Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuimarisha uwezo wake katika masuala ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (Environmental, Social and Governance – ESG) pamoja na uripoti wa uendelevu, kupitia mafunzo ya siku tano yaliyotolewa na KPMG kuanzia tarehe 3 hadi 7 Agosti 2026 katika Ofisi ya Kanda ya Temeke ya NEMC, Dar es Salaam.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango endelevu wa Baraza wa kuimarisha mifumo na kanuni za ESG na kuweka uripoti wa uendelevu kuwa sehemu ya utendaji wa kitaasisi. Mpango huo unahusisha maandalizi ya Sera ya ESG, Mfumo wa ESG, pamoja na Ripoti ya Uendelevu ya Baraza kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa kuzingatia vipaumbele vya kitaifa na mifumo ya kimataifa inayotambulika katika uripoti wa uendelevu.
Katika mafunzo hayo, maafisa walioteuliwa kuwa Mabingwa wa ESG na Uripoti wa Uendelevu (ESG & Sustainability Reporting Champions) walipata uelewa na ujuzi wa vitendo kuhusu misingi ya ESG, mifumo ya uripoti wa uendelevu, tathmini ya masuala muhimu ya kimazingira, kijamii na kiutawala, ushirikishwaji wa wadau, usimamizi wa takwimu za ESG, pamoja na namna ya kuandaa na kuratibu uripoti wa uendelevu ndani ya taasisi.
Aidha, mafunzo hayo yameweka msingi wa kuanza kwa vikao na shughuli za vitendo vitakavyowezesha maandalizi ya Sera ya ESG, Mfumo wa ESG na Ripoti ya kwanza ya Uendelevu ya NEMC. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa masuala ya ESG yanaendelea kujumuishwa katika mipango, shughuli na mifumo ya utendaji wa Baraza.
Kupitia hatua hiyo, NEMC inaendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa mazingira, ufanisi wa kitaasisi, uwajibikaji na uwazi, sambamba na kuchangia katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na vipaumbele vya taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni