Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeshiriki katika Mkutano wa majadiliano kuhusu Fedha za Tabianchi (Climate Finance Roundtable) uliofanyika tarehe 5 Oktoba 2026 katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dar es Salaam.
Mkutano huo umewakutanisha wadau kutoka Serikali, taasisi za fedha za kimataifa, washirika wa maendeleo, sekta ya fedha na sekta binafsi kujadili namna ya kuongeza upatikanaji na uhamasishaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza uchumi wenye ustahimilivu.
Mkutano huu umefanyika katika wakati muafaka ambapo Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa zinaendelea na maandalizi kuelekea Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) utakaofanyika mwezi Novemba 2026 jijini Antalya, Türkiye. Hivyo, majadiliano haya yanatoa fursa muhimu ya kuimarisha vipaumbele vya Tanzania katika eneo la fedha za tabianchi na kuendeleza mikakati ya kuvutia rasilimali zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Ushiriki wa NEMC katika mkutano huo unaendeleza mchango wa
Baraza katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa ya mabadiliko ya
tabianchi, uandaaji na usimamizi wa miradi ya tabianchi, pamoja na jitihada za
kuongeza upatikanaji wa fedha za kimataifa kwa ajili ya utekelezaji wa hatua za
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

.jpeg)

.jpeg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni