeshaji wa mazingira zilijadiliwa na nchi wanachama pamoja na mapungufu na changamoto zake na kujifunza njia bora inayoweza kutekelezwa na nchi husika.

Uwasilishaji wa mada ukifanyika katika kikao cha kutathmini mapungufu na changamoto za teknolojia za kimazingira zinazotumika kwenye kurejesha mazingira yaliyoharibiwa au kuchafuliwa (remediation technologies) kilichofanyika nchini Austria 

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA KIMATAIFA WA TAKA ZA KIELEKTRONIKI NCHINI KENYA

Baraza la Taifa la Hifadhi  na usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kurugenzi ya Utekelezajia na Uzingatiaji wa Sheria limeshiriki Mkutano wa tano wa Kimataifa unaohusu masuala ya taka za kielektroniki uliofanyika kuanzia tarehe 16 na 17 Oktoba, 2025 Mombasa, nchini Kenya.

Mkutano huo umewaleta pamoja  wadau kutoka Serikalini, wadau wa Maendeleo, wataalamu, Sekta binafsi pamoja na asasi za kiraia ili kujadili kwa pamoja masuala yanahusu taka za kielektroniki.

Meneja Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akiwasilisha mada katika Mkutano huo

Katika mkutano huo NEMC ilishiriki katika kutoa neno la ukaribisho pamoja na kusisitiza wadau kutumia jukwaa hilo la majadiliano vizuri ili  kutatua changamoto na kuibua fursa ambazo zitaleta tija katika kuhifadhi mazingira, kuongeza ajira na kukuza uchumi rejeshi.

 

Meneja Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akiwasilisha mada katika Mkutano huo

"Lengo mahususi la mkutano huo ni kuoanisha Sera, Sheria, na mifumo ya Usimamizi wa taka hizo. Kujadili ukuaji wa teknolojia unaoenda sambamba na ongezeko kubwa la uzalishaji wa taka za kielektroniki.

Aidha, Uwekezaji, fursa na mbinu mbalimbali za uchakataji wa taka hizo pia ni eneo lililojadili na wadau.

Meneja Utekelezaji wa Sheria (NEMC) Bi. Amina Kibola akifuatilia uwasilishaji mada katika Mkutano huo, kulia kwake ni Mhandisi Bi. Beatitude Sizya 

Mkutano pia umeangazia  mitazamo mipya ya nchi  za Afrika na  jinsi ya kushughulikia changamoto zinazosababishwa na ongezeko kubwa la taka za kielektroniki, huku ikibainisha fursa za kuendeleza ubunifu, kuimarisha utawala, na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika juhudi za kusimamia taka za kielectronia  kwa njia endelevu."

    Uwasilishaji wa Mada ukiendelea  katika Mkutano huo 

Timu ya NEMC iliyoshiriki Mkutano huo ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano huo

NEMC YAWAFIKIA MAAFISA WA FORODHA MIPAKANI -ELIMU YA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kupitia Mradi wa kujenga uwezo katika Usimamizi wa Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira (EMA), limeanza kutoa mafunzo kwa maafisa forodha waliopo mipakani, taasisi, wizara, idara pamoja na vyombo vya serikali kuhusu usimamizi wa bidhaa hatarishi kwa mazingira zinazopita mipakani.

Mafunzo hayo yamezinduliwa Oktoba 15, 2025 katika ofisi za Forodha Mtukula na yanatarajiwa kufanyika katika mipaka ya Rusumo, Kigoma na Tunduma kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wa watendaji wa serikali katika kusimamia utekelezaji wa Sheria na taratibu za mazingira kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini.

Afisa Mazingira Mkuu (NEMC) ambaye ndiye Mratibu wa Mradi EMA, Bw. Paul Kalokola akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi huo, Bw. Paul Kalokola ambaye pia ni Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC, amewataka washiriki kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria za mazingira na kuhakikisha bidhaa zote zinazovuka mipaka zinakidhi matakwa ya kisheria.

“Ni wajibu wa maafisa wote wanaohusika na usimamizi wa mipaka kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia au kutoka nchini hazina athari hasi kwa mazingira. Utekelezaji sahihi wa Sheria na Kanuni za mazingira utasaidia kulinda afya za wananchi na kudhibiti taka hatarishi zinazoweza kuathiri mfumo wa ikolojia,” alisema Bw. Kalokola.

Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC Bw. Fredrick Mulinda akiwasilisha mada katika mafunzo hayo

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mfawidhi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) – Mtukula, Bw. Elpidius Bigilwamungu, ameishukuru NEMC kwa kutoa mafunzo hayo muhimu, akisisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza ufanisi katika utambuzi na udhibiti wa bidhaa hatarishi mipakani.

Katika mafunzo hayo, wataalamu kutoka NEMC wamewasilisha mada mbalimbali zikiwemo Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Kudhibiti Taka Hatarishi, Mikataba na Miongozo ya Kimataifa ya Usimamizi wa Mazingira, Masuala ya Sera za Mazingira pamoja na Matumizi Salama ya Zebaki.

Baadhi ya maafisa wa NEMC waliohusika katika utoaji wa mafunzo kwa maafisa Forodha wa mipakani kupitia Mradi wa EMA  

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kupitia NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) katika kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) unafanyika kwa weledi, ushirikiano na uwajibikaji, hasa katika maeneo ya mipakani ambayo ni lango kuu la bidhaa kuingia nchini.

Afisa Mazingira Mkuu (NEMC) ambaye ndiye Mratibu wa Mradi EMA, Bw. Paul Kalokola akiwasilisha mada katika mafunzo hayo.

NEMC YASHIRIKI MKUTANO WA SABA WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linashiriki Mkutano wa Saba (07) wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (07th Unit...