Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuanzia Machi 9 hadi 16 linafanya ufuatiliaji katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Mlimba, Kilolo na Mafinga kwa lengo la kutathmini mafanikio ya Mradi wa Kihansi ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na ustawi wa jamii.
Mradi huo ulitekelezwa kuanzia mwaka 2001 hadi 2019 kupitia awamu tatu ambazo ni Lower Kihansi Environmental Management Project (LKEMP I na II) pamoja na Kihansi Catchment Conservation Management Project (KCCMP). Miradi hiyo ililenga kuimarisha uhifadhi wa baioanuai katika bonde la Kihansi pamoja na kulinda vyanzo vya maji.
Kupitia miradi hiyo, wananchi walipewa elimu ya uhifadhi wa mazingira na kuwezeshwa kufanya shughuli za kilimo nje ya vyanzo vya maji ili kupunguza uharibifu wa mazingira. Miradi hiyo ilitekelezwa chini ya uratibu na usimamizi wa NEMC kwa kushirikiana na taasisi za utafiti na wadau wengine.
Aidha, wananchi wa Halmashauri hizo waliwezeshwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kupitia vikundi, ikiwemo kilimo cha mpunga, kilimo cha miti, ufugaji wa nyuki na ufugaji wa samaki. Hatua hiyo imechangia kuongeza kipato na kuboresha ustawi wa kaya nyingi katika maeneo hayo.
Kutokana na uwezeshaji huo, baadhi ya wanufaika wamefanikiwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto, kuongeza ukubwa wa mashamba ya kilimo pamoja na kumiliki mifugo, jambo ambalo limeimarisha ustawi wa familia zao na jamii kwa ujumla.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bw. Philiscacius Shaban Masongela, ameishukuru NEMC kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya uhifadhi na uwezeshaji wa kiuchumi. “Kupitia mradi huu nimeweza kuongeza kipato, kujenga nyumba nzuri, kukuza shamba la mpunga na kumiliki mifugo. Hakika mradi huu umeleta mabadiliko chanya katika maisha yetu,” amesema Bw. Masongela.
Naye Bi. Pudensiana Valentine Chagawe kutoka Kikundi cha Nguvu Kazi katika Kijiji cha Chita, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, amesema elimu ya shamba darasa aliyopatiwa kupitia mradi huo imemwezesha kutumia mbinu za kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa mazao. “Awali nilikuwa napata takribani debe 30 (magunia matatu) za mpunga katika nusu heka, lakini baada ya kupata mafunzo ya shamba darasa na kutumia mbinu bora za kilimo, uzalishaji umeongezeka hadi kufikia debe 180 (magunia 18). Hii imenisaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia yangu,” amesema Bi. Chagawe.
Timu ya NEMC imewapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kuendelea kutumia maarifa na ujuzi walioupata kupitia Mradi wa Kihansi katika kuboresha shughuli zao za kiuchumi, kuinua vipato vya familia zao hiki wakitunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.