Nyumbani

KATIBU MKUU DR. RICHARD MUYUNGI AKUTANA NA MENEJIMENTI YA NEMC

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo amekutana na Menejimenti ya Baraza kwa lengo la kujitambulisha na kujionea utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo.



Katika kikao kilichohusisha pia Mameneja wa Kanda 13 nchi nzima kiliwasilisha taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Baraza, ikiwemo mafanikio yaliyofikiwa, changamoto za mazingira zinazojitokeza pamoja na hali ya mazingira kwa ujumla. 

Aidha, ziliainishwa pia fursa za kiuchumi zilizopo katika sekta ya mazingira  hususani eneo la urejelezaji wa taka zinazoweza kuvutia uwekezaji na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi endelevu wa mazingira.

Dkt. Richard Muyungi alipozungumza  ameishukuru NEMC kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhifadhi na kusimamia mazingira ikiwa ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa Sheria

Amesisitiza umuhimu wa Baraza  kuzingatia mabadiliko ya sayansi, teknolojia na mahitaji ya sasa ya jamii ili kuendana na ulimwengu wa kidigitali katika kufikisha elimu ya  Mazingira kwa jamii.

Katika maelekezo yake, Dkt. Muyungi ameitaka NEMC kuanzisha kitengo cha Ubunifu  kitakachokuwa na jukumu la kubuni na kuibua mawazo mapya yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mazingira, ikiwemo kutatua changamoto zinazojitokeza kwa njia bunifu na endelevu.

Vilevile amesisitiza kuzingatiwa kwa weledi katika uchakataji na usimamizi wa miradi ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na misingi ya uhifadhi wa mazingira.

Sambamba na hilo, aliagiza kuimarishwa kwa matumizi ya teknolojia ya kisasa itakayowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na za haraka za mazingira, jambo litakalosaidia katika kufanya maamuzi yenye tija na kulinda rasilimali za taifa.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Dkt. Muyungi kufika na kuzungumza na Menejimenti ya NEMC tangu kuteuliwa kwake kushika wadhifa wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na imeelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano, mawasiliano na uratibu wa masuala ya mazingira nchini.

NEMC YAUNGA MKONO JITIHADA ZA MHESHIMIWA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN KATIKA KUTUNZA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhifadhi na kusimamia mazingira kwa kushiriki zoezi la upandaji miti katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa tarehe 27 Januari.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Mheshimiwa Rais alipanda mti kama ishara ya kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni utekelezaji wa kaulimbiu isemayo “Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti.”
Kupitia kanda zake 13 nchini kote, NEMC imeshirikiana na wizara, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia pamoja na kamati za mazingira kushiriki katika zoezi la upandaji miti katika maeneo mbalimbali yakiwemo shuleni, zahanati na katika masoko.


Akizungumza katika hafla hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Mkurugenzi wa  Utawala na Fedha Bw. Dickson Mjinja alieleza umuhimu wa kupanda miti kama njia mojawapo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi huku akisisitiza kuwa miti ina mchango mkubwa katika kuhifadhi ikolojia na kuboresha maisha ya binadamu.
Kwa upande wake, Meneja wa NEMC Kanda ya Ilala, Bi. Abella Muyungi, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhifadhi mazingira nchini kwa vitendo, akisisitiza kuwa jukumu la uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja.

NEMC imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za Serikali za awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Zoezi la upandaji miti Kata ya Ilala viwanja vya msikate tamaa limeratibiwa na NEMC na Balozi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Grit Godfrey.



Akifafanua katika kikao hicho, Meneja wa Kanda ya Ilala, Bi. Abella Muyungi, alisema kuwa NEMC itaendelea kushirikiana kwa karibu na jamii na wadau wa mazingira katika kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya mazingira, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za mazingira kwa ajili ya kulinda afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.

Kupitia kikao hicho, NEMC ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na wadau wa mazingira katika kulinda na kusimamia mazingira kwa maendeleo endelevu, huku ikiahidi kuendelea kutoa elimu na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. 








Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Mhandisi Mwanasha Tumbo akipanda mti, kuadhimisha siku ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan

 "Uzalendo ni kutunza mazingira, shiriki kupanda miti "





NEMC KANDA YA ILALA YAENDESHA KIKAO CHA MASIKILIZANO NA WADAU WA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupitia Kanda ya Ilala limeendesha kikao cha masikilizano na wadau wa mazingira tarehe 21 Januari, 2026 katika Ukumbi wa Uhasibu, Ofisi za NEMC Mikocheni jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya mazingira kutoka kwa jamii zinazozunguka Kanda hiyo pamoja na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya mazingira na utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.

Katika kikao hicho, NEMC ilisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na wadau wa mazingira katika kulinda na kusimamia mazingira, kuhimiza wananchi kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za mazingira, na kuahidi kuendelea kutoa elimu ya mazingira pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa maendeleo endelevu na ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.




NEMC YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU KUIMARISHA USAFI WA MAZINGIRA JIJINI DODOMA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuonesha dhamira yake katika kuimarisha usafi wa mazingira kwa kushiriki kikao kazi cha wadau kilicholenga kutathmini utekelezaji wa afua mbalimbali za usafi wa mazingira kilichofanyika Januari 19, 2026 katika jiji la Dodoma.

Kikao hicho, kilichoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa safi, salama na lenye mazingira bora yanayochangia ustawi wa wananchi na maendeleo ya jiji kwa ujumla.

Akitoa mada ya ufunguzi, Meneja wa NEMC Kanda ya Kati, Bw. Novatus Mushi, aliwasilisha juhudi na mikakati inayotekelezwa na Baraza katika kuimarisha usafi wa mazingira Jijini Dodoma. Katika wasilisho lake, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, mamlaka za Serikali za mitaa na wadau wengine wa mazingira ili kufanikisha utekelezaji endelevu wa afua hizo.

Katika kikao hicho, wadau mbalimbali waliwasilisha taarifa na mada zinazohusu utekelezaji wa afua za usafi wa mazingira kwa kuzingatia majukumu yao ya kisheria na kiutendaji. Majadiliano hayo yaliibua mapendekezo muhimu yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa shughuli za usafi wa mazingira pamoja na kuimarisha uratibu na uwajibikaji wa wadau husika.

Sambamba na hilo, kikao hicho kilibainisha mikakati ya pamoja itakayotekelezwa kwa ushirikiano wa wadau wa mazingira, kwa lengo la kuimarisha na kudumisha usafi wa mazingira kwa namna endelevu katika Jiji la Dodoma.

Wadau wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), TANROADS, TARURA, LATRA pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

NEMC YAWALETA PAMOJA WATUMISHI WAKE KUJIPANGA KWA MWAKA 2026

 Ni katika kufanya tathmini na kuimarisha umoja. 

Watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Makao Makuu na kutoka kanda zote 13 nchini, wamekutana katika eneo la Ndotopolepole, Wilaya ya Bagamoyo, katika hafla maalum iliyolenga kuimarisha mshikamano, kujengeana uelewa, kufanya tathmini fupi ya utendaji kazi na kufurahi pamoja, ikiwa pia ni sehemu ya kufunga mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Immaculate Sware Semesi, amewataka watumishi wa Baraza kudumisha umoja na mshikamano katika utendaji kazi (team building), kufanya kazi kwa bidii na kuongeza nidhamu pamoja na unadhifu wa kazi, kama nguzo muhimu za kufanikisha maono na dira ya Taasisi katika mwaka 2026.

Dkt. Semesi ameongeza kuwa katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi, NEMC imejipanga kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidigitali, ambapo tayari baadhi ya mifumo ya ufuatiliaji wa mazingira imeanza kutumika, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika kazi.

Hafla hiyo pia imehusisha utoaji wa zawadi kwa watumishi walioonesha utendaji kazi mzuri na bidii, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ari, nidhamu na ushindani chanya mahali pa kazi.

Akitoa pongezi kwa wafanyakazi waliofanya vizuri, Dkt. Semesi aliipongeza menejimenti na watumishi wote wa NEMC kwa ujumla, na kuwasihi kuongeza bidii, ubunifu na ari mpya katika kutekeleza majukumu yao kwa mwaka 2026.

Aidha, hafla hiyo ilipambwa na michezo mbalimbali ya kujenga ushirikiano, mshikamano na moyo wa kutokata tamaa katika kazi, ambapo washindi walitunukiwa zawadi kama motisha.





















NEMC YASHIRIKI UTEKETEZAJI WA VIELELEZO VYA DAWA ZA KULEVYA MKOANI MTWARA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini tarehe 15 Novemba 2025 lilishiriki kusimamia na kushuhudia Uteketezaji wa vielelezo mbalimbali vya Mahakama Kanda ya Kusini ambavyo ni madawa ya kulevya vyenye Kilogramu 73. Vielelezo hivyo viliteketezwa katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Mkoani Mtwara

NEMC YATAMBUA USHIRIKIANO KATI YAKE NA JESHI LA POLISI

Yashiriki mahafali ya kumi ya programu za vyuo vya polisi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetambua mchango wa ...